Rafiki yangu mpendwa,
Kila mtu anapenda kuwa na furaha kwenye maisha, lakini ambacho nakiona kwa wengi ni hawajui kutofautisha raha na furaha. Wengi wanahangaika na vitu vitakavyowapa raha, lakini haviwapi furaha.
Kwa kuanza na tofauti ya msingi kabisa, raha ni hisia nzuri unayoipata kwa muda mfupi, mfano hisia unayoipata baada ya kula kitu kitabu, kufanya mapenzi, kutumia kilevi au unapopata kitu ulichokuwa unakitaka sana kwa mara ya kwanza. Hisia hii haidumu kwa muda mrefu, huwa inaisha baada ya tukio lililoleta raha hiyo kuisha.
Furaha ni hisia ya muda mrefu, ni hisia inayoanzia ndani ya mtu, kulingana na mtazamo na fikra alizonazo juu ya maisha yake. Furaha huwa inaanzia ndani na haitegemei kupata kitu fulani au kutumia kitu fulani. Furaha inaanza na mtu mwenyewe kwa namna anavyochukulia maisha yake.
Watu wengi wanavurugwa sana pale wanapokimbizana na vitu fulani wakiamini vitawaletea furaha. Mfano mtu ambaye siyo tajiri, anakazana sana apate utajiri na kujiaminisha kwamba akipata utajiri basi atakuwa na furaha sana kwenye maisha yake. Ni mpaka pale mtu huyo anapopata utajiri na kugundua hakuna kikubwa kimebadilika kwenye maisha yake.
Siyo mafanikio au utajiri unaoleta furaha, bali ni furaha ndiyo inaleta mafanikio na utajiri. Kwa maana nyingine kama huna furaha wakati huna utajiri, basi jua kwamba hata ukiwa na utajiri bado hutakuwa na furaha.
Najua swali unalojiuliza sasa ni je furaha inatengenezaje? Kama haitokani na mafanikio wala utajiri, je mtu unawezaje kuwa na furaha kwenye maisha?
Jibu lipo hapa, jibu ni kwamba kuna viungo vitatu muhimu sana kwa furaha ya kudumu kwenye maisha yako. Kwenye makala hii tunakwenda kujifunza viungo hivi kwa undani na jinsi ya kuvitumia ili kuwa na furaha zaidi.
Kiungo cha kwanza; ustadi.
Kiungo cha kwanza na muhimu sana cha furaha ni ustadi, umahiri katika jambo fulani unalofanya kwenye maisha yako. Mtu unakuwa na furaha pale unapojua kwamba kuna kitu unaweza kukifanya vizuri na kikawa na msaada kwenye maisha ya wengine.
Mtu unakuwa na furaha pale unapofanya kitu chenye maana kwako na kuweza kukifanya kwa ustadi na umahiri wa hali ya juu. Hata kama kitu ni kigumu kiasi gani, unapoweza kukifanya vizuri, unajijengea kuridhika ndani yako na hiyo ndiyo inakufanya uwe na furaha ya kudumu.
Ukitaka kudhibitisha hili angalia watu ambao wanapata fedha nyingi bila ya kufanya kazi. Labda wameshinda bahati nasibu au wamepata urithi, maisha yao huwa mabovu sana licha ya kuwa na fedha nyingi. Ni kwa sababu wanakuwa hawajafanya kitu kikubwa kupata fedha hizo, na wengi huishia kuzipoteza.
Ufunguo wa furaha; chagua kitu au eneo utakalokuwa na ustadi nalo kwenye maisha yako, eneo ambalo utafanya vizuri na utaongeza thamani kwenye maisha ya wengine. Kama ni mwalimu fundisha vizuri sana, kama daktari tibu vizuri, kama mwandishi andika vizuri vitu vinavyowasaidia watu. Kadhalika kwenye kilimo, ufundi, uwakili na ujuzi mwingine wowote.
SOMA; Mbinu Nane (8) Za Kuanza Siku Yako Kwa, Furaha, Hamasa Ya Hali Ya Juu Ili Kuwa Na Mafanikio Makubwa.
Kiungo cha pili; mahusiano chanya.
Kiungo cha pili cha furaha ni mahusiano chanya uliyonayo. Mahusiano yetu na wengine yana mchango mkubwa sana wa namna maisha yetu yanavyokuwa. Kama utakuwa na mahusiano chanya, mahusiano ya kuelewana na wale watu unaojihusisha nao, mahusiano ya kujaliana, mahusiano ya kuwa tayari kutoa zaidi, kwa kuhusiana na wanaotoa zaidi, basi maisha yako yatakuwa ya furaha.
Kitendo cha kujua kuna watu wapo kwa ajili yako, na wewe upo kwa ajili ya wengine kinakufanya uridhike na maisha na kuwa na furaha.
Kwa upande mwingine mahusiano hasi, yasiyo na maelewano, yenye msuguano mara zote, ni chanzo cha kukosa furaha kwa wengi.
Ufunguo wa furaha; tengeneza mahusiano chanya kwenye maisha yako, chagua wale watu ambao ni wa muhimu kwako na unapenda kuwa na mahusiano bora na wao, kisha wape muda na wajali zaidi. Kuwa tayari kujitoa zaidi kwa ajili yao, na wao watakuwa tayari kujitoa kwa ajili yako.
Kiungo cha tatu; uhuru.
Wapo watu ambao wameajiriwa na wanalipwa mshahara mkubwa sana, kipato chao kinawawezesha kupata chochote wanachotaka, kwa upande wa kipato, lakini bado wanakosa furaha kwenye maisha yao. Na sababu kubwa ni kukosa uhuru wa maisha yao. Kwa sababu kadiri mtu anavyolipwa, ndivyo anavyotumika zaidi. Kadiri kipato cha ajira kinavyokuwa kikubwa, ndivyo majukumu yanakuwa mengi na kutegemewa kuwa tayari na kazi wakati wowote. Mtu hawezi kuchagua afanye nini na maisha yake, ni mpaka aombe ruhusa kwanza.
Uhuru ni kiungo muhimu sana cha furaha, huwezi kuwa na furaha kama huna uhuru.
Na uhuru siyo kwenye eneo la fedha na kazi pekee, bali hata kwenye fikra za wengine. Kama una chuki na wengine haupo huru, hivyo huwezi kuwa na furaha. Kama unashindana na wengine huwezi kuwa huru, kwa sababu muda wote utakuwa unawaangalia wanafanya nini.
Ili kuwa na furaha ya kudumu kwenye maisha yako, lazima uwe na uhuru na maisha yako. Kadiri unavyokuwa huru, ndivyo unavyokuwa na furaha.
Ufunguo wa furaha; tengeneza uhuru kamili kwenye maisha yako, ondoa utegemezi wako kwa wengine au vitu fulani ndiyo maisha yako yakamilike. Hata kama huna kila unachotaka, kitendo cha kuwa huru na muda wako na maisha yako, kinakuwezesha kuwa na furaha ya kudumu kwenye maisha yako.
Rafiki, hivyo ndiyo viungo vikuu vitatu vya furaha ya kudumu kwenye maisha yako. Kama unavyoona, viungo vyote vitatu havianzii nje au kwenye vitu ulivyonavyo, bali vinaanzia ndani yako. Hii ina maana kwamba, unaweza kuwa na furaha kwenye wakati wowote wa maisha yako, bila ya kujali una nini. Kuwa na ustadi kwenye eneo lako, tengeneza mahusiano chanya na kuwa na uhuru, hivi vitakupa furaha ya kudumu kwenye maisha yako.
Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha
Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; http://eepurl.com/dDZHvL