“Only human beings can reorder their lives any day they choose by refining their philosophy.” – Jim Rohn
Hongera sana mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari UNAWEZA KUBADILI MAISHA YAKO LEO…
Uzuri na upekee wa kuwa binadamu ni kwamba tunayo mamlaka ya kuyafanya maisha yetu vile ambavyo tunataka sisi wenyewe.
Huu ni upendeleo ambao hakuna kiumbe hai mwingine ambaye anao.
Mti ukiota eneo ambalo siyo zuri, hauwezi kuamua kuhama na kwenda eneo jingine, utajitahidi kupeleka mizizi mbali uwezavyo lakini kuondoka wenyewe hauwezi.
Lakini wewe mwanadamu ukijikuta sehemu ambayo haikufai, unao uwezo wa kuondoka sehemu hiyo na kwenda sehemu inayokufaa.
Hii ni furaa nzuri sana na ya kipekee, ambayo siyo kila kiumbe anayo, lakini wengi hawaitumii.
Utawakuta watu wanalalamikia mazingira yao, kazi zao, biashara zao na hata mahusiano yao na wengine.
Wanaishia tu kulalamika na kuendelea na kile wanacholalamikia, badala ya kuchukua hatua ya kubadili kile ambacho hakipo sawa.
Unaweza kubadili maisha yako leo, unaweza kubadili maisha yako wakati wowote kwa kubadili falsafa yako kwenye eneo la maisha yako.
Kuna falsafa fulani unazifuata kwenye kila eneo la maisha yako, iwe unajua au hujui. Sehemu ya kwanza ya madabiliko ni kubadili falsafa hizi.
Kama kazi yako inakusumbua na haikulipi vizurim huenda falsafa unayoisimamia ni kufanya kidogo kwa sababu unalipa kidogo. Kama ukibadili falsafa hiyo na kuwa unafanya zaidi ya unavyolipwa, si muda utaanza kukipwa zaidi.
Kadhalika, kama kila ukipata fedha hazitulii, huenda falsafa uliyonayo kwenye upande wa fedha ni ukipata fedha unatumia mpaka ziishe, huenda unapanga kuweka akiba baada ya matumizi na pia huenda fedha zikiisha unakopa.
Kwa kubadili falsafa yako kwenye matumizi ya fedha, kwa kuanza kuweka akiba kabla ya matumizi na matumizi kuwa chini ya mapato, utapunguza changamoto zako za kifedha.
Rafiki, kama kuna eneo kwenye maisha yako linakusumbua, haliendi sawa, basi anza na falsafa uliyonayo kwenye eneo hilo. Ukibadili falsafa, utaweza kubadili maisha yako wakati wowote ule.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kubadili falsafa za maisha yako ili kuweza kuwa na maisha bora sana kwako.
#Fanya #HakunaSababu #NiLeoTu #IngiaMzimaMzima #AnzaNaHatuaMoja #MafanikioNiHakiYako #NidhamuMsingi #WhatEverItTakes #WachaManenoWekaKazi #SkinInTheGame #OwnTheDayOwnYourLife #UsileteSababuLetaMatokeo #MudaNiSasa
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha