“Whenever we give up, leave behind, and forget too much, there is always the danger that the things we have neglected will return with added force.” — Carl Jung

Hongera sana mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi nyingine nzuri na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari UNACHOKIPUUZA, KITARUDI KWA NGUVU KUBWA.
Kuna vitu ambavyo huwa tunavipuuza kwenye maisha,
Vitu vidogo ambavyo tunaona havina madhara makubwa kwetu kwa sasa.
Na hivyo hatuvipi uzito unaostahili.
Kwa kuvipuuza, vitu hivyo vinapotea kwenye mawazo yetu, lakini vinaendelea kuwepo, na mbaya zaidi vinaendelea kukua zaidi.

Baadaye vitu hivi vinarudi kwetu vikiwa na nguvu kubwa sana ambayo hatuwezi kukabiliana nayo.
Nguvu hiyo inakuwa ni kubwa sana kiasi cha kutushinda.

Angalia mfano wa magonjwa, huwa yanaanza kidogo kidogo na ya kuvumilika, lakini baadaye yanakuwa makubwa na sugu.
Mfano mwingine ni changamoto za kifedha kama madeni, yanaanza kidogo kidogo, baadaye yanakuwa makubwa na mtu anakuwa kwenye matatizo makubwa kifedha.
Hata vitu kama mahusiano, yanaweza kuwa yanadorora kidogo kidogo na siku mtu unastuka yameshafikia hatua ambayo hayawezi kuendelea tena, yanavunjika.
Kadhalika kwenye biashara, hakuna biashara inayokufa siku moja, biashara inaanza kudorora kwa muda lakini inapuuziwa, inafika siku haiwezi kuendelea tena na haiwezi kuponeshwa.

Kitu chochote ambacho ni muhimu kwa maisha yako, kipe uzito unaostahili.
Usipuuze chochote hata kama ni kidogo kiasi gani. Kama kinahusisha eneo muhimu la maisha yako, kifanyie kazi wakati bado ni kichanga.
Chochote unachoona hakipo sawa, kipe uzito, usijiambie ni kitu kidogo na kitaisha, jiridhishe kwa kukifanyia kazi kikiwa bado ni kidogo.

Mara zote na kwenye maeneo yote, kinga ni bora na nafuu kuliko tiba. Ukiwa mtu wa kufuatilia kwa umakini yake ambayo ni muhimu kwako, utaweza kujikinga na mengi.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuchukua hatua mapema kabla mambo hayajaharibika.
#Fanya #HakunaSababu #NiLeoTu #IngiaMzimaMzima #AnzaNaHatuaMoja #MafanikioNiHakiYako #NidhamuMsingi #WhatEverItTakes #WachaManenoWekaKazi #SkinInTheGame #OwnTheDayOwnYourLife #UsileteSababuLetaMatokeo #MudaNiSasa

Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha