Rafiki yangu mpendwa,
Sisi binadamu ni viumbe wa hisia, maamuzi tunayoyafanya kila siku kwenye maisha yetu yanasukumwa zaidi na hisia kuliko kufikiri. Japo huwa tunapenda kujiambia tumefikiri kwa kina, huwa tunaanza na hisia kwanza kisha tunakuja kufikiri kwa nini hisia hizo ni sahihi.
Na kama tulivyojifunza kwenye uchambuzi wa kitabu cha kemikali nne za furaha, mara nyingi ubongo wetu huwa unafanya mambo kwa mazoea, yaani kabla hata hatujafikiria, unajikuta hisia zako zimebadilika kutokana na hali fulani unayopitia.
Kama utashindwa kuzielewa na kuzidhibiti hisia zako, maisha yako yatakuwa ya utumwa. Kwa sababu kila wakati utajikuta uko juu kwa hisia za furaha na muda mfupi baadaye uko chini kwa hisia ambazo siyo za furaha.
Zipo hisia mbili ambazo zimekuwa kikwazo kwa wengi, hisia hizi zimekuwa zikichochewa pale tunapokutana na wengine na kutufanya tujisikie vibaya.
Hisia hizi mbili ni WIVU na KUDHARAULIWA. Tunapokutana na wengine, mara nyingi hisia hizi huibuka ndani yetu na kuibuka kwa hisia hizi kunatuzuia kupiga hatua kubwa kwenye maisha yetu.
Kwenye makala hii ya leo nakwenda kukushirikisha jinsi unavyoweza kuondokana na hisia hizi na kuweza kuweka juhudi kwenye yale ambayo ni muhimu zaidi kwako.
HISIA ZA WIVU.
Hisia za wivu zinazaliwa pale mtu unapojilinganisha na mwingine, pale unapomwangalia mtu mwingine unayemjua na unayeona mpo ngazi moja lakini yeye amefanya kitu kikubwa au kupiga hatua ambayo wewe hujapiga, hisia za wivu zinakuingia.
Wengi husema wivu ni mzuri na kuna wivu wa maendeleo. Lakini katika mafanikio, hakuna wivu mzuri, kwa sababu kama huwezi kupata msukumo wa kuchukua hatua kwenye maisha yako mpaka uone wengine wamechukua hatua, hata utakapopata kile wengine wamepata hakitakuletea furaha.
Hivyo kwa maisha ya mafanikio, siyo tu kwamba wivu utakuchosha, bali pia utakuondoa kwenye kufanyia kazi yale muhimu kwako. Unapoanza kujilinganisha na wengine unawafanya wao kuwa sahihi na wewe kutokuwa sahihi. Unaacha kuyaishi maisha yako na kuishi maisha yao, kitu ambacho kinakupoteza kabisa.
Jinsi ya kuondokana na hisia za wivu.
Kwenye kitabu kimoja cha Jack Confield amewahi kutoa mfano huu wa wivu ambao niliuelewa sana na nikaona ni njia bora sana ya kuondokana na hisia za wivu.
Anasema ukiwa njiani na Raisi wa nchi akapita akiwa kwenye gari ya kifahari hakuna chembe yoyote ya wivu itawaka ndani yako. Lakini hapo hapo akapita mtu uliyesoma naye au jirani yako akiwa kwenye gari ya kifahari kama ile ile aliyopita nayo raisi, utaingiwa na wivu.
Sasa je nini kimebadilika hapo, watu wawili, wametumia kitu kinachofanana, lakini mmoja umepata wivu wakati mwingine hujapata wivu?
Kilichobadilika ni kujilinganisha. Hujilinganishi na Raisi wa nchi, kwa sababu unajua kabisa kwamba raisi wa nchi yupo ngazi nyingine kabisa na uliyopo wewe. Lakini kwa mtu uliyesoma naye au jirani yako, unaweza kujilinganisha na kujiuliza amewezaje kupiga hatua hiyo ambayo wewe hujapiga, kwa kuwa unamjua kwa ukaribu na unajua mpo ngazi sawa wote.
Ukiacha kujilinganisha na yeyote, hutaingiwa na wivu, unapojiangalia wewe kama mtu tofauti na wa kipekee na kuwaona wengine wakiwa tofauti pia, hutapata hisia hizo za wivu.
Pia kwa kujua uko tofauti na kukazana kufanyia kazi utofauti wako, hutapata muda wa kuanza kujilinganisha na wengine. Unapokuwa umetingwa kweli na kufanyia kazi yale yaliyo muhimu, hutapata hata muda wa kuangalia wengine wanafanya nini na maisha yao, na hilo litakuondoa kabisa kwenye wivu.
SOMA; Tabia Ndogo Ndogo 18 Za Kuishi Kila Siku Ili Uwe Na Furaha Ya Kudumu Kwenye Maisha Yako.
HISIA ZA KUDHARAULIWA.
Hisia nyingine zinazowakwamisha wengi kupiga hatua ni hisia za kudharauliwa. Pale wengine wanapofanya kitu ambacho kinaenda kinyume na ulivyotaka wafanye, unajisikia kudharauliwa na watu hao.
Kudharauliwa nako ni matokeo ya kujilinganisha na kujipa hadhi fulani ambayo unataka kila mtu aiheshimu kwako. Inapotokea mtu ameenda kinyume na hadhi uliyojiwekea, unaona umedharauliwa.
Huwezi kupata hisia za kudharauliwa kama hujajiwekea hadhi fulani kwenye maisha yako na kutaka kila mtu aishi kama unavyotaka wewe. Unapata hisia hizi za kudharauliwa pale unapotaka dunia iende kama wewe, na anapotokea mtu ambaye anaenda kama atakavyo bila ya kujali wewe unataka nini, unaona ni dharau kwako.
Hisia za dharau ni mzigo mkubwa kwako, kwa sababu zitakuumiza sana na wakati huo wale wanaozichochea kwako wakiwa hata hawajui nini kinaendelea kwako.
Pia wakati mwingine watu wanapojua hisia hizo zinakusumbua, wanazichochea kwa makusudi ili kukuvuruga na kukuondoa kwenye yale muhimu unayoyafanya.
Jinsi ya kuondokana na hisia za kudharauliwa.
Njia bora ya kuondokana na dhana ya kudharauliwa ni kupuuza, kuchukulia kama hujaona wala kusikia kile mwingine amefanya. Kupuuza siyo tu inakusaidia wewe kutokupata hisia za dharau, bali pia kunarudisha ile dharau kwa mtendaji wa kitu.
Mfano mtu anapofanya kitu makusudi kukuumiza, halafu wewe ukapuuza kama vile hakuna kilichotokea, mfanyaji anajisikia vibaya sana.
Hivyo jifunze kupuuza pale mtu anapofanya kitu kinachoibua hisia za kudharauliwa ndani yako, chukulia kama hujaona au hujasikia, itakusaidia sana.
Mbinu nyingine nzuri ya kutoka kwenye Falsafa ya Ustoa ni kumchukulia mfanyaji wa jambo kama mtoto asiyejua chochote.
Mtoto akikuambia neno baya, utajua ni utoto unamsumbua, lakini mtu mzima akikuambia neno hilo hilo, utachukulia anakudharau. Sasa ukichukulia kila anayefanya jambo la kukudharau kama mtoto asiyejua chochote, unaishia kumwonea huruma na siyo wewe kujisikia kudharauliwa.
Kwa kuwachukulia wanaokufanyia mambo ya dharau kama watoto, kunaondoa mzigo mkubwa sana kwako na unakuwa huru kuendelea na maisha yako bila ya kubeba mizigo ya wengine.
Rafiki, hivi ndivyo unavyoweza kuondokana na hisia hizo mbili ambazo zimekuwa mzigo na kikwazo kwa wengi kupiga hatua. Na kama ambavyo umejifunza, kama ukijua nini unataka na maisha yako, na ukajitoa kufanyia kazi ili kukipata, utapunguza sana muda na nguvu za kuweka kwenye hisia hizo. Mara nyingi unapokuwa huna cha kufanya, ndiyo unapata muda wa kuanza kuangalia wengine wanafanya nini na kujilinganisha, na hapo unaibua hisia za wivu na dharau.
Kazana na yako na waache wengine wakazane na yao, pima mafanikio yako kwa kupata kile ulichotaka na siyo kwa kuwashinda au kuwa juu ya wengine. Hilo litakusaidia sana, kwa sababu haijalishi umepiga hatua kiasi gani, lazima kuna mtu ambaye yuko juu yako. Ukiacha kuangalia nani yuko juu na ukaangalia hatua gani unapiga, hisia za wivu na dharau hazitakusumbua.
Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha
Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; https://amkamtanzania.com/jiunge