Hongera sana mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana kwetu.
Ni nafasi bora na ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari GHARAMA YA KUDANGANYA…
Kudanganya,
Kuishi maisha ya uongo au ya kuigiza,
Kusaliti na hata kutapeli,
Kuna gharama kubwa sana kwenye maisha yako.

Gharama hiyo ni kwamba inakubidi uishi maisha ya aina mbili au zaidi, kitu ambacho siyo rahisi hata kidogo.
Kuishi maisha hayo ya aina moja tu uliyonayo ni changamoto kwako, je vipi kuishi maisha ya aina mbili?
Kuwa wewe mwenyewe tu ni changamoto, je vipi kujaribu kuwa mtu mwingine?

Kudanganya kunakulazimu uishi maisha ya maigizo, maisha ya kutengeneza, ambayo ni maisha magumu sana kwa yeyote.
Kudanganya kunakutaka utunze kumbukumbu za yote uliyodanganya, na kila wakati ujikumbushe kama hujawahi kusema kitu cha tofauti na kile unachokwenda kufanya.
Pia kudanganya kunakufanya uendelee kudanganya zaidi, kwa sababu uongo mdogo unafunikwa na uongo mkubwa.
Wengi huanza na uongo mdogo lakini mwishoni hujikuta kwenye uongo mkubwa ambao hawawezi kuendelea kuutunza.

Rafiki, ni ukweli pekee ambao utakuwekw huru kwenye maisha yako,
Ni uaminifu na uadilifu pekee utakaoyafanya maisha yako yawe huru nw rahisi kwako kuyaishi.
Pale ambapo huhitaji kuigiza chochote, pale ambapo huhitaji kutaka kuonekana tofauti na ulivyo, huhitaji kutumia nguvu yoyote kuwashawishi watu kitu cha tofauti.

Nguvu ulizonazo kama utazipeleka kwenye kufanya yale muhimu kwako, ukaacha kuzipoteza kwenye uongo na maisha ya maigizo, utaweza kupiga hatua kubwa sana kwenye maisha yako.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuishi ukweli, kuwa mwaminifu na mwadilifu na kuepuka kila aina ya uongo au maisha ya maigizo.
#Fanya #HakunaSababu #NiLeoTu #IngiaMzimaMzima #AnzaNaHatuaMoja #MafanikioNiHakiYako #NidhamuMsingi #WhatEverItTakes #WachaManenoWekaKazi #SkinInTheGame #OwnTheDayOwnYourLife #UsileteSababuLetaMatokeo #MudaNiSasa

Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha