“Receive wealth or prosperity without arrogance; and be ready to let it go.” – Marcus Aurelius.

Siku mpya,
Siku bora,
Na siku ya kipekee sana kwetu.
Ni nafasi nyingine nzuri sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari KIBURI NI SUMU…
Watu wengi wanapoanzia chini, huwa wanakuwa wanyenyekevu sana,
Huwa wanakuwa tayari kujifunza, wanakuwa tayari kujituma zaidi na hilo linawaweka kwenye nafasi ya kupiga hatua zaidi.

Lakini kadiri wanavyopiga hatua na kuanza kufanikiwa, hapo ndipo shida kwa wengi huanza.
Wengi huanza kuwa na kiburi,
Wengi huanza kuona wanajua kila kitu, hawahitaji tena kujituma kama awali, kwa sababu wameshapiga hayua fulani kwenye maisha yao.

Hii ndiyo sumu kubwa sana ambayo inawaangusha wengi, sumu inayowazuia wengi kupiga hatua.
Haijalishi upo kwenye hatua ipi ya maisha yako, epuka sana kiburi, epuka sana ujuaji na mara zote, kazana kuweka juhudi zaidi.
Kila unavyozidi kupiga hatua, jilazimishe kuwa kama vile ndiyo unaanza.
Kwa kuwa kwenye hali ya anayeanza mara zote, kunakuweka kwenye nafasi ya kuzidi kupiga hatua zaidi.

Epuka sumu ya mafanikio inayowaangusha wengi, ambayo ni kiburi.
Chochote unachopata kwenye maisha yako, jua unaweza kukipoteza pia.
Hivyo usiweke utu wako au thamani yako kwenye nini unamiliki.
Badala yake thamani yako iweke ndani yako, kwa kujua uwezo mkubwa uliopo ndani yako, vipaji ulivyonavyo na kukazana kuvitumia kila siku.

Kama utajiona hujakamilika mpaka uwe na vitu fulani unavyotaka, unajiweka kwenye nafasi ya kuwa na maisha ya hovyo sana. Kwa sababu hakuna chochote ulichonacho, ambacho kitadumu na wewe milele.

Ukawe na siku bora sana ya leo rafiki, siku ya kuepuka sana kiburi, siku ya kufanya kama vile ndiyo unaanza, na siku ya kuwa tayari kupoteza chochote ulichonacho.
#Fanya #HakunaSababu #NiLeoTu #IngiaMzimaMzima #AnzaNaHatuaMoja #MafanikioNiHakiYako #NidhamuMsingi #WhatEverItTakes #WachaManenoWekaKazi #SkinInTheGame #OwnTheDayOwnYourLife #UsileteSababuLetaMatokeo #MudaNiSasa

Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha