Zama hizi, kila mtu anajiita mjasiriamali.
Hakuna ubaya kwa watu kujiita wajasiriamali, lakini wanapaswa kujua maana ya ujasiriamali kabla ya kutumia neno hilo. Ili hata kama bado hawajafikia kwenye ujasiriamali wenyewe, wajue ni wapi na wakazane kufika hapo.
Mjasiriamali ni mtu ambaye anatengeneza biashara na biashara ni mfumo ambao unajiendesha wenyewe unaozalisha fedha kwa mmiliki wa mfumo huo. Kwa kuelewa hili vizuri, utaweza kujiweka sehemu sahihi na kutengeneza kipato huku ukiwa na uhuru wako.
Watu wengi waliopo kwenye biashara na wanaojiita wajasiriamali siyo wajasiriamali kwa sababu hawawezi kutenganishwa na biashara zao. Biashara wanazofanya zinawategemea wao kwa asilimia 100, wasipokuwepo biashara haziendi. Lakini mjasiriamali anatengeneza mfumo wa biashara ambao unaweza kujiendesha wenyewe, hata kama yeye hayupo.
Kwa kuelewa hili, sasa tunapata kazi kuu ya mjasiriamali, ambayo ni kutengeneza mfumo utakaoiwezesha biashara kujiendesha yenyewe, hata kama yeye hayupo. Hii ndiyo kazi kuu, na kazi ambayo ni ngumu, ndiyo maana wengi hawaifanyi.
Kama mjasiriamali unahitaji kufanya kazi hii ngumu mwanzoni mwa biashara ili mfumo unapokuwa umekomaa, biashara yako inakwenda vizuri bila ya tatizo lolote, hata kama wewe haupo moja kwa moja.
Kama mjasiriamali, mara zote unapaswa kufanya yale majukumu magumu ya biashara yako, huku ukiwapa wengine yale rahisi wafanye. Na lengo la kufanya hayo magumu siyo kuwa mfanyaji wa hayo muda wote, bali kuyatengenezea mfumo mzuri wa kuwawezesha wengine kuyafanya pia.
Usichochwe na kufanywa mtumwa wa biashara yako, kama lengo lako ni kuwa mjasiriamali. Badala yake tengeneza mfumo ambao utaiwezesha biashara yako kujiendesha yenyewe bila ya wewe kuwepo moja kwa moja.
Watu wengine wamezoea kusema ujasiriamali ni sawa na kumiliki mashine inayochapisha fedha, mashine hiyo ni biashara. Biashara inapoweza kujiendesha yenyewe na kwa faida, hapo mjasiriamali anakuwa na mafanikio makubwa.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,