“Choose what is best, and habit will make it pleasant and easy.” — Plutarch

Tuna siku nyingine mpya kabisa mbele yetu.
Ni siku ambayo tumepata nafasi mpya na ya kipekee kwetu kwenda kufanya makubwa zaidi.
Ni siku ambayo ina kila linalowezekana kwetu, kama tu sisi wenyewe tutachukua hatua sahihi kwenye siku hii.

Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari TABIA ITARAHISISHA MAMBO…
Unapoanza kufanya jambo lolote jipya, mwanzo huwa ni mgumu sana, kitendo tu cha kufikiria kufanya kitu hicho kipya, kinakuchosha.
Kwa sababu unafikiria kila kinachohusika kwenye kufanya kitu hicho.
Unajikuta unaona vitu vya kufanya ni vingi mno kiasi cha kuchoka kabla hata ya kuanza.

Lakini akili zetu na miili yetu ina njia bora ya kutuwezesha kuendelea kufanya jambo hata kama ni gumu kiasi gani.
Na inachofanya ni kutengeneza tabia.
Kila kitu ambacho ni kigumu kufanya mwanzo, baada ya muda huwa kinakuwa rahisi kwa sababu ya tabia.
Akili na mwili vinatengeneza tabia ambayo inapunguza wewe kufikiria kika hatua, vitu vingi unavifanya bila hata ya kufikiria.

Pata picha wakati unajifunza kuendesha chochote, iwe ni baiskeli, gari au hata mashine. Mwanzo ulikuwa unaona ni ngumu na kila hatua uliifikiria, ulipokanyaga breki ulitaka uiangalie ndiyo ukanyage, lakini pia wakati huo huo unaacha kuangalia mbele. Hukuweza hata kuongea na mtu mwingine wakati unaendesha, akili yako yote ilikuwa kwenye kile unachoendesha.

Lakini baada ya muda unajikuta unaendesha bila hata ya kifikiria, unajikuta unaendesha huku unaongea na watu wengine au kufikiria mambo mengine na hupati changamoto kubwa.

Hivyo rafiki, chochote ambacho kinakusumbua mwanzoni, ambacho ni muhimu ufanye lakini unaona kama huwezi kufanya, jua huo ni mwanzo tu. Baada ya muda tabia itajengeka na haitakuwa tena vigumu kwako kufanya.
Na njia pekee ya kujenga tabia siyo kwa kujifunza, bali kwa kuendelea kufanya.
Kadiri unavyorudia rudia kufanya, ndivyo akili na mwili wako unakariri vile unavyorudia rudia mara nyingi na kuviingiza kwenye sehemu ya vitu unavyoweza kufanya bila hata ya kufikiri.
Ikishakuwa tabia, inakuwa ni kitu mwili unaweza kufanya wenyewe bila ya wewe kufikiri sana.

Kadhalika, tabia mbaya pia zinajengwa hivi, hivyo kama kuna tabia mbaya unataka kuivunja, fanya kinyume na namna ya kujenga tabia. Acha kufanya kitu hicho na baada ya kuda akili na mwili vinasahau.

Ukawe na siku bora sana kwako leo, siku ya kujijengea tabia imara ya kukuwezesha kufikia mafanikio makubwa.
#Fanya #HakunaSababu #NiLeoTu #IngiaMzimaMzima #AnzaNaHatuaMoja #MafanikioNiHakiYako #NidhamuMsingi #WhatEverItTakes #WachaManenoWekaKazi #SkinInTheGame #OwnTheDayOwnYourLife #UsileteSababuLetaMatokeo #MudaNiSasa

Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha