Kipimo bora sana unachopaswa kutumia kwa mafanikio yako, ni matokeo unayopata, na siyo nguvu wala muda, bali matokeo.
Watu wengi wanapenda kutumia muda au nguvu wanazotumia kufanya kitu kama kipimo au kama njia ya kuonekana wanafanya sana. Ni rahisi kutumia njia hii, kwa sababu unaweza kuigiza kwa njia hii.
Lakini maigizo hayatakuletea mafanikio unayopata, kitu pekee kitakacholeta mafanikio ni matokeo unayopata. Hivyo kama utaanza kupima kila kitu kwa matokeo unayopata, itakuwa rahisi kwako kujua maeneo gani ya kuweka juhudi zaidi ili kuweza kupata matokeo zaidi.
Kama umeweka nguvu kubwa na kutumia muda mwingi, lakini ukapata matokeo madogo sana, kuna tatizo mahali, lazima uliangalie ili uweze kufika kule unakotaka kufika.
Kama unaweka juhudi kutoa huduma bora sana kwenye biashara yako, na unakazana kuwafikia wateja wengi zaidi wa biashara yako, lakini mauzo ni madogo, kuna tatizo mahali. Haijalishi unakaa kwenye biashara yako kwa masaa mengi kiasi gani, au unakazana kwa kiasi gani, kama mauzo ni madogo, huwezi kupiga hatua.
Hivyo kabla hujakazana kuweka juhudi zaidi, kabla hujataka kupata sifa kwa juhudi kubwa unazoweka, angalia kwanza matokeo unayozalisha, kama siyo mazuri, kuna tatizo kwenye juhudi unazoweka, huenda siyo sahihi au hujaziweka kwenye eneo sahihi.
Na hii ndiyo maana ni muhimu sana kwako kugawa malengo yako makubwa kwenye malengo madogo madogo ambayo yanapimika na kukamilika kwa muda mfupi. Hii inakuwezesha kupima mapema matokeo unayopata kabla hujaweka juhudi kubwa na kupata matokeo mabaya.
Unapokuwa umeweka malengo madogo madogo, mfano ya siku, kisha mwisho wa siku ukajipima kwa matokeo uliyopata, ni rahisi kurekebisha kwa siku inayofuatia kama matokeo unayopata siyo sahihi kukufikisha kwenye malengo yako makubwa.
Kitu kingine muhimu sana, hasa kwenye dunia ya sasa, dunia ya kutambiana kwenye mitandao nani anafanya zaidi, unaweza kuachana na matambo hayo na wewe ukafanya kazi yako, na ukaacha matokeo yaseme yenyewe.
Pima kila unachofanya kwa matokeo unayopata, juhudi na muda ni muhimu, lakini usipopima kwa matokeo unayopata, juhudi na muda wako utapotea bure.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,