“Discipline is the bridge between goals and accomplishment.” – Jim Rohn

Ni siku mpya,
Siku bora na ya kipekee sana kwetu.
Tumepata nafasi nyingine nzuri sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari DARAJA KATI YA MALENGO NA MAFANIKIO…
Lipo daraja linalounganisha malengo yako na mafanikio yako,
Bila ya daraja hili, huwezi kupiga hatua yoyote na huwezi kufanikiwa.
Na daraja hili lisipokuwa imara, hatua yoyote utakayopiga, utaanguka.

Daraja tunalozungumzia hapa ni NIDHAMU,
Bila ya nidhamu, tena nidhamu hasa, malengo yoyote unayojiwekea ni hadithi za kujifurahisha.
Nidhamu ndiyo inayokusukuma kuchukua hatua hata kama huoni matokeo mazuri kwa wakati huo.
Nidhamu ndiyo inayokusukuma kusonga mbele hata kama kuna ugumu.
Nidhamu ndiyo inakuwezesha kuwapuuza wale wanaokukatisha tamaa na kukurudisha nyuma.

Tunahitaji sana kuwa na daraja hili muhimi,
Na pia tunapaswa kuimarisha daraja hili kila siku ili kuweza kufanikiwa.

Nidhamu ni kufanya kile ulichopanga kufanya, kwa wakati uliopanga kufanya bila ya kuruhusu sababu yoyote kukuzuia.
Nidhamu ni kufanya licha ya kuwa na kila sababu ya kutokufanya.
Nidhamu ni kuusukuma mwili wako hata kama hautaki kwenda.
Nidhamu ni kuamua kufanya, inyeshe mvua au liwake jua, umechagua kufanya na utafanya.
Na nidhamu ni maamuzi ya kupata kile unachotaka au kufa ukikitafuta.

Bila ya nidhamu, ugumu uliopo kwenye safari ya mafanikio, vishawishi vya kuacha unachofanya sasa na ufanye vitu vingine havitakuacha salama.
Kila siku imarisha sana msuli wako wa nidhamu.
Na kila unaposema hapana kwa vishawishi na uvivu, kila unapojiambia nitafanya kesho, lakini ukakataa na ukafanya leo, msuli wako wa nidhamu unaimarika zaidi.
Imarisha msuli wako wa nidhamu na utawesa kufikia mafanikio makubwa sana kwenye maisha yako.

Ukawe na siku bora sana kwako leo, siku ya kuimarisha zaidi nidhamu yako kwa kufanya yale yote uliyopanga kufanya na kuyafanya kwa viwango vya juu.
#Fanya #HakunaSababu #NiLeoTu #IngiaMzimaMzima #AnzaNaHatuaMoja #MafanikioNiHakiYako #NidhamuMsingi #WhatEverItTakes #WachaManenoWekaKazi #SkinInTheGame #OwnTheDayOwnYourLife #UsileteSababuLetaMatokeo #MudaNiSasa

Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha