Rafiki yangu mpendwa, je unajua kwamba kila mtu yupo kwenye biashara na ili ufanikiwe kwenye chochote unachouza kuna njia kumi za kupata mpenyo ambao utakuwezesha kupiga hatua sana? Karibu usome makala ya leo, uondoke na mambo ya kwenda kufanyia kazi.

Zama tunazoishi sasa ni zama ambazo ajira rasmi zinapotea kabisa. Nafasi za kazi zimekuwa chache na siyo za uhakika kama kipindi cha nyuma. Hili linawasukuma watu wengi kuingia kwenye biashara zao wenyewe. Pamoja na watu wengi kuingia kwenye biashara, wengi pia wamekuwa wanashindwa kwa sababu hawana maarifa sahihi ya kufanikiwa kwenye biashara.

Hata wale ambao wanapata nafasi za kuajiriwa, bado changamoto kwenye ajira ni kubwa, huku vipato vikiwa vidogo na visivyotosheleza. Lakini wapo wachache ambao wameweza kutengeneza vipato vikubwa kwenye kazi walizoajiriwa, kwa kujua njia sahihi ya kupata mpenyo unaowawezesha kutoa thamani zaidi na hivyo kulipwa zaidi.

breakthrough1

Kwenye makala ya leo, tunakwenda kujifunza njia kumi za kupata mpenyo ambao utaiwezesha biashara au kazi yako kukua sana na hivyo kuweza kufikia mafanikio makubwa.

Kwenye kitabu cha mwandishi na mshauri bora wa biashara na masoko Jay Abraham, kinachoitwa GETTING EVERYTHING YOU CAN OUT OF ALL YO’VE GOT, ametushirikisha njia 21 za kujitofautisha kabisa na wale wanaofanya kile tunachofanya na hivyo kuweza kufanikiwa sana.

Moja ya vitu ambavyo ametufundisha kwenye kitabu hiki ni kupata mpenyo, ambao unarahisisha sana kile tunachofanya na kujitofautisha na wengine wote ambao wanafanya kile tunachofanya sisi pia (washindani). Iwe upo kwenye biashara au ajira, unaweza kupata mpenyo ambao utakuweka wewe mbele ya wengine wote na hivyo kuwa na nafasi kubwa ya kufanikiwa.

Mwandishi ametushirikisha njia mbalimbali za kupata mpenyo, kwenye makala hii nakwenda kukushirikisha zile 10 muhimu unazoweza kuanza kuzitumia hapo ulipo sasa na ukapata matokeo bora sana.

Kabla hatujaingia kwenye njia kumi za kupata mpenyo, Jay ameanza kitabu chake kwa kutuonesha njia TATU PEKEE za kukuza biashara yako.

NJIA TATU PEKEE ZA KUKUZA BIASHARA YAKO.

Jay anatuambia zipo njia tatu pekee za kukuza biashara yako;

Moja; kuongeza idadi ya wateja.

Hapa unaongeza idadi ya wateja kwenye biashara yako, kwa kuwafikia wateja wapya ambao kwa sasa hawaijui biashara yako na hivyo kuweza kuuza zaidi. Haijalishi biashara yako ni kubwa kiasi gani, kwa hakika kuna wateja hawaijui. Hivyo kila wakati kazana kuwafikia wateja wengi wapya.

Mbili; ongeza kiwango cha manunuzi kwa mteja.

Hapa unaongeza kiwango cha manunuzi ambacho mteja anafanya anapokuja kwenye biashara yako. Mteja anaweza kuja na uhitaji wa kitu kimoja, lakini ukaweza kumshawishi akanunua na vitu vingine vinavyoendana na kile alichotaka. Kwa bidhaa au huduma unazouza, zipo ambazo unaweza kuziuza pamoja na zikamsaidia mteja, huku zikikupa faida zaidi.

Tatu; ongeza idadi ambazo mteja anarudi kununua.

Hapa unaongeza idadi ambazo mteja anarudi kununua kwenye biashara yako. kama mteja anakuja kununua mara moja kwako basi unamshawishi arudi kununua zaidi na zaidi. Iko hivi, kwenye biashara, kama utamuuzia mteja mara moja halafu asirudi tena, basi umepoteza fedha. Ili unufaike unahitaji mteja kurudi kununua tena na tena.

Ukiweka nguvu zako kwenye maeneo hayo matatu, utaiwezesha biashara yako kukua sana.

Jay ametupa mfano huu rahisi wa kuelewa ukuaji mdogo kwenye maeneo hayo matatu unavyoleta matokeo makubwa kwenye mapato na faida kwa ujumla.

Chukua mfano una wateja 1000 ambao kiwango chao cha manunuzi ni tsh 100,000/= na wananunua mara mbili tu kwa mwaka.

Mapato yako kwa mwaka yatakuwa;

1,000 x Tsh 100,000/=  x 2 = Tsh 200,000,0000/=

Sasa fikiria umeongeza asilimia 10 tu kwenye kila eneo katika maeneo hayo matatu.

Hivyo wateja wanakuwa 1,100, kiwango cha manunuzi kinakuwa 110,000 na idadi ya manunuzi inakuwa 2.2 kwa mwaka.

Mapato mapya kwa mwaka yatakuwa;

1,100 x Tsh 110,000/= x 2.2 = Tsh 266,200,000/=

Jionee kwenyewe hapo, ongezeko la asilimia 10 kwenye maeneo hayo matatu, umezalisha ongezeko la asilimia 33.1 kwenye mapato ya jumla ya biashara yako.

Kadiri unavyoongeza namba na viwango kwenye maeneo hayo matatu, ndivyo biashara yako inavyoweza kukua zaidi.

Yaelewe vizuri maeneo hayo matatu muhimu ya biashara yako na yafanyie kazi ili kuweza kukuza biashara yako zaidi.

SOMA; Sababu Tano Kubwa Zinazozuia Biashara Nyingi Kukua Na Jinsi Ya Kuondoka Kwenye Mkwamo Wa Kibiashara.

NJIA KUMI ZA KUPATA MPENYO UTAKAOIWEZESHA BIASHARA YAKO KUKUA.

Mpenyo ni wazo jipya la kufanya kitu ambalo linaleta matokeo bora kuliko ambavyo ilikuwa ikifanywa awali. Watu wote ambao wamefanikiwa sana kuna kipindi walikuwa chini kabisa, kisha wakapata mpenyo na kuutumia vizuri.

Hapa tunakwenda kujifunza njia kumi za kupata mpenyo ambao utaweza kukusaidia sana wewe kufanikiwa kwenye kazi au biashara unayofanya. Jifunze hapa kisha uchukue hatua na hutabaki pale ulipo sasa.

  1. Kuna fursa zimejificha kila mahali.

Watu wengi hufikiri kwamba fursa ni kitu adimu sana ambacho kinapatikana kwa bahati na kwa watu wachache. Lakini hili siyo kweli, fursa zipo kila mahali, na hapo ulipo sasa, kwa kazi au biashara unayofanya, zipo fursa nyingi kwako kupiga hatua zaidi. Ili kuziona na kuweza kuzitumia fursa hizi lazima uwe na mtazamo wa kuzitafuta fursa kwenye kila unachofanya na ukishazipata kuchukua hatua mara moja bila ya kuchelewa. Wanaofanikiwa ni wale ambao wanakuwa wa kwanza kwenye fursa yoyote ile.

  1. Tafuta njia mpya ya kuingiza kipato kila miezi mitatu.

Kwa kile unachofanya, kila wakati tafuta njia mpya ya kuingiza kipato kila miezi mitatu. Watu wengi wamekuwa wanaendesha maisha yao kwa mazoea kwa kufanya kile ambacho wamekuwa wanafanya siku zote. Hawakuzi kipato chao siyo kwa sababu fursa hazipo, ila kwa sababu hawazitafuti na kuzifanyia kazi. Wewe jisukume kila miezi mitatu uje na njia mpya ya kuingiza kipato. Kumbuka, atafutaye hupata, asiyetafuta hapati.

  1. Jitofautishe na wengine.

Njia ya uhakika ya kupata mpenyo wa kibiashara au hata kwenye kazi ni kujitofautisha kabisa na wengine. Hakikisha kwamba kuna kitu ambacho watu wanakipata kwako, ambacho hawawezi kukipata sehemu nyingine yoyote ile. Kile unachofanya kiwe cha kipekee na chenye manufaa makubwa kwa wale wanaokutegemea na hapo utaweza kuwavutia wengi zaidi.

  1. Kazana kuwanufaisha wengine kabla hujajifikiria wewe.

Kinachowazuia watu wengi kufanikiwa ni ubinafsi uliopitiliza. Watu wamekuwa wanajifikiria wao wenyewe zaidi kuliko wanavyowafikiria watu wengine. Hivyo kwa kile mtu anachofanya, anajiuliza nanufaikaje kwanza mimi. Wewe usijiulize hivyo, bali uliza wengine wananufaikaje kupitia kile unachofanya. Ukiweka mbele maslahi ya wengine, utaweza kupata mpenyo wa kufanikiwa sana kwenye kile unachofanya.

  1. Tengeneza na kuza mtandao wako.

Ni kupitia mtandao wako ndipo unapojifunza na kupata mawazo ya tofauti, ambayo ukiyatumia utaweza kufanikiwa sana kwenye kile unachofanya. Unahitaji kuwa na mtandao mzuri wa wale ambao mnafanya kitu kimoja na kupitia mtandao huo utajifunza njia bora kabisa za kufanya unachofanya. Pia unahitaji kuwa na mtandao wa nje ya kile unachofanya, na hapo utaweza kujifunza vitu vinavyofanyika kwingine na jinsi ya kuvitumia kwenye kile unachofanya.

SOMA; Hii Ndiyo Kanuni Muhimu Ya Kutengeneza Mpenyo Wa Mafanikio Makubwa Kwenye Maisha Yako.

  1. Ondoa kabisa hatari kwa mteja.

Moja ya vitu vinavyowafanya wateja kusita kuchukua hatua ni kukosa uhakika wa kile wanachoshawishiwa kununua. Wateja wanakuwa na hofu kwamba wanaweza kupoteza fedha, kama watanunua kitu ambacho hakiwafai. Njia bora kwako kutumia ili kuwapa wateja uhakika ni kuondoa kabisa hatari kwao. Hapa unawapa uhakika kwamba iwapo walichonunua hakitawafaa, basi wataweza kupata kitu kingine au wakarejeshewa fedha walizolipa, bila ya usumbufu wowote. Kwa kuondoa hatari kwa mteja, unatengeneza mpenyo wa biashara yako kukua zaidi.

  1. Kuwa na njia mbadala za kupata mawazo bora.

Wazo moja bora linaweza kuwa na matokeo makubwa sana kwenye biashara yako. Lakini wafanyabiashara wengi wamekuwa hawapati mawazo bora kwa sababu wanajiwekea ukomo wa wapi pa kupata mawazo yao. Unapaswa kuwa na njia nyingi na mbadala za kupata mawazo bora ya kuiwezesha biashara yako kukua zaidi. Kwa kifupi, kila wakati na kwa kila unachofanya, jiulize ni kipi unajifunza unachoweza kutumia kwenye biashara yako. Mfano umeenda kwenye mgahawa kupata chakula, ukapata huduma nzuri au mbovu, ondoka hapo na somo la vitu gani vya kuzingatia au kuepuka kwenye biashara yako. Kila unachokutana nacho au kupitia kwenye biashara yako, hakikisha unaondoka na hatua za kwenda kuchukua kwenye biashara yako.

  1. Fikra za ukuaji.

Fikra za ukuaji na mpenyo ni vitu ambavyo vinakwenda kwa pamoja. Fikra za ukuaji zinachochea mpenyo na mpenyo unachochea fikra za ukuaji. Kwenye kitu chochote unachokua, usiridhike na pale ulipofika sasa, badala yake kila wakati jiulize unawezaje kukua zaidi. Fikiria ukuaji zaidi na hapo utaziona fursa za ukuaji, na kadiri unavyokua, ndivyo unavyohamasika kufikiria ukuaji zaidi.

  1. Tengeneza nyenzo.

Lengo lako kwenye kazi na hata biashara ni kupata matokeo makubwa zaidi ya kwa nguvu unazoweka. Huu ndiyo msingi wa nyenzo, kuweka nguvu kidogo na kupata matokeo makubwa. Kwenye kile unachofanya, unapaswa kutafuta nyenzo, kupitia rasilimali za wengine kama muda, fedha, utaalamu, uzoefu na kadhalika. Angalia ni jinsi gani unaweza kutumia rasilimali za wengine kwa wewe kupiga hatua zaidi.

  1. Tumia njia zilizofanikiwa kwenye maeneo mengine.

Upo usemi kwamba usijaribu kuvumbua tairi ya tofauti. Tairi ni tairi, hakuna cha tofauti unaweza kuvumbua kuhusu tairi. Watu wengi wamekuwa wanatumia muda mwingi kuja na kitu cha tofauti cha kufanya ili wafanikiwe. Wakati mara nyingi kitu bora kufanya ni kile ambacho kimeshafanikiwa kwa wengine. Kwa kila unachofanya, angalia wengine wanaofanya kitu kama hicho au tofauti na wamefanikiwa sana. Angalia ni kwa namna gani wanafanya, kisha wewe fanya kwa ubora zaidi na utafanikiwa.

Rafiki, unahitaji mpenyo wa kukutoa hapo ulipo sasa ili uweze kupiga hatua kubwa zaidi kwenye maisha yako. Tumia njia hizi kumi ulizojifunza hapa ili kuweza kutengeneza mpenyo utakaoiwezesha biashara au kazi yako kukua sana na wewe kufikia mafanikio makubwa.

Kwenye TANO ZA JUMA hili tunakwenda kujifunza njia 21 za kujitofautisha kabisa na wengine na kuweza kupata mafanikio makubwa kwenye kazi au biashara unayofanya. Usikose tano za juma hili, zitakupa misingi bora sana ya kufanikia kwenye kile unachofanya.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; https://amkamtanzania.com/jiunge