Mpendwa rafiki yangu,

Tunapaswa kuelewa kuwa sisi binadamu ni viumbe vya hisia na hakuna kitu kibaya sana kama kumuumiza binadamu kihisia kwa sababu unamwachia uchungu ndani ya moyo. Ni heri kumchapa mtu fimbo maamivu yataisha mara moja lakini siyo maneno. Maneno yanaumiza na yanakaa sana moyoni hivyo sisi kama binadamu tunatakiwa sana kuchunga maneno yetu kwa sababu kile kinachotoka kila mtu ana kitafsiri vile anavyojua yeye na bahati mbaya ni kwamba hatuna uwezo wa kukirudisha  kile tulichoongea.

Uongozi ni asili ya binadamu, tangu enzi na enzi na mpaka sasa uongozi ulikuwepo na utaendelea kuwepo. Kama umeshindwa kujiongoza mwenyewe basi kuna mtu atakuongoza. Na habari njema ni kwamba kila mtu ni kiongozi wa maisha yake mwenyewe, kiongozi mzuri ni yule anayejiongoza yeye mwenyewe vizuri.

Hakuna kitu hatari sana katika uongozi kama upendeleo na maamuzi ya kujiangalia wewe na siyo watu wengine. kabla hujamfanyia mtu kitu hebu vaa viatu vyake kwanza, ukiona vinakuumiza basi usimfanyie mwingine hicho kitu ulichotoka kufanya kwa sababu unachomfanyia mwenzako sheria ya asili ya karma itakurudia. Naye kama unawafanyia wenzako ubaya lazima ule ubaya utakarudia na malipo yake ni hapa duniani

golden_rules1

Kama wewe ni kiongozi kuanzia katika ngazi ya familia tafadhali, kazi au kampuni fulani tafadhali usiweke upendeleo kwa wafanyakazi wako hata kama kuna mtu anakupendeza zaidi iwe ni siri yako siyo kuonesha kwa watu wote kwa sababu upendeleo unavunja nguvu watu wengine. Hata kama ni katika taasisi watu wataacha kuweka zile juhudi walizokuwa wanaweka mwanzoni. Upendeleo unavunja watu moyo, ukiwa kiongozi kuwa mtu wa haki.

SOMA; Hii Ndiyo Njia Pekee Ya Wewe Kuacha Alama Hapa Duniani Na Kuishi Milele Hata Baada Ya Kufa Kwako.

Upendeleo sehemu yoyote haujawahi kumuacha mtu salama, upendeleo unaleta mpasuko mkubwa sana. wape watu haki sawa, wape uhuru wa kuchagua kile wanachotaka, unaweza kumchagulia mtoto mdogo lakini huwezi kumchagulia na kumuamulia mtu mzima kile anachotaka.

Uongozi wako kuanzia eneo la familia yako mpaka eneo la kazi unatakiwa kutenda haki na kusimamia ukweli na epuka upendeleo.

Hatua ya kuchukua leo. Upendeleo ni kitu hatari katika ngazi yoyote ile, unaleta mpasuko baina ya wale unaowaongoza hivyo ongoza kwa kufuata demokrasia na haki.

Hivyo basi, wape watu nguvu ya kusikilizwa, wasikilize na watoe maoni yao. Wafanye watu wajihisi wanathaminiwa kadiri walivyo hii itawapa hamasa kubwa ya kufanya kazi.

Ukawe na siku bora sana ya leo rafiki yangu.

Rafiki na mwalimu wako,

Deogratius Kessy

0717101505/0767101504

deokessy.dk@gmail.com , kessydeo@mtaalamu.net

Unaweza kutembelea tovuti yangu kwa kujifunza zaidi kila siku na kupata huduma mbalimbali kama vile vitabu, kwa kutembelea tovuti  hii  hapa  www.mtaalamu.net/kessydeo .

Asante sana na karibu sana