Tunapozungumzia uvivu, wengi tumezoea ule uvivu wa nguvu, kutokutaka kutumia nguvu na hivyo kuepuka kutekeleza majukumu fulani. Uvivu huu huoneshwa kwa tabia ya kuahirisha mambo, kutafuta njia ya mkato na hata kukimbia majukumu ambayo mtu anapaswa kuyabeba.

Sasa kuna uvivu mwingine wa kisasa, uvivu ambao wengi hawajui kama ni uvivu, ila unawakwamisha sana katika kupiga hatua kwenye maisha yako.

Huu ni uvuvi wa kihisia, hapa mtu anakwepa kuchukua hatua au kubeba majukumu yake kwa kuogopa kuumiza hisia za wengine.

Huu ni uvivu wa kusema ndiyo ili kuridhisha mtu wakati jibu sahihi lilipaswa kuwa hapana. Uvivu wa kuona kuna tatizo lakini huulizi au kusema kuna tatizo ili usionekane mbaya.

Uvivu huu pia unaenda kwenye kukwepa mazungumzo ambayo unajua ni muhimu, lakini pia yanaweza kukuumiza wewe au kumuumiza mwingine. Ni uvivu wa kutokuweka kujali sana kwenye kile unachofanya, unafanya juu juu na hutaki kuzama ndani na kuweka maisha yako yote kwenye kile unachofanya.

Uvivu huu unaweza kumpa mtu kile anachotaka kwa muda mfupi, kutokuumia yeye au kuumia mtu mwingine, lakini unatengeneza maumivu makubwa zaidi baadaye.

Pata picha pale mtu anaposhindwa kusema hapana kwa kuogopa kuwaumiza watu, anakuwa na ndiyo nyingi, vitu vingi vya kufanya kuliko uwezo wake, anashindwa kuvitekeleza na kuwaangusha watu. Kama angewaambia hapana au haiwezekani, angejipunguzia mzigo na watu hao wangepeleka mahitaji yao pengine.

Kila unapojaribu kukwepa kufanya kitu kwa sababu hutaki kuwaumiza wengine, jikamate mara moja, jua umeingia kwenye uvivu wa kihisia, uvivu ambao utakukwamisha sana kama hutachukua hatua.

Usiogope kuumia na wala usiogope kuwaumiza wengine, kama kitu ni sahihi, kitabaki kuwa sahihi iwe unachukua hatua au la. Hivyo ni vyema ukachukua hatua kwa sababu huwezi kushindana na ukweli na ukashinda.

Kazi za kihisia ndiyo kazi zinazowawezesha watu kupiga hatua zaidi, wale wanaokabiliana na kazi hizi bila ya hofu, ndiyo ambao wanakuwa huru zaidi na maisha yao na kuweza kufanya makubwa.

Usikubali uvivu wa kihisia uendelee kuwa mzigo kwako, chukua hatua kukabiliana na kila hisia na utaweza kuwa huru sana.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha