#TANO ZA JUMA #5 2019; Furaha Zao La Ndani, Tabia Za Ubongo Wenye Furaha, Tabia 18 Za Kuwa Na Furaha Ya Kudumu, Mchango Wa Fedha Kwenye Furaha Na Usiangalie Upande Mbaya Pekee.

Karibu rafiki yangu mpendwa kwenye makala hii ya TANO ZA JUMA.

Kama ambavyo utakuwa umeona, kwa sasa kuna mabadiliko kwenye makala hizi za tano za juma, ambapo kwa sasa tano za juma zitakuwa zinatokana na kitabu cha juma ambacho nimesoma.

Hii inanipa nafasi ya kuzama ndani sana na kusoma kitabu kwa kina zaidi, kisha kuja na vitu ambavyo wote tunaweza kuvifanyia kazi na maisha yetu yakawa bora sana.

Hongera kwa kumaliza juma la tano la mwaka huu 2019, mwaka unazidi kuchanja mbuga na ni imani yangu kwamba malengo yako yanachanja mbuga pia. Kupiga hatua kidogo ni bora kuliko kutokupiga hatua kabisa, hivyo hata kama unachukua hatua ndogo, upo pazuri kuliko kutokuchukua hatua kabisa.

Tano za juma hili zinatoka kwenye kitabu kinaitwa HABITS OF A HAPPY BRAIN, hivyo tunakwenda kuzama kwenye tabia za ubongo wetu ambazo zinatuletea furaha kwenye maisha yetu.

Karibu sana tujifunze na kuondoka na hatua za kwenda kuchukua ili maisha yetu yawe bora zaidi.

#1 NENO LA JUMA; FURAHA ZAO LA NDANI.

Kila ambaye amekuwa anaanza kufanya kitu chochote kwenye maisha yake kwa lengo la kupata furaha, amekuwa anaishia kujisikia vibaya baada ya kupata alichofikiri akipata kitampa furaha.

Wengi wanapokutana na hali hii huwa wanafikiri kuna shida kwenye kile walichopata, lakini ukweli ni kwamba shida haipo kwenye chochote unachotaka, bali shida ipo ndani yako.

Furaha ya kweli kwenye maisha ni zao la ndani, ni kitu kinachoanzia kwenye fikra zako na siyo matokeo ya kile unachopata. Hata kama umepata kitu kikubwa na muhimu kiasi gani, furaha yake huwa ni ya muda mfupi tu, baada ya hapo unarudi kwenye hali yako ya kawaida.

Sasa unaweza ukawa unajiuliza nini kinasababisha hilo? Kwa nini usiwe na furaha muda wote baada ya kupata kila unachotaka?

Rafiki, ubongo wetu huzalisha furaha kwa kutoa kemikali nne ambazo tutajifunza zaidi kwenye kitabu cha juma. Kemikali hizi huzalishwa mara moja pale unapokamilisha kitu fulani. Lakini baada ya kuzalishwa, mwili huvunja kemikali hizi na ndiyo maana ile hali ya furaha inadumu kwa muda mfupi.

Ili uendelee kupata furaha hiyo, inabidi mwili uzalishe tena kemikali hizo za furaha, kitu ambacho kinakutaka ukamilishe kitu kikubwa kuliko kile cha awali. Na hili ndiyo linawapelekea wengi kujikuta kila wakati wanatamani vitu vikubwa zaidi, wakiamini kuvipata kutawapa furaha ya kudumu, lakini wakishavipata furaha inapotea baada ya muda mfupi.

Furaha ya kweli inaanzia ndani yako na siyo nje, ili kuwa na furaha ya kweli, kwanza lazima uielewe akili yako jinsi inavyozalisha furaha na kisha kuitumia vizuri kutengeneza furaha inayotegemea ndani yako na siyo nje.

Kwa mfano, badala ya kusubiri mpaka ukamilishe lengo kubwa ndiyo upate furaha, unagawa lengo hilo kwenye hatua ndogo ndogo za kuchukua kila siku, na kila siku unapokamilisha hatua uliyojipangia unapata furaha. Kwa njia hii utakuwa na furaha inayodumu kila siku kwa hatua ndogo ndogo unazopiga badala ya kusubiri mpaka ukamilishe lengo moja kubwa, ambalo furaha yake itadumu kwa muda mfupi pekee.

habits-of-a-happy-brain

#2 KITABU CHA JUMA; TABIA ZA UBONGO WENYE FURAHA.

Rafiki yangu mpendwa, kitabu chetu cha juma la tano ni kitabu kinachoitwa HABITS OF A HAPPY BRAIN : Retrain Your Brain to Boost Your Serotonin, Dopamine, Oxytocin, & Endorphin Levels ambacho kimeandikwa na LORETTA GRAZIANO BREUNING.

Hiki ni kitabu ambacho kinatufundisha kuhusu nguvu kubwa ya kemikali zilizopo kwenye ubongo wetu, ambazo ndiyo zinazalisha furaha kwenye maisha yetu.

Hiki ni kitabu muhimu sana kama mtu unataka kujijengea tabia ambazo zitakuletea furaha ya kudumu kwenye maisha yako. Hapa tunakwenda kujifunza yale muhimu kuhusu kemikali hizo zilizopo kwenye ubongo wetu na jinsi ya kuzitumia kuzalisha furaha ya kudumu kwenye maisha yetu.

Karibu sana kwenye kitabu cha juma, ujifunze na kutafakari kisha kuchukua hatua kwenye maisha yako.

Kuhusu mwandishi wa kitabu hiki.

Loretta Graziano Breuning alikulia mazingira ambayo hayana furaha. Akiwa mdogo hakujua chanzo cha yeye kukosa furaha, hivyo alifanya yale ambayo wanaokosa furaha huwa wanafanya, na kubwa ni kulaumu mifumo iliyopo. Lakini baadaye aliamua kuchukua jukumu la kufanya utafiti juu ya hali ya kukosa furaha kwa wanadamu.

Na hapo ndipo alipogundua kemikali nne ambazo ndiyo chanzo cha furaha kwa wanadamu na jinsi ambavyo zinazalishwa na kuleta furaha. Tangu hapo Loretta amekuwa akiandika na kutoa mafunzo juu ya kujitabua sisi binadamu kama sehemu ya wanyama na jinsi ya kutumia ubongo wetu kuwa bora zaidi.

Loretta ana shahada ya uzamivu (PHD) kwenye sayansi za kijamii na pia ni mhadhiri wa chuo kikuu. Vitabu vyake vingine ni I, Mammal: Why Your Brain Links Status and Happiness na Beyond Cynical: Transcend Your Mammalian Negativity. Vitabu vyote hivi vinaangalia asili yetu binadamu na jinsi ya kutumia ubongo kuwa na maisha bora.

TABIA ZA UBONGO WENYE FURAHA.

Kama ambavyo jina la kitabu linakwenda, Loretta amefanya kazi kubwa ya kutuonesha tabia ambazo zinafanya ubongo wetu uzalishe furaha. Hapa nakwenda kukushirikisha yale muhimu sana kuhusu tabia za furaha ambayo unaweza kuyafanyia kazi kwenye maisha yako na ukawa na furaha ya kudumu.

KUSUDI KUU SIYO FURAHA BALI KUISHI.

Ukiangalia historia ya sisi wanadamu, furaha ni kitu ambacho tumeanza kukizungumzia baada ya kuanza kuishi kama jamii zilizostaarabika. Ukiangalia enzi ambazo tuliishi misituni na wanyama, hakuna mtu alikuwa anafikiria kuhusu furaha. Fikra zetu binadamu zilikuwa kwenye kuishi, na tulifikiria yale tu ambayo yalituwezesha kuendeleza maisha yetu.

Vitu vitatu ambavyo vilikuwa fikra kuu za wanadamu enzi hizo zilikuwa kuhusu kupata chakula, ambacho kilikuwa ni uhaba mkubwa, kuhusu kuepuka hatari ya kuliwa na wanyama wakali, ambao walikuwa kila eneo na kuhusu kupata mwenza wa kujamiiana naye na kuzalisha watoto, kitu ambacho hakikuwa rahisi.

Ili kuhakikisha kwamba kizazi cha binadamu kinaendelea, ubongo wa binadamu ulijifunza kumsukuma mtu kwenye yale mazuri na kumwondoa kwenye yale mabaya. Na hapa ndipo zilipozalishwa kemikali nne ambazo zilimsukuma mtu kuchukua hatua sahihi zinazomwezesha kupona na kuzaliana.

Kwa kuwa sasa hatupo tena kwenye hatari za enzi hizo, lakini ubongo bado unazalisha kemikali zile, zimebaki kuwa sehemu ya kuleta furaha badala ya kuwa sehemu ya kuhakikisha tunapona na kuzalisha.

Tunaishi kwenye zama tofauti, usalama kwa sasa ni mkubwa sana, chakula ni kingi na wenza ambao mtu unaweza kujamiiana nao na kupata watoto ili kuendeleza kizazi chako wapo wengi.

Tumehamisha zile hatari kubwa ambazo watangulizi wetu walipambana nazo na sasa kitu kikubwa kwetu kimekuwa furaha. Kama tutaweza kuelewa vizuri jinsi ubongo unavyofanya kazi na kuzielewa kemikali nne za furaha, tutaweza kuwa na maisha bora na ya furaha.

ZIJUE SEHEMU KUU TATU ZA UBONGO.

Ubongo wa binadamu una sehemu kuu tatu, kuna ubongo wa chini kabisa ambao unahusika na mifumo ya maisha kama kupumua na mapigo ya moyo, huu upo kwa wanyama wote. Upo ubongo wa kati ambao unahusika na tabia ambazo tunakuwa nazo, huu pia upo kwa wanyama wote. Na upo ubongo wa juu ambao unahusika na kufikiri na kufanya maamuzi, ubongo huu upo kwa binadamu na wanyama wa jamii ya binadamu kama nyani na sokwe.

Ubongo wa kati, ambao unahusika na tabia una eneo linaitwa limbic system ambalo linazalisha kemikali ambazo zinausukuma mwili kuchukua au kutokuchukua hatua fulani. Kemikali hizi zipo za aina mbili, kuna ambazo zinaupa mwili hongera kwa kufanya kitu na hivyo kuutaka mwili ufanye zaidi. Na kuna ambazo zinautaarifu mwili kwamba kuna kitu hakijafanyika na hivyo uchukue hatua mara moja.

Hapo ndipo ulipo mgawanyiko wa kemikali za furaha na kemikali zisizo za furaha.

Wanyama wengine ambao hawana ubongo wa juu, huwa hawana muda wa kufikiri na kuja na njia bora ya kufanya kitu, badala yake wanafanya kile ambacho mwili unawasukuma kufanya. Kwa mfano mjusi akisikia kishindo, hana muda wa kusubiri na kufikiria kishindo hicho kinatokea wapi au kinahusu nini. Yeye anaanza kukimbia. Lakini sisi binadamu kwa kuwa tuna ubongo unaofikiri, hatukimbii mara moja badala yake tunajiuliza kwanza kishindo hicho kinatokea wapi na kinaashiria nini.

ZIJUE KEMIKALI NNE ZA FURAHA ZINAZOZALISHWA NA UBONGO WAKO.

Ubongo unazalisha kemikali nne ambazo ndizo zinaleta furaha kwenye maisha yetu. Kemikali hizi zinatofautiana kwa ufanyaji wake wa kazi, lakini mwisho wa siku zote zinaishia kuleta furaha.

MOJA; DOPAMINE.

Kemikali ya kwanza ni DOPAMINE. Hii ni kemikali ambayo huzalishwa na ubongo pale ambapo mtu anakuwa amepata kile anachotaka. Asili ya kemikali hii ilikuwa kwenye kutafuta chakula. Kwa kuwa chakula kilikuwa adimu, pale ambapo mtu alipata chakula ubongo ulizalisha kemikali hii na kuufanya mwili uelewe kwamba kupata chakula ni kitu muhimu na hivyo utafute chakula zaidi.

Kwa sasa unaweza kutumia kemikali hii kwenye kufikia malengo yako ya kimaisha, kwa kuwa kila hatua unayopiga kwenye maisha, inazalisha kemikali hii. Kwa kuweka lengo unalofanyia kazi na kuligawa kwenye hatua ndogo ndogo, kila unapokamilisha hatua moja, ubongo wako unazalisha kemikali hiyo na unajisikia furaha.

Kwa kutumia hivi kemikali hii, utaweza kupiga hatua kubwa kwenye maisha yako huku ukiwa na furaha wakati wote.

MBILI; ENDORPHIN.

Kemikali ya pili ni ENDORPHIN, hii ni kemikali ambayo huzalishwa na ubongo kufubaza maumivu. Hapa mtu unapokuwa na maumivu, ubongo huzalisha kemikali ya endorphin ambayo inakufanya ujisikie vizuri. Asili ya kemikali hii ilikuwa ni kwenye kujiokoa. Pale ambapo mtu ulikuwa kwenye hatari kubwa na unahitaji kujiokoa, lakini pia ukaumia, bado ulipata nafasi ya kujiokoa. Unakuta mtu ameumia na kwa hali ya kawaida hawezi kabisa kujiokoa, lakini ubongo unazalisha kemikali hiyo ambayo inamfanya asisikie maumivu na aweze kujiokoa.

Kwa sasa tunaweza kutumia kemikali hii kwa kufanya mazoezi au kuuweka mwili kwenye hali inayozalisha maumivu ambayo yatachochea ubongo kuzalisha kemikali hii. Mazoezi ya viungo, kucheka, kulia na mengine yanayohusisha mwili kufanya kazi na kuleta maumivu, yanachochea kuzalishwa kwa kemikali hii na kutupa furaha.

Kwa kutumia kemikali hii unaweza kunufaika na maumivu unayokutana nayo kwenye maisha.

TATU; OXYTOCIN.

Hii ni kemikali inayozalishwa na ubongo pale unapoaminiwa na wengine na kuwa sehemu ya kundi la wengine. Kemikali hii inazalishwa pale ambapo unakuwa ndani ya kundi au unapokuwa na mahusiano mazuri na wengine. Asili ya kemikali hii ilikuwa usalama wa kuweza kuishi kwenye zama ambazo zilikuwa hatari sana. Enzi hizo ambapo usalama haukuwa mkubwa, ilikuwa hatari sana mtu kufanya mambo yako mwenyewe. Hivyo ndani ya kundi palikuwa na usalama mkubwa. Kuwa ndani ya kundi kulizalisha kemikali hii ambayo ilimfanya mtu ajisikie vizuri.

Kemikali hii pia inazalishwa kwa kufanya mapenzi, pale mtu anapojifungua, pale mama anaponyonyesha mtoto na hata kukumbatiana na kushikana.

Kwa sasa tunaweza kutumia kemikali hii kuboresha mahusiano yetu na wengine, lakini tunapaswa kujua siyo lazima tuwe ndani ya kundi ili kuwa salama.

NNE; SEROTONIN.

Hii ni kemikali ambayo inazalishwa na ubongo pale mtu unapothaminiwa na kuheshimiwa na wengine. Pale unapoonekana ni wa thamani basi ubongo huzalisha kemikali hii inayoleta furaha. Asili ya kemikali hii ilikuwa kwenye kupata nafasi ya kuzaliana. Kama ambavyo tumeona, nafasi za kupata mwenza wa kujamiiana naye na kuzalisha zilikuwa haba. Hivyo wale waliokuwa na uwezo mkubwa kinguvu au mwonekano bora ndiyo waliopata nafasi ya kupata mwenza wa kujamiiana nao. Hivyo ubongo ulijifunza kuzalisha kemikali inayozalishwa pale mtu anapothaminiwa na kumfanya achukue hatua ya kupata nafasi anayotaka. Kemikali hii pia ndiyo inayojenga madaraja yaliyopo kwenye jamii, wale walio daraja la juu iwe ni kwenye maisha, kazi na hata biashara, wanazalisha kwa wingi kemikali hii ya serotonin.

Kwa sasa tunaweza kuitumia kemikali hii kuwa na ufahari kwa kile tunachofanya na kwa uwezo wa kipekee uliopo ndani yetu. Nia nyingine tunazoweza kutumia kuchochea kuzalishwa kwa kemikali hii ni kujithamini sisi wenyewe, kufanya vitu kwa ajili ya wengine na pia kufurahia nafasi ya kijamii ambayo upo, iwe ni chini au juu.

Rafiki, hizi ndizo kemikali nne ambazo zinazalisha furaha kwenye ubongo wako. Pale unapofanya kitu kinachoendana na kemikali husika, ubongo unazalisha kemikali hiyo na hivyo unapata furaha. Lakini furaha hiyo imekuwa haidumu kwa sababu kemikali hizo huvunjwa na mwili. Hivyo ili kupata tena furaha inabidi urudie kile kilichozalisha kemikali husika. Na hapa ndipo wengi wanapoingia kwenye mtego ambao unaharibu kabisa maisha yao.

KEMIKALI YA KUTOKUWA NA FURAHA.

Ipo kemikali moja inayozalishwa na ubongo ambayo inapelekea hali ya kutokuwa na furaha. Kemikali hii inaitwa Cortisol. Kazi ya kemikali hii ni kuukumbusha mwili kwamba kuna kitu ambacho umekosa hivyo uchukue hatua mara moja.

Pale unaposikia njaa na kusukumwa kutafuta chakula ni cortisol inafanya kazi yake, pale unapokosa unachotaka na kujisikia vibaya ni cortisol inakuwa imezalishwa, na pale unapokuwa mpweke na kujisikia vibaya, cortisol inakuwa inakukumbusha kuhusu kuwa ndani ya kundi.

Cortisol ni kemikali ambayo huwa inausukuma mwili ufanye kitu ili kuzalisha kemikali ya furaha. Kemikali hii imekuwa inawasukuma watu kutafuta njia za mkato za kuzalisha kemikali za furaha kwa sababu huwa haitulii mpaka pale ubongo umezalisha kemikali ya furaha, kiashiria kwamba kila kitu kipo vizuri.

Hii ni kemikali ambayo unapaswa kuijua na kuitumia vizuri ili isikupeleke kwenye kufanya maamuzi mabovu kwenye maisha yako. Na kwa kuwa zama tunazoishi sasa ni salama, kitu bora cha kufanya pale kemikali hii inakusukuma ufanye kitu ni kutulia na kutokufanya chochote, hii ndiyo njia pekee unaweza kujidhibiti na kujijengea tabia unazotaka wewe badala ya kufuata mazoea.

TABIA 18 ZA KUWA NA FURAHA YA KUDUMU.

Ili kuweza kutengeneza furaha ya kudumu, unapaswa kuweza kuzalisha kemikali za furaha kwa njia ya asili na mara kwa mara. Zipo tabia 18 za kuishi kila siku ambazo zitakuwezesha kuzalisha kemikali hizo kila siku na hivyo kuwa na furaha ya kudumu.

Kwenye makala ya juma nimezielezea tabia hizo kwa kina, unaweza kuisoma makala hapo chini.

NJIA KUMI ZA KUTENGENEZA TABIA ZA FURAHA KWENYE UBONGO WAKO.

Wote tunajua kwamba mabadiliko huwa yanakuwa magumu kwa sababu ya tabia. Tabia mpya huwa ni ngumu kujijengea, na tabia za zamani huwa ni ngumu kuvunja. Bila ya kuwa na njia sahihi, zoezi la kutumia ubongo wako kuzalisha furaha litakwama.

Loretta ametushirikisha njia kumi za kutusaidia kutengeneza tabia za furaha kwenye ubongo wetu. Tujifunze na kutumia njia hizi ili kuweza kuzalisha furaha ya kudumu kwenye maisha yetu.

Moja; jifunze kwa wengine, angalia watu ambao wana tabia unazotaka kujijengea kisha jifunze wanafanya nini na wewe ufanye. Ukifanya kile ambacho wenye furaha wanafanya, na wewe utakuwa na furaha pia.

Mbili; tumia kemikali za furaha ambazo hutumii kwa sasa. Kila mtu kuna kemikali anazotumia sana na ambazo hatumii kabisa. Ili kutengeneza tabia za furaha, angalia ni kemikali zipi hutumii na anza kuzitumia. Kama umekuwa mtu wa kuweka malengo na kuyafikia, kazana pia kuboresha mahusiano yako na wengine na hilo litakupa furaha.

Tatu; tengeneza tabia mpya kwenye tabia za zamani ulizonazo sasa. Angalia kile kitu ambacho unapenda kukifanya sasa, kisha ona jinsi gani unaweza kukifanya na ile tabia unayotaka kujenga. Unapohisianisha vitu hivi viwili unaweza kujenga tabia bora kwako.

Nne; nguvu. Kujenga tabia yoyote kunahitaji nguvu, hivyo panga kufanya kile unachofanya ili kujenga tabia mpya unapokuwa na nguvu. Asubuhi na mapema ni muda mzuri wa kufanya yale yanayojenga tabia mpya.

Tano; sifa. Unapofanya kitu kwa ajili ya sifa yako ya baadaye inakuwa rahisi kwa kitu hicho kuwa tabia. Pale unapofikiria kuacha alama fulani hata baada ya kuondoka, unasukumwa kufanya zaidi.

Sita; burudani. Fanya zoezi la kujenga tabia mpya kuwa burudani kwako. Usifanye kama ni jukumu zito na linalochosha, badala yake fanya kuwa burudani na itakuwa rahisi kwako kuendelea nalo.

Saba; vunja jukumu kubwa kwenye majukumu madogo madogo, na unavyokamilisha sehemu ndogo ya jukumu unapata hamasa ya kuendelea na sehemu nyingine. Kwa kugawa majukumu madogo madogo haikuchoshi wala kukukatisha tamaa.

Nane; fanya inayoridhisha badala ya kutaka kufanya iliyo kamili. Badala ya kusubiri mpaka uweze kuchukua hatua iliyo kamilika na sahihi zaidi, chukua hatua inayoridhisha. Unapoona nafasi ya kuchukua hatua, hata kama haijakamilika, ni bora kuliko kusubiri mpaka upate ukamilifu ambao haupo.

Tisa; anza maandalizi mapema. Unapojua kuna tabia unataka kujijengea, anza maandalizi yake mapema kabla ya kufika wakati unaohitaji.

Kumi; tengeneza taswira ya kuwa na ile tabia unayotaka kutengeneza. Kwa kutengeneza taswira ya aina hiyo, njia zako za kwenye ubongo zinazotengeneza tabia zinaimarika hata bila ya kufanya tabia husika. Hili limedhibitishwa na tafiti kwenye michezo, wachezaji ambao wanatengeneza taswira wakiwa wanacheza vizuri wanaimarisha uchezaji wao hata kama hawajacheza.

Rafiki, tumia njia hizi kumi kujijengea tabia za furaha ambazo zitadumu kwenye maisha yako.

NI MUDA KIASI GANI UNAHITAJI KUJENGA TABIA MPYA ZA FURAHA?

Rafiki, tumalizie na muda unauhitaji ili kujenga tabia mpya za furaha kwenye maisha yako.

Loretta anatuambia unahitaji siku 45 za kufanya tabia unayoijenga ndiyo iweze kuwa sehemu ya maisha yako. unapaswa kufanya kwa siku 45 bila kuacha hata siku moja, na baada ya hapo inakuwa mazoea kwako.

Kama umefanya kwa siku 10 na siku ya 11 ukaacha, basi inabidi uanze tena upya. Mpaka utakapoweza kukamilisha siku 45 bila ya kuacha hata siku moja ndiyo tabia hiyo itakuwa sehemu ya maisha yako.

Rafiki, hizo ndizo tabia za furaha zinazozalishwa na ubongo tulionao kupitia kemikali za furaha. Fanyia kazi haya uliyojifunza ili uweze kujenga tabia bora za furaha ya kudumu na mafanikio makubwa kwenye maisha yako.

#3 MAKALA YA JUMA; TABIA 18 ZA KUWA NA FURAHA YA KUDUMU.

Kuwa na furaha ya kudumu kwenye maisha inaonekana kama ni kitu kisichowezekana. Na wengi waliojaribu kutumia njia za mkato kutengeneza furaha ya kudumu kwenye maisha yao wameishia kwenye tabia ambazo zimeleta madhara makubwa kwao.

Wengi wameishia kwenye ulevi na uteja wa vile vitu ambavyo walikuwa wanavitegemea viwape furaha muda wote. Inaweza kuwa pombe, madawa ya kulevya, sifa kutoka kwa wengine na hata ufanyaji wa mapenzi.

Sasa ipo njia ya kutengeneza furaha ya kudumu kwenye maisha yako, njia ambayo haina madhara yoyote kwako kwa sababu siyo ya mkato, bali ni njia ya asili.

Kuna tabia ndogo ndogo 18 ambazo ukiweza kuziishi kwenye kila siku ya maisha yako, utakuwa na furaha ya kudumu bila ya kujali una nini kwenye maisha yako.

Kwenye makala ya juma hili, nimekushirikisha tabia hizo 18 na jinsi ya kuziishi kwenye maisha yako ili uwe na furaha ya kudumu.

Kama hukusoma makala hiyo unaweza kuisoma sasa hapa; Tabia Ndogo Ndogo 18 Za Kuishi Kila Siku Ili Uwe Na Furaha Ya Kudumu Kwenye Maisha Yako. (https://amkamtanzania.com/2019/02/01/tabia-ndogo-ndogo-18-za-kuishi-kila-siku-ili-uwe-na-furaha-ya-kudumu-kwenye-maisha-yako/)

#4 TUONGEE PESA; MCHANGO WA FEDHA KWENYE FURAHA.

Hakuna sehemu ambayo wengi wamevurugwa kama inapokuja kwenye fedha na furaha. Wengi wamekuwa wakifikiri wakishapata fedha basi watakuwa na furaha kwenye maisha yao. Hivyo wanakazana kupata fedha ili wapate furaha, wanazipata fedha lakini furaha inakuwa ya muda mfupi, haidumu.

Mchango wa fedha kwenye furaha ni pale ambapo unapotengeneza kipato halali, kwa kufanya kitu ambacho kina manufaa kwa wengine na pia kipato hicho kuendelea kukua siku hadi siku.

Unapopata fedha kwa njia halali, na ambayo inazalisha thamani kwa wengine unajithamini wewe mwenyewe na kuona umuhimu wako kwa wengine, hili linakuletea furaha.

Na pale ambapo kipato chako kinaendelea kukua siku hadi siku unapata furaha kadiri unavyopanda ngazi kwenye kipato.

Hivyo ili upate furaha kwenye fedha, usisubiri mpaka upate fedha nyingi ndiyo ufurahi, badala yake fanya kile kinachoongeza thamani kwa wengine, na endelea kuweka juhudi kila siku ili kipato chako kiendelee kukua.

Isitokee hata siku moja ukajiambia umeshakuwa na fedha za kutosha hivyo huhitaji tena kufanya chochote, hapo ndipo utakaribisha hali ya kukosa furaha na utakazana kutumia fedha hizo kwa njia za mkato za kupata furaha, kitu ambacho kitakupoteza zaidi.

#5 TAFAKARI YA KUFIKIRISHA; USIANGALIE UPANDE MBAYA PEKEE.

“Things go wrong occasionally, but when you focus on that, you miss the enormity of what goes right.” ― Loretta Graziano Breuning

Ni kawaida yetu sisi binadamu kuangalia upande mbaya wa jambo lolote lile. Kama huamini fungulia redio, tv au soma gazeti lolote linaloripoti habari. Kwa siku kuna mamilioni ya magari yanayofanya safari zake, lakini katika mamilioni hayo ya magari, kuna magari kumi yatapata ajali. Na tutakazana kuangalia magari hayo kumi yaliyopata ajali na kusahau mamilioni ya magari ambayo yamekamilisha safari zake salama kabisa bila ya ajali.

Kuangalia upande mbaya wa kitu ilikuwa na manufaa kwetu sisi binadamu kipindi ambacho maisha yetu wanadamu yalikuwa magumu na usalama ulikuwa mdogo. Kipindi ambacho hatari ya kuliwa na wanyama wakali ilikuwa kubwa, mara zote ilibidi uangalie dalili za mambo kuwwa mabaya.

Lakini kwa zama tunazoishi sasa, hatari kama hizo ni ndogo sana, lakini akili zetu bado zinafanya kazi kama zilivyorithi kwa watangulizi wetu walioishi kwenye hatari hizo.

Hivyo tunapaswa kuzitengeneza upya akili zetu, badala ya kuangalia upande mbaya pekee, tuangalie hali nzima na tutaona mengi mazuri.

Mambo mabaya lazima yatokee, lakini kama utapeleka fikra zako zote kwenye upande mbaya wa mambo, utakosa mengi mazuri ambayo yanaendelea kwenye maisha yako.

Na katika kila baya linalotokea, jua kuna zuri ambalo linaambatana na baya hilo. Angalia na utaona.

Rafiki, hizi ndizo tano za juma la tano tunalolimaliza, ni imani yangu umepata msingi sahihi wa kujitengenezea furaha kwenye maisha yako, furaha inayoanzia ndani na siyo nje.

Unapoanza na furaha ya ndani na ya kudumu kwenye maisha yako, basi mafanikio kwenye maisha yako ni lazima. Lakini kama utaweka furaha pembeni na ukazane kwanza kufanikiwa, unaweza ukafanikiwa lakini hutaipata furaha. Acha sasa kukimbizana na furaha kama wengi wafanyavyo na anza kuishi kwa misingi ambayo itazalisha furaha ya kudumu na mafanikio makubwa kwenye maisha yako.

Uwe na tafakari bora ya juma unalimaliza na maandalizi bora ya juma la sita unalokwenda kuanza. Lipangilie juma hilo kwa namna ambayo kila siku itakuwa siku ya furaha kwako na hilo litakuwezesha kuwa na maisha bora sana.

Makala hii imeandikwa na Kocha Dr Makirita Amani.

Dr. Makirita ni Daktari wa binadamu, Kocha wa mafanikio, Mwandishi na Mjasiriamali.

Dr. Makirita anaendesha mafunzo ya mafanikio kwa wale waliojitoa hasa kufanikiwa kupitia program ya KISIMA CHA MAARIFA.

Kama bado hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA, tuma sasa ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa njia ya wasap namba 0717 396 253 (tumia wasap tu)

Kupata huduma nyingine za ukocha tembelea www.amkamtanzania.com/kocha

Kupata vitabu vizuri vya kusoma tembelea www.amkamtanzania.com/vitabu