Watu wote unaojihusisha nao kwenye maisha yako, wanaweza kugawanyika kwenye makundi mawili.
Kundi la kwanza ni wale watu ambao wanakusukuma ili uweze kupiga hatua zaidi. Hawa ni watu ambao wanapenda kuona unafanikiwa, wanataka uwe bora zaidi na ufike kule unakotaka kufika. Kundi hili lina watu wachache sana, na huenda ukawa huna kabisa watu wa aina hii kwenye maisha yako.
Kundi la pili ni wale watu ambao wanakuvuta ili usiweze kupiga hatua, hawa wanahakikisha huendi mbele zaidi. Ni watu ambao hawataki kuona ukifanikiwa, kwa sababu kufanikiwa kwako kutawafanya wao waonekane ni wazembe, au utawaacha nyuma. Kundi hili lina watu wengi sana, watu unaowapenda na kuwajali sana, na wana hatari kubwa ya kukuzuia wewe usifanikiwe kabisa.
Watu wote unaojihusisha nao, watakuambia wapo nyuma yako linapokuja swala la mafanikio, lakini hawatakuambia nyuma yako wanafanya nini. Maana kusukuma na kuvuta kote kunafanyika ukiwa nyuma ya mtu.
Hivyo usifurahie tu pale mtu anapokuambia nipo nyuma yako, badala yake angalia nyuma yako anafanya nini? Anakusukuma uende mbele zaidi au anakuvuta urudi nyuma.
Njia nzuri ya kujua nyuma yako mtu anafanya nini, ni kuangalia kwenye maisha yake binafsi anafanya nini. Kama yeye mwenyewe anakazana kupiga hatua zaidi, basi anakusukuma, lakini kama hapigi hatua, kama ameshakata tamaa basi huyo anakuvuta nyuma.
Watu wengi walioshindwa na kukata tamaa huwa wanapenda wengine nao washindwe, ili wahalalishe kushindwa kwao. Hawataweza kusema mambo ni magumu na hayawezekani, kama wewe utakuwa umeweza. Hivyo unapaswa kuwa makini sana na watu wanaokuambia wapo nyuma yako.
Kundi la watu ambao wanakuvuta usifanikiwe, ni kundi ambalo unapaswa kulifuta mara moja kwenye maisha yako, hawa ni watu unaopaswa kuwaepuka kama ukoma, kaa nao mbali sana.
Haijalishi unawapenda watu hawa kiasi gani, ni sumu kwa mafanikio yako, na sumu yao inaambukizwa hata kwa mbali. Hata kama unajiambia utakuwa nao lakini hutawasikiliza wanachosema, kitendo cha kuwa tu karibu na watu hawa, kinakuambukiza sumu walizobeba ndani yao.
Kwanza kabisa wewe unapaswa kuwa bize, unapaswa kuwa umetingwa sana kukazana kupiga hatua kiasi kwamba hupati muda kwa ajili ya wale ambao hawana makubwa wanayofanya na maisha yao.
Usiruhusu akili yako iingie wasiwasi wowote juu ya kile unachotaka, utakutana na magumu, lakini haimaanishi ndiyo mwisho wa safari. Na ni kweli kabisa kwamba mafanikio ni magumu, lakini je unataka kuendelea kuambiwa hilo kila siku na watu ambao wameshindwa?
Huhitaji kukumbushwa kila siku, unahitaji kuwa na muda wa kuweka juhudi kubwa, na ndiyo maana unapaswa kuwapunguza wale wasiokuwa na mchango mkubwa kwenye mafanikio yako.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,