Dhumuni kuu la biashara ni kutengeneza wateja, na lengo la biashara baada ya kuwa na wateja ni kutengeneza faida.
Kama biashara haitengenezi faida, haiwezi kudumu kwa muda mrefu, itaishia kuanguka na kufa.
Wafanyabiashara wengi wamekuwa hawapo makini na namba zao za kibiashara, hasa upande wa faida. Huwa wanafurahi kuona fedha zipo kwenye biashara, ila hawajui kama ni mauzo au faida.
Zipo njia kuu mbili za kutengeneza faida kwenye biashara;
Njia ya kwanza ni kuwa na gharama ndogo za uzalishaji na uendeshaji wa biashara. Na hapa ndipo makini, ndipo faida yote huwa inapotelea, hasa pale gharama za kuendesha zinapokuwa kubwa na ushindani unakuwa mkali. Unapoweza kuendesha biashara yako kwa gharama ndogo zaidi, hata ushindani ukiwa mkali na bei kuwa chini, bado utabaki na faida nzuri.
Njia ya pili ni kuuza kitu ambacho hakipatikani sehemu nyingine yoyote ile. Kama unachouza kinapatikana kwako tu, na watu wanakihitaji, unajiweka kwenye nafasi ya kuuza vizuri na hivyo kutengeneza faida nzuri. Kadiri kitu kinavyokuwa adimu kupatikana, ndivyo thamani yake inavyokuwa kubwa.
Sasa nataka nikupe siri ambayo itakusaidia kuongeza faida mara dufu kwenye biashara yako, njia hiyo ni kufanyia kazi njia hizo mbili kwa pamoja.
Hapa unahitaji kuuza kitu ambacho hakuna mwingine anayeuza au kuuza kwa namna ambayo wengine hawawezi kuuza na pia kufanya gharama zako za kuendesha biashara kuwa chini sana.
Kwa kutumia njia hizi mbili kwa pamoja, utaweza kutengeneza biashara imara, yenye faida nzuri na inayokua.
Kila siku jiulize swali hili muhimu, nawezaje kujitofautisha zaidi na nawezaje kupunguza gharama za kuendesha biashara? Ukipata majibu hayo na kuboresha kila siku, utapiga hatua sana kibiashara.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,