Siku mpya,
Siku bora,
Na siku ya kipekee sana kwetu.
Ni nafasi nzuri sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa, ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari MARA YA MWISHO KUFIKIRI MWENYEWE NI LINI?
Moja ya changamoto kubwa tunayokabiliana nayo kwenye zama tunazoishi sasa ni kutekwa kifikra.
Watu wengi wanadhani wanatumia akili zao kufikiri, kumbe akili zao zimetekwa na wanafikiri kile walichotengenezewa kufikiri na siyo kile ambacho ni muhimu kwao.
Kwa mfano umeianza siku yako, mara ghafla unakutana na habari fulani, basi siku nzima unafikiria kuhusiana na kilichotokea, unabishana, unatafuta kujua zaidi, unatoa na maoni yako na kadhalika.
Hapo hujafikiri, badala yake umeshikwa akili ufikiri yale yanayotokea.
Na hatari zaidi ni kwamba hakuna siku inaanza na kuisha bila ya kuibuka kitu au habari ambayo inawasisimua watu kuiongelea muda wote.
Rafiki, hebu jiulize kwa kina swali hili asubuhi ya leo, ni lini mara ya mwisho kwako kufikiri mwenyewe?
Ni lini umeamka na kuianza siku kwa ajenda zako, kufanyia kazi ajenda hizo kwa siku nzima na kupuuza mengine yanayoendelea?
Ni lini mara ya mwisho kwako kuzingatia yale uliyopanga wewe na kuyapa kipaumbele huku ukipuuza ambayo hukupanga?
Ni lini mara ya mwisho kwako kutuliza mawazo yako kwenye kile unachofanya, kwa muda mrefu, bila ya kufungua fungua simu yako na kuingia kwenye mitandao ya kijamii kuona nini kinaendelea, au kama wengi wanavyojiambia, wasipitwe?
Rafiki, kama ni siku nyingi hujafikiri wewe mwenyewe, unalemaza akili yako, mwishowe utaishia kutegemea watu wanafanya nini, wanasema nini au nini kinaendelea ndiyo na wewe uende nacho.
Na kama hujafikiri mwenyewe kwa muda mrefu, nikukumbushe kwamba kutokufikiri wewe mwenyewe, kuruhusu akili yako itekwe na kutumiwa na watu wengine, ni njia ya uhakika ya kushindwa kwenye maisha.
Rafiki, nina habari njema kwako, hata kama hujafikiri mwenyewe jwa muda mrefu, leo unayo nafasi ya kuanza kufikiri mwenyewe.
Ianze siku hii kwa ajenda zako binafsi, panga yale muhimu kwako.
Epuka kabisa habari zozote kwenye siku yako hii.
Usitembelee kabisa mtandao wowote wa kijamii.
Unapofanya kazi muhimu, zima kabisa simu yako au iweke kwenye ukimya na iweke mbali, usiifungue fungue kila mara.
Usijali wengine wanasema au kufanya nini, wewe kazana kufikiri na kufanya yale muhimu kwako.
Jaribu hilo kwa leo tu, halafu ona matokeo yake kwenye ufanisi na uzalishaji wako.
Na kama matokeo ni mazuri, kwa nini hayo yasiwe ndiyo maisha yako ya kila siku?
Ukawe na siku bora sana ya leo rafiki, siku ya kufikiri wewe mwenyewe, wa kuitawala akili yako badala ya kuwa mateka wa kifikra. Siku ya kuiendesha kwa ajenda zako mwenyewe.
#Fanya #HakunaSababu #NiLeoTu #IngiaMzimaMzima #AnzaNaHatuaMoja #MafanikioNiHakiYako #NidhamuMsingi #WhatEverItTakes #WachaManenoWekaKazi #SkinInTheGame #OwnTheDayOwnYourLife #UsileteSababuLetaMatokeo #MudaNiSasa
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha