Rafiki yangu mpendwa,
Kwenye maisha huwa wapo watu ambao wanaonekana kama wana bahati sana. Watu hawa, kila wanachokigusa huwa kinageuka na kuwa mafanikio makubwa. Hawa ni watu ambao huwa wanaanzia chini kabisa na kuweza kufikia mafanikio makubwa.
Wakati kwa nje wanaweza kuonekana ni bahati zinawasaidia, kwa ndani bahati ina nafasi ndogo sana. Kwa ndani watu hawa huwa wanakuwa na kanuni ambayo wanaifuata, kanuni inayowatengenezea mpenyo wa mafanikio makubwa sana kwenye maisha yao.
Cha kushangaza, wengi huwa hata hawajui kama wanafuata kanuni, wao wanakuwa tu wanafanya mambo yao na mwisho wa siku wanakutana na mafanikio makubwa. Wanakuwa wanajua yale muhimu kwao na kuyafanya, ila hawajui kwamba ni kanuni wanaifuata.
Sasa rafiki yangu mpendwa, leo nataka nikushirikishe kanuni hiyo muhimu ambayo kama wewe utaamua kuifuata, utaweza kutengeneza mpenyo wa mafanikio makubwa kwenye maisha yako. kanuni siyo ngumu, haihitaji uwe na elimu kubwa au fedha nyingi, bali kanuni inakutaka uwe umejitoa sana na kuwa tayari kufanya kila unachopaswa kufanya ili kupata unachotaka.
Kanuni ya kutengeneza mpenyo wa mafanikio makubwa kwenye maisha yako una viungo vikuu vitano;
Moja; KUJUA KWA NINI YAKO.
Kitu cha kwanza kabisa unachopaswa kujua ni KWA NINI YAKO, ni nini hasa unachotaka kwenye maisha yako. Kadiri kwa nini yako inavyokuwa kubwa na ya kuhamasisha, ndiyo unavyopata nguvu ya kuchukua hatua zaidi na kuweza kufanikiwa zaidi.
Jua nini hasa unachotaka kwenye maisha yako, kuwa na ndoto na maono makubwa na maisha yako na tengeneza taswira ambayo unajiona ukiwa umeshafika pale ulipofika. Taswira hii itakuwa msukumo kwako kuchukua hatua kubwa.
Mbili; TENGENEZA MATUMAINI.
Safari ya kupata kile unachotaka kwenye maisha yako haitakuwa rahisi, dunia haitakuachia kirahisi ufanye kila unachotaka. Utakutana na vikwazo, changamoto na magumu mbalimbali. Kuna wakati utajiona kama umekosea kila ulichokuwa unafanya. Utafikia hatua ya kukata tamaa na kuona haina haja ya kuendelea tena.
Kitu pekee kitakachokuwezesha kuendelea unapofika kwenye hali kama hii ni matumaini uliyoyatengeneza kwenye maisha yako. Kadiri unavyokuwa na matumaini makubwa kwenye kile unachotaka na kwako binafsi, ndivyo unavyopata hamasa ya kuendelea zaidi hata kama mambo ni magumu.
Wale wanaokutana na magumu sana lakini bado wanaendelea siyo kwamba ni mashujaa zaidi au wana nguvu zaidi, bali wana matumaini.
Tatu; CHOCHEA HAMASA.
Hamasa ni kama moto, usipouchochea huwa unazima. Ili moto uendelee kuwaka, lazima uchochewe, lazima kuwepo na nishati na hewa ya oksijeni. Kadhalika kwenye hamasa, unaweza kuhamasika mara moja, lakini muda unavyokwenda hamasa hiyo inapungua.
Hivyo unapaswa kuchochea hamasa yako kila siku, unapaswa kujikumbusha kule unakoenda na jinsi maisha yako yatakuwa bora ukifika. Pia unapaswa kuwaangalia wale ambao wameweza kupiga hatua kubwa na kuhamasika kwamba inawezekana.
Kila hatua ndogo unayopiga na ukakamilisha, itumie hiyo kama hamasa kwako kupiga hatua zaidi. Kila ushindi mdogo unaupata, utumie kupata ushindi mkubwa zaidi.
Nne; FUNGUA UBUNIFU WAKO.
Kila mtu ni mbunifu, tunatofautiana tu kwa namna tunavyofungua na kutumia ubunifu ambao tayari upo ndani yetu. Watu wengi huwa hawatumii ubunifu wao, hivyo hufifia na kushindwa kufanya makubwa.
Kila siku fungua ubunifu wako zaidi, jiulize kipi cha tofauti unaweza kufanya, kipi bora zaidi unaweza kufanya, kipi kipya unaweza kujaribu. Usiwe mtu wa kufanya vitu vile vile kila siku kwa namna ile ile. Badala yake jaribu vitu vipya na utaibua ubunifu mkubwa ambao upo ndani yako.
Tano; TENGENEZA TABIA ZA USHINDI.
Hamasa inakuwezesha kuanza, tabia ndiyo inakufanya uendelee kwa muda mrefu. Mafanikio yoyote unayotaka kupata kwenye maisha yako, jua utahitaji muda, hakuna mafanikio ya haraka. Sasa kwa muda mrefu unaohitaji, kitu pekee kitakachokuwezesha kwenda kwa muda wote huo ni tabia.
Unahitaji kujijengea tabia za ushindi, tabia ambazo zitakuwezesha kila siku kupiga hatua kuelekea kwenye malengo yao. Angalia wale ambao wamefanikiwa wana tabia zipi kisha jijengee tabia hizo.
Tabia za msingi kabisa za mafanikio, kama nidhamu, uadilifu, kujituma, kujali muda, kujenga mahusiano bora, kujali fedha na uvumilivu na ung’ang’anizi, ni tabia ambazo unapaswa kujijengea ili kuweza kutengeneza mpenyo wa mafanikio makubwa kwenye maisha yako.
Rafiki yangu, hayo ndiyo mambo matano muhimu sana ya kufanya ili kuweza kutengeneza mpenyo wa mafanikio makubwa kwenye maisha yako. Yafanyie kazi kama bado hujaanza na kama utayafanya kwa usahihi na kwa msimamo, mafanikio makubwa kwako itakuwa swala la muda tu.
Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha
Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; https://amkamtanzania.com/jiunge