Ili ufanikiwe, unahitaji kufanya vitu tofauti na ulivyozoea kufanya, kwa namna tofauti na ulivyozoea, unahitaji kujituma na kujisukuma zaidi ya ulivyozoea.
Wengi wanashindwa siyo kwa sababu hawawezi kufanya hayo, bali ni kwa sababu hawapo tayari kufanya. Hawapo tayari kujisukuma, hawapo tayari kuumia zaidi.
Wengi wanakuwa wameridhika na kile ambacho tayari wanacho, na hawaoni haja ya kujisukuma zaidi.
Unaweza kuona hili ni kawaida, lakini ukiangalia kwa ndani, utagundua ni ubinafsi wa hali ya juu.
Kama kuna kitu unaweza kufanya, ambacho kingekuwa na msaada kwa wengine, lakini hukifanyi, huo ni ubinafsi na utakuzuia wewe kufanikiwa zaidi.
Kwa mfano una wazo fulani la biashara, ambalo linaweza kuwasaidia watu wengi sana, lakini pia una kazi ambayo tayari inakupa kipato cha kuendesha maisha yako, unaweza kuachana na wazo hilo kwa sababu tayari una kazi. Lakini utakuwa umewanyima watu fursa ya kuwa na maisha bora zaidi na wewe utakuwa umejinyima nafasi ya kuongeza kipato chako zaidi.
Kufanya kwa mazoea na kuepuka kujisukuma na kujiumiza zaidi ni ubinafsi. Kuona mwili wako ni wa kipekee na usiohitaji kuchoshwa ni ubinafsi na kikwazo kikubwa kwa mafanikio yako.
Kila ukiangalia waliofanikiwa zaidi na wale ambao hawajafanikiwa, hakuna tofauti kubwa kwenye uwezo, tena wakati mwingine wanaofanikiwa zaidi wanakuwa na uwezo mdogo kuliko ambao hawajafanikiwa.
Kinachowatofautisha watu hawa ni kimoja, utayari wa kuchukua hatua kwenye mawazo ambayo wanayo na ung’ang’anizi walionao baada ya kuwa wamechukua hatua.
Ubinafsi ni sumu kubwa sana kwenye mafanikio yako na hata ya wengine. Kwa sababu unapojionea huruma, unapojiepusha na magumu, unajiepusha na mafanikio pia.
Na njia ya uhakika ya wewe kufanikiwa, ni kuwawezesha wengine kufanikiwa pia. Utafanikiwa kwa kadiri unavyowawezesha wengi zaidi kufanikiwa na kuwa na maisha bora.
Hivyo kama unachofanya kwenye maisha yako ni kujiangalia wewe tu, kuridhika na kidogo ulichopata na kutokujisukuma zaidi, unakuwa umejiweka kwenye kundi la wasiofanikiwa kabisa.
Uwezo tayari upo ndani yako, tena mkubwa kuliko unavyofikiri. Unaweza kukabiliana na magumu kuliko unavyodhania, lakini hutaweza kujua hayo mpaka pale utakapochukua hatua kwenye maisha yako.
Huwezi kujua ni umbali kiasi gani unaweza kwenda, mpaka utakapoanza kwenda mbali zaidi ya ulivyozoea kwa sasa. Huwezi kujua ni magumu kiasi gani unayoweza kukabiliana nayo mpaka pale utakapokabiliana na magumu zaidi ya uliyozoea kukabiliana nayo.
Njia pekee ya kuondokana na ubinafsi, njia ya kutengeneza mafanikio makubwa, ni kutumia kila uwezo ambao upo ndani yako. Hakikisha kila kilichopo ndani yako umekitumia kabla hujaondoka hapa duniani. Maana kila ulichonacho, hukupewa ili ukitunze badala yake ni ili ukitumie.
Tumia uwezo uliopo ndani yako na utaweza kufanya makubwa kwako na kwa wengine pia.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,