Rafiki yangu mpendwa,

Nimekuwa nakuambia kwamba kwenye mafanikio, bahati ni pale fursa inapokutana na maandalizi. Kile ambacho watu wa nje wanakiona ni bahati kwa wale waliofanikiwa, huwa hawayaoni maandalizi makubwa ambayo watu hao wamekuwa wameyaweka kwa muda mrefu kabla ya kukutana na fursa hiyo.

Lakini pia bado kuna bahati nyingine ambazo huwa zinakutana na kila mtu, na kuna watu wanaziona bahati hizi wakati wengine hawazioni bahati hizo. Sasa kwa wale wanaoona bahati ambao wamekutana nazo na kuzitumia, huwa wanapata mafanikio kiasi, lakini wanafikiri mafanikio yale wameyapata kwa ujanja na nguvu zao, hivyo wanajiamini kupita kiasi kitu ambacho kinawapeleka kwenye anguko kubwa.

cropped-mimi-ni-mshindi

Wacha nikupe mfano mmoja wa utapeli ambao kwa siku za nyuma watu walikuwa wanautumia sana, na wengi waliumia.

Mtu anawasiliana na wewe, anakuambia sehemu alipo kuna bidhaa fulani ambayo inapatikana kwa urahisi na kwa bei nzuri, hivyo ukinunua na ukaiuza kule ulipo wewe, itakulipa sana. Anakushawishi sana utume hata fedha kidogo tu ya kujaribu biashara hiyo, na wewe unaona wacha ujaribu kwa kiasi kidogo cha fedha, ambacho hata kikipotea hakitakuumiza sana.  Basi unatuma fedha, kisha unatumiwa mzigo, unauuza na kupata faida. Unaanza kutengeneza imani.

Safari ya pili anakuambia sasa tuma kiasi kikubwa zaidi ili upate mzigo mkubwa zaidi na faida kubwa zaidi. Unakuwa bado hujapata uhakika sana, unaongeza kiasi kidogo, ambacho pia hakikuumizi sana, unatumiwa mzigo, unauza na kupata faida kubwa. Hapa sasa unaanza kujiamini, unaanza kujiona ni mjanja wa biashara, unaanza kuona una maamuzi mazuri kibiashara.

Sasa mwenzako anakuambia fursa ndiyo hii, chukua mzigo mkubwa zaidi, na wewe umeshajiamini zaidi, unachukua fedha zako zote, unaweza hata kukopa fedha zaidi, ukiwa na uhakika mzigo ukiingia unalipa zote hata kama ni kwa riba. Unatuma fedha ukijua utapokea mzigo mkubwa zaidi, na hapo ndipo unakuja kujifunza somo chungu sana, fedha yote inakuwa imepotea, uliyemtumia alikuwa anakupanga ili kukutapeli.

SOMA; Huyu Ndiye Tapeli Mkubwa Anayewalaghai Watu Wengi Katika Maisha Yao.

Nimekupa mfano huu kwa sababu hata kwenye maisha ya kawaida ndivyo mambo yanavyoenda. Kuna bahati fulani ambazo watu wamekuwa wanakutana nazo, halafu wanajisahau na kuona ni ujana wao, kitu kinachowaumiza sana baadaye.

Nikupe mfano mwingine, mwaka mmoja umelima mahindi yako, kwenye eneo ambalo halikuwa na changamoto kubwa sana, ukavuna vizuri na kuyahifadhi. Sasa wakati uko na mahindi yako, ukasikia habari kwamba bei za mahindi zinapanda sana maana maeneo mengi mahindi hayajatoka vizuri. Kwa kuwa huna haraka ya kuuza, unasubiri, mara bei zinapanda kweli kweli, na kuwa mara mbili ya bei uliyotegemea awali. Baadaye unachukua hatua ya kuuza mahindi yako na unapata faida kubwa mno.

Hapa sasa unapata kujiamini, unajiona wewe ni mkulima bora, unayejua kuweka ‘timing’ nzuri ya kulima na hata kuuza. Unarudi shambani ukiwa na hamasa kubwa, unaweka fedha zote na hata nyingine za kuchukua kwa watu, ukiamini mambo yatakuwa kama msimu uliopita. Unavuna mahindi yako vizuri, na kuyahifadhi, ukisubiria bei ipande. Lakini msimu huo wengi wanakuwa walivuna mahindi na yakatoka vizuri. Hivyo bei hazipandi, na kila unapoendelea kusubiri, bei zinazidi kupungua. Mwishowe unapata hasara kubwa na kupoteza fedha.

Rafiki, sikuambii haya kwa lengo la kukukatisha tamaa, au kukuogopesha, bali nakuandikia haya ili kuiwezesha akili yako ifikiri sawasawa.

Kwa kila mafanikio kidogo unayopata, jiulize je ni kwa juhudi na akili zako au kuna bahati fulani iliyoingia na kupelekea mafanikio hayo. Kama ni kwa juhudi na akili zako basi endelea kuweka juhudi na akili hizo. Lakini kama kuna bahati iliingia mahali, basi kuwa makini usichanganye bahati hiyo na akili na juhudi zako.

Kama palikuwa na bahati, jua ni kwa namna gani utaweza kupata tena matokeo uliyopata kwa akili na juhudi na siyo kwa bahati. Hii ni kwa sababu bahati huwa zinatokea mara moja na hazitabiriki, lakini akili na juhudi ni vitu unavyokuwa navyo mara zote na unaweza kuvitumia kupata matokeo bora wakati wote.

SOMA; Sababu Tatu Kwa Nini Mafanikio Madogo Yanakuwa Sumu Ya Wewe Kufikia Mafanikio Makubwa Zaidi Na Jinsi Ya Kuziepuka.

Usileweshwe na mafanikio kidogo ukajisahau, maana hali hiyo imewaangusha wengi. Tafakari kwa kina kila mafanikio unayoyapata, angalia nafasi ya bahati kwenye mafanikio hayo na jinsi gani unaweza kuyarudia mafanikio hayo kwa usahihi bila ya kufanya makosa na ukapoteza.

Kamwe usilewe mafanikio ya aina yoyote ile, yakakufanya uache kutumia akili na juhudi zako mara zote. Hata kama kitu umekizoea kiasi gani, usifanye kwa mazoea, badala yake fikiri kwa kina na hakikisha unaweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.

Kila hatua unayopiga kwenye maisha yako, kuna mchango fulani unaotokana na bahati, elewa mchango huo na ona ni jinsi gani utaugeuza kwenda kwenye juhudi na akili.

Makala hii imeandikwa na Kocha Dr Makirita Amani.

Dr. Makirita ni Daktari wa binadamu, Kocha wa mafanikio, Mwandishi na Mjasiriamali.

Dr. Makirita anaendesha mafunzo ya mafanikio kwa wale waliojitoa hasa kufanikiwa kupitia program ya KISIMA CHA MAARIFA.

Kama bado hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA, tuma sasa ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa njia ya wasap namba 0717 396 253 (tumia wasap tu)

Kupata huduma nyingine za ukocha tembelea www.amkamtanzania.com/kocha

Kupata vitabu vizuri vya kusoma tembelea www.amkamtanzania.com/vitabu