Rafiki yangu mpendwa,

Furaha imekuwa mtego kwenye maisha ya watu wengi. Wengi huanza kufanya kitu fulani kwenye maisha yao, wakifikiri kwamba watakapomaliza kukifanya, au watakapopata wanachotaka basi watakuwa na furaha sana.

Lakini cha kushangaza pale mtu anapomaliza au anapopata anachotaka, anapata furaha inayodumu kwa muda mfupi sana. Na baada ya hapo anarudi kwenye hali yake ya kawaida, hali ya kujisikia vibaya na kama vile kuna utupu ndani yake.

Hili ni jambo linalowaumiza wengi, wasijue nini cha kufanya, kwa sababu wanakuwa wamekazana sana mpaka kupata walichopata, lakini furaha waliyotegemea kupata siyo.

Rafiki, mwandishi Loretta Graziano anatuambia hii ni hali ya kawaida kabisa, ambayo haipaswi kutushangaza. Badala yake tunapaswa kuizoea na kisha kuitumia vizuri ili kuweza kutengeneza furaha ya kudumu kwenye maisha yetu.

Loretta ni mtafiti na mwandishi kuhusu namna ubongo wa binadamu na wanyama unavyofanya kazi. Na amepata umaarufu kwa kitabu chake kinachoelezea kemikali nne za furaha ambazo zipo ndani ya kila mmoja wetu.

Anachotuambia Loretta ni kwamba, kama tukizijua vizuri kemikali nne zinazofanya kazi kwenye ubongo wetu, na kisha tukaweza kuzitumia vizuri basi tutaweza kuwa na furaha ya kudumu kwenye maisha yetu.

Tutaondoka kwenye ile hali ya kupata furaha inayodumu kwa muda mfupi na kisha kurudi kwenye hali ya kujisikia vibaya.

Kwenye kitabu chake cha HABITS OF HAPPY BRAIN, Loretta anatushirikisha tabia ndogo ndogo 18 za kuishi kila siku ambazo zitatuwezesha kuwa na furaha ya kudumu kwenye maisha yetu.

Kwenye makala hii nakwenda kukushirikisha tabia hizo 18, lakini kwanza nitaanza na utangulizi mfupi kuhusu kemikali nne za furaha zinazofanya kazi kwenye ubongo tulionao.

kemikalizafuraha

KEMIKALI NNE ZA FURAHA.

Zipo kemikali nne za furaha ambazo zinafanya kazi kwenye ubongo wa binadamu, kemikali hizi zinatolewa kwa misukumo tofauti lakini zote lengo ni kulete furaha na kujisikia vizuri.

Kemikali ya kwanza ni DOPAMINE, hii ni kemikali ambayo huachiliwa kwenye ubongo pale unapopata unachotafuta. Ndiyo maana unapopata kitu unachotafuta huwa unajisikia vizuri kwa muda mfupi.

Kemikali ya pili ni ENDORPHIN, hii ni kemikali ambayo huachiliwa kwenye ubongo ili kufubaza maumivu. Kemikali hii inazuia ubongo usikuambie kwamba kuna maumivu kwenye mwili.

Kemikali ya tatu ni OXYTOCIN, hii ni kemikali ambayo huachiliwa kwenye ubongo pale unapokuwa na mahusiano mazuri na wengine. Kemikali hii hutufanya tujisikie vizuri pale tunapokuwa ndani ya kundi au tunapokuwa na ushirikiano mzuri na wengine.

Kemikali ya nne ni SEROTONIN, hii ni kemikali ambayo huachiliwa kwenye ubongo pale ambapo mtu unakuwa umeheshimiwa na wengine. Kemikali hii inakufanya ujisikie vizuri pale wengine wanapokukubali na kukusifia kwa ulichofanya au kwa jinsi ulivyo.

Kemikali hizi nne zipo kwa wanyama wote na lengo lake ni kwa ajili ya kumwezesha mnyama kuepuka hali za hatari na kuwa na maisha salama.

SOMA; Hivi Ndiyo Viungo Vikuu Vitatu Vya Furaha Ya Kudumu Kwenye Maisha Yako.

Kwa nini furaha inadumu kwa muda mfupi?

Kama nilivyoanza kukueleza kwenye makala hii, kuna vitu unakazana kufanyia kazi au kuvipata, na unaweka juhudi kweli ukitegemea ukivipata utakuwa na furaha. Unapata kweli, lakini furaha unayopata haidumu kwa muda mrefu.

Kinachosababisha hali hii ni kwamba mwili huwa unaachilia kemikali hizi pale unapokuwa umekamilisha lile unalofanya, lakini kemikali hizi huwa zinavunjwa haraka sana kwenye mwili. Ndiyo maana furaha inadumu kwa muda mrefu.

Na ili furaha iweze kudumu kwa muda mrefu, unahitaji kuwa na njia ya kuuwezesha mwili kuachilia kemikali hizi kila mara, jambo ambalo ni gumu kwa maisha ya kawaida.

Ipo njia ya mkato ambayo watu wamekuwa wanatumia kuufanya mwili kuachilia kemikali hizi, na njia hiyo ni matumizi ya madawa ya kulevya. Madawa ya kulevya yanakwenda kufanya kazi kama kemikali hizi na hivyo huleta furaha sana. Mfano cocain huenda kufanya kazi ya dopamine na heroine huenda kufanya kazi ya endophin.

Lakini madawa ya kulevya yana madhara makubwa, kwa sababu ili uendelee kupata furaha inabidi uendelee kuongeza kiwango cha kutumia. Mfano unapoanza na kiasi kidogo, unasikia raha sana. Lakini ukiendelea kutumia kiasi kile kile, ubongo unazoea na hakuna tena furaha. Hivyo ili kupata furaha zaidi, inabidi uongeze kiwango kila mara, na hapa ndipo uteja unapotengenezwa.

Sasa rafiki yangu wewe huhitaji kutumia njia hii ya mkato ya kupata furaha ambayo itakuumiza baadaye.

Zipo njia za asili ambazo unaweza kuzitumia kupata furaha ambayo itadumu kwenye maisha yako na hakuna madhara ya baadaye.

Na hapa ndipo zinakuja tabia ndogo ndogo 18 ambazo tukiziishi kila siku zinatuletea furaha ya kudumu kwenye maisha yetu.

TABIA ZINAZOZALISHA DOPAMINE.

 1. Sherekea ushindi mdogo mdogo.

Badala ya kusubiri mpaka ufikie lengo kubwa ndiyo usherekee, gawa lengo hilo kwa hatua utakazochukua kila siku kisha sherekea pale unapokamilisha hatua hizo. Hili litakupa furaha kila siku kwa kukamilisha hatua hizo ndogo.

 1. Gawa lengo kubwa kwenye hatua ndogo ndogo.

Badala ya kuliendea lengo kwa ukubwa wake, ligawe kwenye hatua ndogo ndogo na kila unapomaliza hatua moja, unapata furaha na kupata msukumo wa kupiga hatua ya juu zaidi.

 1. Kwa jukumu kubwa ambalo ni gumu kufanya, ligawe kwenye muda mfupi mfupi.

Kila mtu huwa ana jukumu kubwa analotaka kufanya, lakini hawezi kulianza kwa kuwa ni kubwa na gumu, hivyo anaishia kuliahirisha kila mara. Tenga muda mfupi mfupi wa kufanya jukumu hilo na anza. Mfano weka dakika kumi tu za kufanya jukumu hilo kisha fanya kwa dakika hizo kumi. Kwa njia hii utaanza kuchukua hatua na dakika kumi zinapoisha unakuwa unajisikia vizuri kuliko ulivyoanza.

 1. Endelea kuongeza ugumu wa hatua unazochukua.

Kama ilivyo kwenye madawa ya kulevya, ukitumia kiwango kile kile, furaha huipati tena. Kadhalika kwenye kuchukua hatua ndogo ndogo, kama hatua unazochukua ni zile zile na zimeshakuwa rahisi kwako kiasi cha kuweza kufanya bila hata ya kufikiri hutapata tena furaha unapokamilisha. Badala yake ongeza ugumu kwenye kila hatua inayofuata, na unapovuka ugumu huo unapata furaha kubwa.

TABIA ZINAZOZALISHA ENDORPHIN.

 1. Cheka.

Kucheka kunazalisha kemikali ya endorphin ambayo inakuletea furaha. Kuwa na njia za kukuwezesha kucheka kila siku na utakuwa na maisha ya furaha. angalia, sikiliza au soma vitu vinavyochekesha na ucheke.

 1. Lia.

Kulia pia kunazalisha kemikali ya endorphin na kukuletea furaha. Ila kwenye kulia unapaswa kuwa makini, usijilazimishe kulie, bali unachopaswa kufanya ni pale unaposikia hasira ndani yako na machozi yanakutoka, usiyazuie, badala yake ruhusu kulia na utajiona umetua mzigo mkubwa sana ndani yako, hili litakupa furaha.

 1. Fanya mazoezi tofauti.

Mazoezi ni moja ya njia zinazojulikana kuzalisha endorphin na kukupa furaha baada ya kumaliza mazoezi. Lakini kama ilivyo kwenye madawa ya kulevya, kama unafanya mazoezi yale yale, baada ya muda hutapata tena furaha. Hivyo unapaswa kuwa na mazoezi tofauti na yanayoongezeka kwa ugumu ili kuwa na furaha kila unapofanya mazoezi.

 1. Jinyooshe

Kunyoosha misuli mbalimbali ha mwili kunachochea ubongo kuzalisha endorphin ambayo inakufanya ujisikie vizuri. Hivyo mara kwa mara fanya mazoezi ya kunyoosha viungo na misuli mbalimbali ya mwili na itajisikia vizuri. Uzuri unaweza kufanya hili ukiwa popote, hata wakati unafanya kazi.

 1. Fanya mazoezi yawe burudani.

Mazoezi wakiwa makali na magumu sana yanapelekea maumivu makali baadaye na kuondoa ile furaha inayotokana na endorphin. Ili kuondoa hili, fanya mazoezi kuwa burudani, kwa kufanya na wengine au kusikiliza muziki mzuri wakati wa mazoezi.

TABIA ZINAZOZALISHA OXYTOCIN.

 1. Tengeneza mahusiano yasiyo ya moja kwa moja.

Moja ya changamoto za mahusiano ni maumivu yanayotokana na kutokuaminika kwa upande wa pili. Ili kuepuka hali hiyo ya kuangushwa na wengine, unaweza kutengeneza mahusiano yasiyo ya moja kwa moja. Mahusiano haya ni kama kuwa na wanyama kama mbwa au paka, kuwa kwenye kundi fulani au hata kuwa na marafiki wa mtandaoni. Hili linakupa ile hali ya kuwa pamoja na wengine, lakini pia linakuondolea maumivu ya kuumia pale unapoangushwa na wengine.

 1. Weka hatua za kutengeneza mahusiano mapya.

Pale ambapo unahitaji kutengeneza mahusiano mapya na mtu mpya au mtu ambaye mahusiano yaliharibika hapo nyuma, unapaswa kuwa na hatua za kutengeneza mahusiano hayo. Badala ya kuingia moja kwa moja kwenye mahusiano hayo, weka ngazi ndogo ndogo za kujenga mahusiano. Kadiri kila ngazi inapofanikiwa, unapata furaha.

 1. Kuwa mtu wa kuaminika.

Kemikali ya oxytocin huzalishwa kwa wengi pale wengine wanapokuamini, hivyo kama ukijijengea tabia ya kuwa mtu unayeaminika, utaweza kuwa na furaha pale wengine wanapokuamini.

 1. Tengeneza mfumo wa kudhibitisha kabla ya kuamini.

Upo usemi kwamba amini lakini dhibitisha, jijengee utaratibu wa kudhibitisha kwanza kabla ya kuamini. Hili litakuondolea hali ya kuangushwa baadaye, hasa pale unapoamini bila ya kudhibitisha. Tatizo kubwa kwenye kemikali ya oxytocin na mahusiano ni pale unapoangushwa na hapo unaumia zaidi.

 1. Kuchua mwili.

Kuchua mwili ni njia nyingine inayozalisha kemikali ya oxytocin na kukuletea furaha. Kupata huduma ya kuchua misuli ya mwili wako kunakuletea furaha kubwa.

TABIA ZINAZOZALISHA SEROTONIN.

 1. Kuwa na fahari kwenye kile ulichofanya.

Kuna vitu vingi vizuri ambavyo umefanya kwenye maisha yako, kuwa na ufahari kwenye vitu hivyo kutakuwezesha kuwa na furaha. Angalia kitu kizuri ulichofanya kwenye siku yako na mwambie mtu mwingine kuhusu kitu hicho, hilo litakufanya ujisikie vizuri.

 1. Furahia nafasi ya kijamii uliyopo.

Huwa tunakuwa na nafasi mbalimbali kwenye jamii, kuna wakati tunakuwa nafasi ya juu na ya utawala, na kuna wakati tunakuwa nafasi ya chini ya kutawaliwa. Sasa wengi huwa hatukubali nafasi tuliyopo, tukiwa juu tunayaogopa majukumu na tukiwa chini hatutaki kutawaliwa. Lakini ukikubali ile nafasi uliyopo na kuona manufaa yake kwako, hilo litakupa furaha.

 1. Furahia ushawishi wako kwa wengine.

Mara nyingi watu huwa wanajidharau na kuona hawana umuhimu wowote kwa wengine. Lakini kila mtu ana watu ambao wanawashawishi, kuna watu ambao wanakukubali kwa kile unachofanya, lakini huenda hawakuambii. Kuna watu wanatamani sana kuwa kama wewe, lakini hawakuoneshi. Jua ushawishi huu ulionao kwa wengine na ufurahie wewe mwenyewe, wala huhitaji kuwaambia wengine. Kwa kutambua ushawishi wako kwa wengine kutakupa furaha kubwa.

 1. Kubaliana na yale yaliyo nje ya uwezo wako.

Kuna mambo yanayotokea kwenye maisha yako, ambayo yako nje ya uwezo wako kuyaathiri. Sasa iwe yametokea kwa haki au siyo kwa haki, kuhangaika nayo hakutakusaidia kwa namna yoyote ile. Kubaliana nayo na kazana na yale yaliyo ndani ya uwezo wako. Kitendo cha kukubaliana na yale yaliyo nje ya uwezo wako, kitakupa furaha kubwa.

Rafiki, hizo ndiyo tabia 18 unazoweza kuziishi kwenye siku yako na ukazalisha kemikali nne za furaha kwenye ubongo wako na ukawa na furaha ya kudumu ambayo haina madhara kwako baadaye.

Chagua kuziishi tabia hizo kwenye kila siku yako na maisha yako yatakuwa bora sana.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; https://amkamtanzania.com/jiunge