Hongera sana mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana kwetu.
Ni nafasi ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari SIYO LAZIMA UWE NA MAONI KWENYE KILA JAMBO…
Kama kuna kitu kinawafunga wengi zama hizi basi ni wingi wa maoni.
Siku hizi kila mtu ana maoni kwenye kila jambo, bila ya kujali kama ni mtaalamu wa jambo hilo au la.
Kitendo tu cha mtu kuwa kwenye mitandao basi kinamfanya kuwa mtaalamu wa kila kitu.
Kuweza kuandika na kutoa maoni kwenye mitandao kunawafanya watu waone wanaweza kuchangia kila kitu, kukosoa kila kitu na kutoa maoni yao, ambayo wanaamini ni muhimu na kila mtu anapaswa kuyasikiliza na kuyazingatia.
Rafiki, maoni ni kama upepo tu, huwa yanapita na hakuna anayeyapa uzito mkubwa.
Hivyo jipumzishe kwenye kukimbilia kutoa maoni.
Siyo lazima uwe na maoni kwenye kila jambo,
Usione aibu kusema huna maoni,
Usijisikie vibaya kukaa kimya na kuwaacha wengine wakisema.
Dunia itaenda vizuri tu bila ya maoni yako.
Rafiki, kama hujaombwa ushauri au maoni, itakuwa vyema sana kama utakaa kimya na kuendelea na shughuli zako.
Rafiki, kama kitu huna utaalamu nacho, siyo mbobezi wa kitu hicho na huna taarifa za kutosha, ukiulizwa maoni yako usione aibu kusema huna maoni.
Siyo lazima uwe na maoni kwenye kila jambo, na kadiri unavyokuwa na maoni mengi, ndivyo unavyojibebesha mzigo mkubwa kwenye maisha yako.
Pia kama utakuwa bize sana na ndoto zako, kama muda wote utakuwa unafikiria unapigaje hatua kubwa zaidi, hutapata muda wa kuanza kuhangaika na maoni kwenye vitu ambavyo havikuhusu.
Hivyo kama kwenye kila jambo linalotokea na wewe una maoni yako, hebu anza kujichunguza kama kweli uko bize vya kutosha na mambo yako mwenyewe.
Jali mambo yako na utapunguza kujiingiza kwenye mambo ya wengine na kutoa maoni ambayo siyo muhimu, siyo sahihi na wala hayahitajiki.
Uwe na siku bora sana ya leo, siku ya kupunguza maoni unayotoa kwenye mambo yasiyokuhusu.
#Fanya #HakunaSababu #NiLeoTu #IngiaMzimaMzima #AnzaNaHatuaMoja #MafanikioNiHakiYako #NidhamuMsingi #WhatEverItTakes #WachaManenoWekaKazi #SkinInTheGame #OwnTheDayOwnYourLife #UsileteSababuLetaMatokeo #MudaNiSasa
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha