Mazingira yetuyana vitu vingi mno kuliko uwezo wetu wa kuona kila kitu.
Hivyo akili zetu zimejifunza kuona vile vitu ambavyo ni muhimu zaidi kwetu.
Na kitu cha kwanza akili zetu zinatuwezesha kuona ni hatari mbalimbali, ndiyo maana kitu cha hatari tunakiona haraka na hofu huwa ni kubwa.
Pia akili zetu hutuwezesha kuona kile ambacho tunakifikiria muda mrefu, kile ambacho kimetawala fikra zetu.
Unaweza kuwa unapita eneo fulani kila siku, lakini usione fursa fulani ambayo ipo. Lakini akili yako inapoanza kufikiria kuhusu fursa fulani, unaanza kuona fursa hizo kwenye maeneo ambayo hukuwa unaziona awali.
Haya siyo maajabu, ni jinsi akili yetu inavyofanya kazi, kwa kuwa na vipaumbele.
Hivyo kwenye maisha yako, kitu cha kwanza unachopaswa kuwa nacho makini sana ni kujua nini unatafuta, kipi ni muhimu zaidi kwako, nini unakifikiria muda wote.
Kwa sababu hata ufanyeje, kile unachofikiria sana ndiyo utakachokipata, hata kama hukitaki.
Yaani rafiki, kama hujanielewa ni hivi, kama unachukia sana kushindwa, na muda wote unajikumbusha kwamba hutaki kushindwa, akili yako haielewi kwamba unachukia kushindwa, yenyewe inaelewa kwamba kushindwa ni kitu muhimu zaidi kwako, ndiyo maana unakifikiria muda wote. Hivyo inakutengenezea mazingira ya kushindwa, ili kutimiza matakwa ya mawazo yako.
Kama hutaki kushindwa, ondoa kabisa fikra za kushindwa kwenye akili yako, peleka mawazo yako yote kwenye ushindi, jione kwenye picha ya ushindi wako, ona umeshapata kila unachotaka na tumia picha hii muda wote. Akili yako itakuletea mazingira ya kutimiza kile unachofikiria kwa muda mrefu.
Rafiki, kauli ya unaona kile unachotafuta ni kauli rahisi sana kuisema, lakini imebeba maana nzito sana. Yaani kama hutajifunza chochote kwenye maisha yako, kama hutakazana na kingine, basi fanya hichi kimoja, ijaze akili yako na fikra zako picha za kile unachotaka, namna ambavyo unataka maisha yako yawe.
Akili yako, yenye nguvu kubwa mno, itakuletea kila aina ya mazingira na fursa unazotaka ili kupata kile ambacho unakitaka, kile unachokifikiria muda wote.
Usipoteze muda wako kufikiria vitu ambavyo huvitaki, haina maana kwako na itakuletea vile usivyotaka.
Tawala fikra zako kwa picha na taswira za kila unachotaka, na kwa hakika utapata kile unachotaka.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,