Siku mpya,
Siku bora na ya kipekee sana kwetu.
Ni nafasi nzuri kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa kwenye kila tunachofanya ili tuweze kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari UNAHITAJI NGUVU YA NJE…
Ili kuweza kupiga hatua kubwa, ili kuweza kufanikiwa zaidi, unahitaji nguvu ya nje.
Nguvu yako ya ndani inakuwezesha kupanga na kuanza, lakini pale unapokutana na magumu, pale unapokutana na changamoto, nguvu ya ndani inafifia na inakuwa rahisi kukata tamaa.
Lakini ukiwa na nguvu ya nje, inakusukuma zaidi na utaweza kuvuka kila aina ya ugumu na kufika unakotaka kufika.
Angalia kwenye maisha yetu ya kila siku, jinsi nguvu ya ndani isivyotosheleza;
Watu huwa hawafanyi kitu mpaka tarehe ya mwisho ifikie,
Wanafunzi hawasomi kwa juhudi mpaja mtihani ukaribie,
Watu huwa hawachukui hatua na umakini mpaka wasaini mkataba,
Watu hufanya zaidi pale wanapojua wengine wanawaangalia.
Kwenye kila eneo la maisha, ukiwa na watu wawili, mmoja ana nguvu ya ndani pekee na mwingine ana nguvu ya ndani na ya nje, mwenye nguvu ya ndani na nje atafanikiwa zaidi kuliko mwenye nguvu ya ndani pekee.
Hivyo rafiki, kwa mafanikio makubwa unayotaka kufikia, hakikisha ipo nguvu ya nje inayokusukuma zaidi.
Na hapa ndipo unapohitaji kuwa na mtu wa kukusimamia kwa karibu.
Unahitaji kuwa na kocha au menta au mshauri au watu wengine unaoshirikiana nao, ambao hawatakuachia kirahisi pale unapotaka kukata tamaa.
Unaweza pia kutoa ahadi kubwa kwa watu, ambayo itakuwa aibu kubwa kwako kama hutaitekeleza.
Kwa vyovyote vile, kazana sana uwe na nguvu ya ndani na ya nje pia, zitakusaidia sana kuweza kifikia mafanikio makubwa.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kutumia nguvu ya ndani na ya nje kuweza kufanya makubwa zaidi.
Tumia nguvu ya nje leo kwa kuorodhesha yote unayopanga kufanya leo na kupangilia kila saa yako ya leo. Kisha mshirikishe mtu mpango huo na akusimamie mpaka uutekeleze.
#Fanya #HakunaSababu #NiLeoTu #IngiaMzimaMzima #AnzaNaHatuaMoja #MafanikioNiHakiYako #NidhamuMsingi #WhatEverItTakes #WachaManenoWekaKazi #SkinInTheGame #OwnTheDayOwnYourLife #UsileteSababuLetaMatokeo #MudaNiSasa
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha