Rafiki yangu mpendwa,

Juma namba 44 kwa mwaka huu 2018 ndiyo linatuacha. Ni juma ambalo kwangu binafsi nimekuwa na majumu mengi sana, lakini nashukuru sana maana yote yamekamilika kwa mafanikio makubwa sana.

Jana tulikuwa na SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA 2018 ambayo ilianza saa moja asubuhi mpaka saa mbili usiku na leo nilikuwa na vikao mbalimbali muhimu pia vilivyochukua siku yangu nzima. Pamoja na hayo mengi, ambayo yangetosha kunipa sababu ya kweli kabisa ya kutokuandika TANO HIZI ZA JUMA, nimejikumbusha ahadi yangu kwako ya kukushirikisha haya matano muhimu kila mwisho wa juma.

Hivyo karibu sana kwenye tano za juma hili la 44, nimekuandalia matano muhimu sana kwa juma hili, yasome, yatafakari, kisha nenda kayaishi kwa juma linalokuja.

Rafiki, kanuni yetu ni moja, MAARIFA SAHIHI + KUCHUKUA HATUA KUBWA = MAFANIKIO MAKUBWA. Jifunze na chukua hatua, na kamwe hutabaki pale ulipo sasa.

#1; MATUKIO YA SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA 2018.

Rafiki, kama ambavyo nilikuwa nakupa taarifa kwa zaidi ya miezi mitatu, SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA 2018 ilifanyika jana tarehe 03/11/2018.

Semina hii imeweza kufanyika kwa mafanikio makubwa sana na washiriki wote wamekiri kuondoka na mafunzo na hamasa ya kwenda kuchukua hatua kubwa zaidi kwenye maisha yao.

Ni semina iliyochukua siku nzima, na tulishirikishana maarifa muhimu sana kwa maisha ya mafanikio.

Pia tulijadili kwa kina changamoto kubwa kumi zinazowazuia wengi kufanikiwa, na kupata mikakati ya kwenda kufanyia kazi.

Wapo wanamafanikio ambao wamepata nafasi ya kufanya kazi na mimi moja kwa moja katika kukuza zaidi biashara zao kwa kipindi cha mwaka mzima wa mafanikio 2018/2019.

Kitu kikubwa sana nilichojifunza ni jinsi ambavyo nguvu ya kukutana pamoja inavyokuwa na mabadiliko makubwa kwa mtu.

Mmoja wa washiriki wa semina, ambaye alikuwa na wasiwasi sana kabla ya kulipia, akijiuliza kama kuna kipya cha kujifunza kwa kuja kwenye semina, baada ya semina aliniambia, “kocha naomba ufanye semina hizi za kukutana ana kwa ana mara mbili kwa mwaka”. Unaweza kuona jinsi gani ushiriki wa semina ulivyo na nguvu kubwa.

Rafiki, hapa nimeambatanisha picha mbalimbali za matukio ya SEMINA HII KUBWA NA YA KIPEKEE KWA MAFANIKIO YETU.

Kama ulikosa semina hii rafiki, nina habari mbili kwako;

Habari ya kwanza ni kwamba umekosa mengi sana, siyo tu kwa kutokuwa kwenye semina, bali hata ile huduma ya karibu ambayo walioshiriki kwenye semina wataendelea kuipata kwa mwaka mzima.

Habari ya pili ni kwamba anza kujiandaa sasa kwa SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA 2019, kama changamoto ilikuwa ada ya kushiriki fungua kabisa akaunti maalumu ya SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA 2019, na kila mwezi kuanzia mwezi kuu weka shilingi elfu 30, ikiwa ni kutenga elfu moja kila mwezi. Kama huna nidhamu ya kufanya hilo, nakupa nafasi ya bure ya kukusimamia kwenye kutekeleza hilo, nijulishe. Kama kilichokuzuia ni ruhusa kwenye kazi, basi anza kabisa kuomba ruhusa sasa, au weka likizo yako ya kazi iwe kipindi cha semina ambapo mwaka 2019 itakuwa mwanzoni mwa mwezi oktoba.

Rafiki yangu, nikuambie kitu kimoja, usiruhusu chochote kikuzuie kushiriki SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA 2019, anza maandalizi sasa na mwakani tuwe pamoja.

DSC_0096DSC_0094DSC_0086DSC_0078DSC_0063DSC_0022SAMSUNG CAMERA PICTURESSAMSUNG CAMERA PICTURESDSC_0099DSC_0097

#2 MAKALA YA JUMA; MWAKA MPYA WA MAFANIKIO.

Rafiki, nimekuwa nakusisitiza kitu kimoja kuhusu kuweka malengo na mipango ya maisha yako ya mwaka; usifanye kosa la kuweka malengo wakati wa mwaka mpya.

Huu ni wakati ambao kila mtu hisia zinakuwa juu, anaweka mipango siyo kwa kufikiri, bali kwa hisia na hamasa. Kinachotokea muda siyo mrefu, pale hisia zinapotulia, wanaachana kabisa na malengo waliyoweka.

Hivyo nimekuwa nakuambia uuanze mwaka wako wa mafanikio mapema, na wakati mzuri wa kuuanza mwaka huu ni mwezi novemba. Hivyo rafiki, tumeshauanza MWAKA MPYA WA MAFANIKIO 2018/2019.

Kujua zaidi kuhusu mwaka huu mpya wa mafanikio, fungua hapa na usome; #ONGEA NA KOCHA; Uanze Mwaka 2019 Mapema Ili Uweze Kufanya Makubwa Na Kufanikiwa Zaidi.

Pia kama unataka kuwa na furaha ya kudumu kwenye maisha yako, hapa kuna viungo vitatu muhimu unavyopaswa kuvifanyia kazi; Hivi Ndiyo Viungo Vikuu Vitatu Vya Furaha Ya Kudumu Kwenye Maisha Yako.

#3 TUONGEE PESA; THAMANI INAYOZIDI FEDHA.

Rafiki, nimekuwa nakusisitizia mara zote kwamba fedha ni zao la thamani. Kwamba kama kipato unachoingiza sasa ni kidogo, basi jua pia thamani unayoitoa ni ndogo.

Na kama unataka kipato chako kiongezeke, basi sehemu ya kuanzia ni kwenye kuongeza thamani.

Sasa unapaswa kutoa thamani inayozidi fedha, na namna ya kufanya hivyo ni KUTOA THAMANI ZAIDI YA MATUMIZI KULIKO THAMANI YA FEDHA UNAYOPOKEA.

Yaani chochote unachofanya kwa wengine, chochote unachowauzia wengine, basi hakikisha kinakwenda kuwapa thamani kubwa kwenye kukitumia kuliko thamani waliyoitoa kwa fedha. Kwa njia hii utakuwa na wateja zaidi, ambao watataka kulipa zaidi na kipato chako kitaongezeka zaidi.

Mara zote jikumbushe kauli hii, TOA ZAIDI THAMANI YA MATUMIZI KULIKO UNAVYOPOKEA THAMANI YA FEDHA.

#4 HUDUMA NINAZOTOA; JIUNGE NA KISIMA CHA MAARIFA.

Rafiki, kama kuna kitu kimoja pekee ninachoweza kukusisitiza ufanye kama bado hujafanya, ni ujiunge na KISIMA CHA MAARIFA. Ninaweza kusema bila ya mashaka wala wasiwasi wowote kwamba kama hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA, hujitendei haki kwenye maisha yako.

Kwa sababu ndani ya KISIMA unapata nafasi ya kujifunza mengi sana, siyo kutoka kwangu tu, bali kutoka kwa jamii nzima ya wanamafanikio, watu ambao wamejitoa na wanapambana ili kufanikiwa. Hii ni jamii ya tofauti kabisa na jamii ulizozoea, jamii inayokupa moyo wa kufanikiwa na siyo kukukatisha tamaa, jamii iliyo tayari kukushirikisha chochote ambacho unahitaji kwa ajili ya mafanikio yako.

Rafiki, nakusisitiza, fanya ufanyavyo, lakini hakikisha unaingia kwenye KISIMA CHA MAARIFA, na ukishaingia usitoke, ng’ang’ana kuwepo maisha yako yote, ili kuendelea kuwa bora maisha yako yote.

Nimalize kwa kukuambia hili rafiki, yajayo kwenye KISIMA CHA MAARIFA, yanafurahisha na kuhamasisha sana, kama upo tayari, hakikisha unakuwa ndani ili usiyakose.

Tena ingia mapema ili tuuanze pamoja mwaka huu mpya wa mafanikio 2018/2019. Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA tuma ujumbe kwa njia ya wasap namba 0717 396 253. Karibu sana.

#5 TAFAKARI YA KUFIKIRISHA; MAISHA, KAZI NA KIFO.

“Work as though you would live forever, and live as though you would die today.” – Og Mandino

Fanya kazi kama utaishi milele, na ishi kama utakufa leo.

Sijui niongeze maneno gani hapa ambayo yatasisitiza hili zaidi, maana watu wengi wanayapoteza maisha yao kwa kutokufanya kazi na pia hata hawaishi. Yaani watu wengi utawakuta wapo wapo tu, yupo kazini na hafanyi kazi ya maana, yupo nyumbani lakini akili ipo kwingine, kinachotokea ni maisha ya mvurugano yaliyojaa msongo wa mawazo.

Unapofanya kazi, fanya kazi kweli, na unapoyaishi maisha yako, yaishi kweli, usiache chochote muhimu kwa ajili ya kesho, kwa sababu kuna siku utasema kesho na hutaiona kesho hiyo.

Ukawe na juma bora sana kwako rafiki yangu, juma la kufanya makubwa sana kwenye maisha yako ili kusogea karibu zaidi na ndoto zako.

Makala hii imeandikwa na Kocha Dr Makirita Amani.

Dr. Makirita ni Daktari wa binadamu, Kocha wa mafanikio, Mwandishi na Mjasiriamali.

Dr. Makirita anaendesha mafunzo ya mafanikio kwa wale waliojitoa hasa kufanikiwa kupitia program ya KISIMA CHA MAARIFA.

Kama bado hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA, tuma sasa ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa njia ya wasap namba 0717 396 253 (tumia wasap tu)

Kupata huduma nyingine za ukocha tembelea www.amkamtanzania.com/kocha

Kupata vitabu vizuri vya kusoma tembelea www.amkamtanzania.com/vitabu