Watu wamekuwa wanaambiwa wayafurahie maisha kama yalivyo, wapokee kila wanachokutana nacho na kukitumia kama kilivyo. Hakuna ubaya wowote kwenye hili, lakini linakufanya uwe na maisha ya kawaida.

Njia pekee ya kuwa na maisha ya kipekee, maisha bora na ya mafanikio makubwa kwako, siyo kwa kufurahia maisha kama yalivyo, bali kwa kuyatengeneza maisha yako kwa namna ambayo utayafurahia.

Kila mmoja wetu ana ndoto tofauti za maisha yake, kila mmoja wetu kuna vitu anavijali zaidi kwenye maisha. Kama kila mtu angekazana kuishi kulingana na ndoto zake, basi maisha ya wengi yangekuwa bora sana.

Lakini wengi wanashindwa kuishi kulingana na ndoto zao, na wanaishia kuwa na maisha ya kawaida, maisha ambayo kila mtu anayo, kwa sababu wamejifunza kupokea maisha kama yanavyokuja kwao.

Ili kutengeneza maisha ambayo yanaendana na ndoto zako, maisha ambayo utayafurahia, itakulazimu pia kuishi tofauti kabisa na wanavyoishi watu wengine. Itakulazimu kufanya vitu ambavyo watu wengine hawafanyi. Itakulazimu kujiumiza zaidi, kwenda hatua ya ziada zaidi, itakubidi kuahirisha baadhi ya starehe na mapumziko.

Wengi hawapo tayari kwa maisha hayo magumu wakati wanatengeneza maisha ya ndoto zao, ndiyo maana wanakubaliana na yale maisha ambayo kila mtu anayo, wanaishia kuwa na maisha ya kawaida, ambayo hawayafurahii na wanakuwa kama wamenasa kwenye mtego kwa sababu wanakuwa hawana cha kufanya.

Kutengeneza maisha unayoyafurahia pia haimaanishi kwamba unakosa shukrani kwa kile ulichonacho au unachopata, bali unajua kwamba unaweza kwenda zaidi ya hapo na unachukua hatua za kufanya zaidi. Unafanya zaidi kwa sababu unajua ipo ndani ya uwezo wako na pia inawezekana, hivyo unajitoa kufanya zaidi.

Ndoto yoyote uliyonayo kubwa kuhusu maisha yako, kwanza jua kitu kimoja, inawezekana, na pia jua kuna gharama ya kulipa ili kuweza kufikia ndoto hiyo. Kama utakuwa tayari kulipa gharama hiyo, utaweza kutengeneza maisha yako na siyo kupokea maisha kama yalivyo.

Utamu na uzuri wa maisha ni pale ndoto zako zinapokuwa uhalisia, pale maono yako yanapokuwa kweli, na pale maisha yako yanavyokuwa kama ulivyopanga yawe. Kitu ambacho kinatokea kama mtu utaweka juhudi kubwa na kutokukata tamaa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha