Hii ni siku nyingine mpya kwetu,
Ni siku ambayo tuna nguvu ya kuitumia vile tunavyotaka.
Tunaweza kuitumia siku ya leo kupiga hatua zaidi kuelekea kwenye ndoto zetu.
Au tunaweza kuipoteza siku hii kwa kuwa bize na mambo ambayo hayana mchango wowote kwenye kufikia ndoto zetu.
Kama utaianza siku ya leo kwa habari, utatumia muda wako kuperuzi mitandao ya kijamii, utaingia kwenye mabishano kuhusu michezo, siasa, wasanii au chochote kile, umechagua kupoteza siku yako.

Nina imani kama unasoma hapa, hutafanya hayo ya kupoteza muda wako. Na kama utafanya, basi utajiadhibu mara moja ili usirudie tena kupoteza muda wako.
Tunakwenda kuiishi siku yetu hii ya leo kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA ambapo tutaweza kufanya makubwa sana leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari KINACHOKUSUMBUA NI KUKOSA MSIMAMO…
Rafiki, umewahi kujiambia utafanya kitu fulani au hutafanya kitu fulani, lakini baadaye ukajikuta umefanya tofautinna ulivyopanga?
Labda umejiambia utawahi kuamka, halafu ukachelewa,
Au unajiambia utaacha kupoteza muda, halafu unaupoteza,
Au unajiambia utakuwa na nidhamu kwenye matumizi yakonya fedha, halafu unazitumia vibaya.
Inawezekana pia umewahi kujiambia hutakunywa tena pombe, au kula vyakula visivyo vya afya, lakini ukafanya tena hivyo.

Nini kinasababisha yote haya, inawezekanaje mtu mzima kama wewe na mwenye uelewa kabisa na maisha yako, na unayetaka kufanikiwa, upange kufanya kitu fulani lakini ufanye kingine tofauti kabisa?

Tatizo ni moja tu, kukosa msimamo.
Msimamo ni pale unaposhikilia kile ulichoamua, bila ya kutetereka, ni pake unapofanya ulichopanga, hata kama mambo ni magumu kiasi gani. Msimamo ni pale unapochagua kuacha kusikiliza sauti zozote zinazokwenda kinyume na mipango yako na kujikumbusha maamuzi yako kila wakati.

Unakosa msimamo pale unapopanga kitu, halafu unapoanza kutekeleza unakutana na ugumu, kisha unajishawishi kwamba siyo lazima kuendelea.
Au unajidanganya kuacha mara moja au kujaribu kile ulichoacha mara moja hakuna ubaya.
Na hakuna ubaya pale unapojiambia, lakini ukishafanya, ubaya ndiyo utauona.

Ukishavunja msimamo wako mmoja, kwanza unajidharau, pili inakuwa rahisi kwako kuvunja msimamo mwingine na mwingine na mwingine. Baada ya muda unajikuta huna msimamo tena na hujiheshimu tena, hivyo maamuzi yoyote unayofanya, huyaheshimu tena, unayavunja baada ya muda mfupi.

Anza leo kujenga upya msuli wako wa msimamo,
Anza na vitu vidogo kisha endelea kukua.
Jiambie leo hutafuatilia habari yoyote ile, na usivunje hilo.
Jiambie leo hutatembekea mtandao wowote wa kijamii na simamia hilo.
Jiambie leo hutabishana na yeyote kwa jambo lolote na jisimamie kwa siku nzima.
Utapata msukumo ndani yako wa kujaribu mara moja tu, kuchungulia kidogo tu ili usipitwe, puuza msukumo huo na simamia maamuzi yako.
Utajiheshimu sana ukiweza kusimamia chochote ulichopanga.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kufanya maamuzi na kuyasimamia bila ya kuyavunja hata kama unashawishika kiasi gani.
#Fanya #HakunaSababu #NiLeoTu #IngiaMzimaMzima #AnzaNaHatuaMoja #MafanikioNiHakiYako #NidhamuMsingi #WhatEverItTakes #WachaManenoWekaKazi #SkinInTheGame #OwnTheDayOwnYourLife #UsileteSababuLetaMatokeo #MudaNiSasa

Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha