Kadiri kelele za dunia zinavyozidi kuwa kubwa, ndivyo amani ya ndani inavyozidi kupungua kwa wengi.
Wengi hawana amani na utulivu wa ndani, hawana utegemezi wa ndani yao kwa maisha mazuri na ya furaha.
Wengi wanaishia kubabaishwa na kelele zinazoendelea kwenye dunia, kelele ambazo hazidumu, ni za kupita na zikishapita zinajazwa na kelele nyingine.
Ukitaka kuliona hili vizuri angalia mwenendo wa habari za kusisimua, kila siku kunakuwa na habari mpya ya kusisimua, kila siku dunia inakuandalia kitu cha kusisimua akili yako na kuyaweka mawazo yako ‘bize’ kufikiria habari hizo zinazoendelea.
Angalia upande wa pili kwenye mitandao ya kijamii, watu wanavyotamani kuona kila kinachoendelea kwenye maisha ya wengine, jinsi ambavyo watu wengi hawataki kupitwa. Na wapo wanaosema kabisa bora wakose chakula lakini siyo kukosa ‘bando’ la kuingia kwenye mitandao hii. Na hata baada ya kuingia kwenye mitandao, bado wengi kiwango cha furaha hakiongezeki, badala yake kinashuka zaidi. Utasikia watu wakilalamika kabisa kwamba hakuna jipya kwenye mitandao, au kujisikia vibaya kwa kupoteza muda mwingi kwenye mitandao hii, lakini bado hawaachi kuitumia na kupoteza muda zaidi.
Rafiki yangu, tiba ya hali hii wanayoipitia wengi siyo kelele zaidi, maana watu wamekuwa wanahama kelele moja kwenda nyingine. Mfano mtu anajiambia hakuna jipya mtandaoni anaenda kwenye tv, au hakuna jipya kwenye tv anaenda kwenye kijiwe na kupiga soga.
Rafiki, tiba ya kurejesha amani ya moyo na utulivu wa ndani ni kufanya vitu hivi vitatua ambavyo vinaendana na ni muhimu;
Moja; UKIMYA.
Kukaa kimya kuna umuhimu mkubwa sana kwenye maisha yako, kadiri unavyokaa kimya, ndivyo unavyoiwezesha akili yako kufikiri vizuri, ndivyo unavyojifunza kupitia wengine. Wanasema unapoongea hujifunzi kitu kipya, lakini unapokuwa kimya, unajifunza mengi.
Mbili; UPWEKE.
Jamii tunayoishi sasa inaupa ukweke taswira mbaya, upweke unaonekana kama ugonjwa au kutengwa, kitu ambacho kinawafanya wengi kupambana nao hasa. Mtu yupo tayari kufanya chochote ili tu asijione mpweke. Wakati hakuna kitu kizuri kwenye maisha kama upweke. Kuna wakati unahitaji kuwa wewe peke yako, ukiwa huna cha kufanya na wakati huu ni mzuri kwako kutafakari maisha yako, unapotoka, ulipo na unapokwenda. Huwezi kufanya tafakari ya kina ukiwa una usumbufu unaoendelea kwenye maisha yako.
Tatu; UTULIVU.
Tunaishi dunia ya kasi, dunia ya haraka, dunia isiyo na subira, lakini pia ni dunia inayohitaji utulivu wa hali ya juu sana. Usisukumwe na presha za nje kufanya mambo ambayo hujayatafakari kwa kina. Unahitaji utulivu mkubwa katika kufikiri kwa kina na kufanya maamuzi sahihi. Utulivu utakuwezesha kufanya maamuzi bora ambayo yatakuletea amani ya moyo na utulivu wa ndani yako.
Rafiki, vitu hivyo vitatu havihitaji uwe na kitu cha ziada kwenye maisha yako ndiyo uweze kuvifanyia kazi, vitu hivyo vitatu havihitaji yeyote akusaidia kuvifanyia kazi. Ni wewe kuamua na kuanza kuvifanyia kazi kila siku kwenye maisha yako. kuwa kimya, kupata muda wa kuwa peke yako na kuwa na utulivu hasa unapoelekea kufanya maamuzi muhimu ya maisha yako.
Fanya hayo matatu rafiki yangu na utaondoka kwenye kelele za dunia zinazowapa wengi msongo wa mawazo.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,