#TANO ZA JUMA #29 2019; Tatizo Hujui Unachotaka, Jinsi Ya Kupata Kila Unachotaka Kwa Kuanzia Hapo Ulipo Sasa, Njia Kumi Za Kupata Mpenyo Wa Mafanikio, Hatua Mbili Za Kuongeza Kipato Chako Na Kitu Kimoja Ambacho Watu Wanahitaji Sana.

Rafiki yangu mpendwa,

Karibu kwenye TANO ZA JUMA la 29 la mwaka huu 2019. Kwenye juma hili tunakwenda kujifunza jinsi ya kupata kila kitu unachotaka kwenye maisha yako kwa kuanzia pale ulipo sasa.

Tunakwenda kujifunza hili kwa kina kutoka kwenye kitabu kinachoitwa Getting Everything You Can Out of All You’ve Got: 21 Ways You Can Out-Think, Out-Perform, and Out-Earn the Competition ambacho kimeandikwa na kocha wa biashara Jay Abraham.

jay abraham 1

Kwenye kitabu hiki, Jay ametushirikisha njia 21 za kuweza kufikiri, kufanya na kutengeneza kipato zaidi kuliko wengine kupitia kazi au biashara tunazofanya.

Karibu tujifunze, tupate maarifa, mikakati na hamasa za kwenda kuchukua hatua ili tusibaki pale tulipo sasa.

#1 NENO LA JUMA; TATIZO HUJUI UNACHOTAKA.

Pata picha, unataka kuwa na safari, unaondoka nyumbani umebeba mizigo yako na kuelekea kituo cha mabasi. Unakaribishwa na kuulizwa unaenda wapi, unasema popote basi linapokwenda. Je unafikiri basi hilo litakupeleka wapi?

Unaweza kushangaa na kujiuliza inawezekanaje mtu mwenye akili timamu aende kituo cha basi kwa ajili ya safari halafu hajui anakokwenda!

Kabla hujaendelea kushangaa, hebu jiulize kwanza maswali haya muhimu; unakwenda wapi na maisha yako? unakwenda wapi na biashara unayofanya? Unakwenda wapi na kazi uliyonayo? Unakwenda wapi na mahusiano uliyonayo?

Kwa maneno mengine, miaka 5, 10, 20 na zaidi ijayo unajiona wapi? Kama huwezi kutoa jibu moja kwamba unajiona wapi katika vipindi hivyo, kwa hakika huna tofauti na anayeenda kwenye kituo cha mabasi huku akiwa hajui anakwenda wapi.

Na hivi ndivyo watu wengi wanavyoendesha maisha yao, wanakazana sana kufanya chochote wanachofanya, lakini hawajui wanakwenda wapi, hivyo wanafanya leo kama walivyofanya jana, huku kesho ikiwa haipo kwenye mawazo yao kabisa.

Kama mpaka sasa maisha yako huyaelewi, kama umeshajaribu kazi na biashara nyingi lakini bado huoni matokeo mazuri, tatizo lako ni moja, hujui nini hasa unachotaka, hujui wapi hata unakotaka kufika.

Na kama hutachukua hatua ya kwanza muhimu ya kujua kwanza nini unachotaka na wapi unapotaka kufika, hutaweza kuwa na maisha bora. Kila siku utaishia kuyumbishwa kama bendera inayopeperushwa na upepo. Watu watakuja kwako na kila aina ya fursa mpya na utahangaika nazo, na hakuna hata moja itakayokusaidia kufanikiwa.

Jua kwanza ni nini hasa unachotaka, jua ni wapi unakotaka kufika, kisha weka juhudi zako zote katika kufika kule unakotaka kufika. Kuwa kiziwi na kipofu kwa vitu vingine vyote visivyohusiana na kile unachotaka. Usiwe mtu wa kukimbizana na kila aina ya fursa mpya, badala yake weka nguvu kubwa kufika kule unakotaka kufika.

Kujua unachotaka na kuweza kukipata, anza kwa kujiuliza maswali haya muhimu sana;

  1. Mimi ni nani?
  2. Ni nini ninachotaka?
  3. Ni nini kinanipa furaha?
  4. Nini hakinipi furaha?
  5. Uimara wangu uko wapi?
  6. Udhaifu wangu uko wapi?
  7. Ni mchango gani mkubwa naweza kutoa kwa wengine kupitia maisha yangu, kazi yangu, biashara yangu na mahusiano yangu?

Ukijiuliza na kujipa majibu sahihi kwenye maswali hayo saba, na kufanyia kazi majibu hayo, utaweza kupata chochote unachotaka kwenye maisha yako.

#2 KITABU CHA JUMA; JINSI YA KUPATA KILA UNACHOTAKA KWA KUANZIA HAPO ULIPO SASA.

Kupitia kitabu cha juma hili, mwandishi ambaye pia ni mshauri na kocha wa biashara, hasa eneo la masoko, Jay Abraham ametushirikisha njia 21 za kuweza kufikiri, kufanya na kulipwa zaidi ya wengine wanaofanya kile tunachofanya.

Kwenye uchambuzi huu wa kitabu nakwenda kukushirikisha njia hizo 21 na hatua za kuchukua ili uweze kupiga hatua na kufanikiwa zaidi kupitia kile unachofanya.

MOJA; JUA UNAKOKWENDA.

Kama hujui unakokwenda, huwezi kufika na hata ukifika hutajua kama umefika. Hatua ya kwanza kuchukua ili kupata unachotaka ni kujua wapi unapokwenda.

Unapaswa kujua kwamba kila mtu kwenye maisha kuna kitu anauza, iwe upo kwenye biashara au ajira, hivyo jua ni nini unachouza na uweze kukiuza vizuri zaidi.

Zipo njia tatu za kukuwezesha kuuza zaidi, kupata wateja wapya, kuuza zaidi kwa wateja ulionao na kuwafanya wateja ulionao waje kununua mara nyingi zaidi.

Kama umeajiriwa, unauza muda wako, utaalamu wako na uzoefu wako kwa mwajiri wako. Na kitu kimoja ambacho kila mwajiri anapenda sana ni mtu ambaye anaweza kutatua matatizo na siyo anayesababisha matatizo.

Chochote unachochagua kufanya, hakikisha unakifanya kwa utofauti mkubwa na wengine wanavyokifanya. Usikubali kufanya kwa mazoea au kuiga kile ambacho wengine wanafanya.

Wape wateja wako urahisi wa kusema ndiyo kwa kile unachouza, kwa kutoa thamani kubwa sana ambayo hawawezi kuipata sehemu nyingine yoyote ile. Yaani unapaswa kutoa thamani kubwa kiasi kwamba mteja atajiona ni mjinga kujaribu kutafuta sehemu nyingine ya kununua.

MBILI; MATARAJIO MAKUBWA.

Watu wengi wamekuwa wanaendesha maisha yao kwa mtazamo kwamba mafanikio yanakuja kwa hatua ndogo ndogo. Huu ni ukomo ambao wengi wanajiwekea na unawazuia kukua zaidi. Unaweza kupiga hatua kubwa sana za mafanikio kwa kuanzia hapo ulipo sasa.

Njia pekee ya wewe kuweza kupiga hatua kubwa za mafanikio ni kuziona fursa ambazo wengi hawazifanyii kasi, kisha kufanyia kazi fursa hizo. Kwenye kila kazi au biashara, kuna vitu ambavyo watu wamezoea kufanya, na vimekuwa vinafanyika hivyo kwa muda mrefu. Lakini zipo fursa nyingi ambazo zipo wazi kabisa ila hazionekani na wengi, kwa sababu siyo kitu kilichozoeleka.

Ni wajibu wako kuangalia fursa ambazo zipo kwenye kile unachofanya, ambazo wengi hawazitumii na wewe ukaanza kuzitumia. Unapaswa kutengeneza mpenyo ambao utakuwezesha kupiga hatua kubwa na kufanikiwa. Unapaswa kuwa kiongozi, kwa kuchagua njia mpya ambayo haijazoeleka. Huwezi kupata mafanikio makubwa kwa kuwa mfuasi, kwa kufuata kile ambacho kila mtu anafanya.

TATU; JUA UIMARA NA UDHAIFU WAKO.

Kabla hujaanza safari yako ya mafanikio makubwa, unapaswa kujua uimara na udhaifu wako. Unahitaji kujifanyia tathmini wewe mwenyewe na kutumia vizuri majibu unayoyapata baada ya tathmini hiyo.

Watu wengi wamekuwa hawajifanyii tathmini hii muhimu sana kwao na hivyo wanaendesha maisha kwa mazoea, wasijue wapi pa kuweka nguvu zaidi na wapi pa kutegemea wengine.

Kwenye #MAKINIKIA ya juma hili tutajifunza maswali 50 ya kujiuliza na kujipa majibu yatakayokuwezesha kujua uimara na udhaifu wako, katika maisha binafsi na hata kwenye kazi au biashara.

NNE; MKAKATI WA MAFANIKIO.

Upo mkakati mkuu wa mafanikio ambao Jay amekuwa anaufundisha, anauita STRATEGY OF PREEMINENCE. Msingi mkuu wa mkakati huu ni kuweka mbele maslahi ya mteja kabla ya maslahi yako binafsi. Ukiweza kusimamia msingi huu, mafanikio makubwa lazima yaje kwako, siyo yanaweza kuja, bali lazima yatakuja.

Mkakati huu wa mafanikio una nguvu kubwa sana ya kuiwezesha biashara yako na hata kazi yako kupiga hatua kubwa na kufanikiwa.

Kwa kuanza, Jay anatuambia tutofautishe kati ya mteja na mtu tunayemhudumia.

Mteja (customer) ni mtu anayenunua bidhaa au huduma. Hivyo hakuna cha ziada hapo, mtu ananunua basi.

Mtu unayemhudumia (client) ni mtu ambaye anakuwa chini ya uangalizi wako. Mtu huyu anakuwa anakutegemea wewe kufanya maamuzi sahihi kwa ajili yake.

Hivyo kuanzia sasa acha kuwaita watu wateja na waite watu unaowahudumia. Na wahudumie kweli, kwa kuweka mbele maslahi yao, kutatua changamoto zao na kuhakikisha kila unachofanya kinaongeza thamani kubwa kwenye maisha yao.

Kuna kitu kimoja pekee unachopaswa kukipenda kwenye biashara yako, wale unaowahudumia. Watu wengi wamekuwa wanakosea kwa kupenda bidhaa au huduma zao, kupenda zaidi faida au vitu vingine. Unapaswa kuamini sana kwenye bidhaa na huduma unazotoa, lakini unapaswa kuwa na mapenzi ya dhati kabisa na wale unaowahudumia. Kwa sababu unapopenda mtu au kitu, basi unafanya maamuzi sahihi na kuweka maslahi ya mtu au kitu hicho mbele.

Wafanye wale unaowahudumia kuwa jukumu lako, chagua lile eneo la maisha yao ambalo unawahudumia kuwa jukumu lako na mara zote jiulize unawezaje kuyafanya maisha yao kuwa bora zaidi ya yalivyo sasa. Hili litakusukuma kutoa thamani zaidi kwa wateja wako, thamani ambayo itarudi kwako pia.

Furahia kila unapopata nafasi ya kukutana na wale unaowahudumia, na hata unapowasiliana nao, onesha kuwa na furaha na upendo wa hali ya juu, kitu ambacho kinatoka ndani yako kweli na watu hao watapenda kuendelea kuwa na wewe kwa muda mrefu.

Fanyia kazi mkakati huu na utaweza kupiga hatua kubwa na kufanikiwa zaidi.

TATO; PATA HASARA MWANZONI KUPATA FAIDA MBELENI.

Kikwazo kikubwa cha ukuaji wa biashara imekuwa kushindwa kumshawishi mteja kununua kwa mara ya kwanza. Hivyo hapa ndipo unapaswa kuweka nguvu zako kubwa.

Kwa sababu tayari una mkakati bora wa kutoa thamani kubwa kwa wateja wako, hawataweza kuona hilo mpaka pale watakaponunua kwako kwa mara ya kwanza.

Swali ni je utawezaje kumshawishi mteja kununua kwako kwa mara ya kwanza, mteja ambaye hajawahi kununua kabisa kwako?

Jibu ni kwa kuondoa vizingiti au vikwazo vyote ambavyo vinamzuia mteja kwa sasa. Kikwazo kikubwa kabisa kimekuwa ni hatari ambayo mteja anaona iko mbele yake, ya kupoteza fedha zake iwapo anachonunua hakitamfaa.

Hatua za kuchukua ni kuwa na mkakati wa kupata hasara mara ya kwanza mteja anaponunua kwako, lakini kwa kuwa utamhudumia vizuri na atarudi tena na tena, basi utaweza kutengeneza faida siku za mbeleni.

Hapa unaweza kutoa zawadi kwa mteja anaponunua kwa mara ya kwanza au kuwa na punguzo fulani. Vyote ni kumfanya achukue hatua ya kununua kwako kama kukujaribu, na akishanunua kwako mara moja, ataendelea kununua.

Zawadi au punguzo unalompa mwanzo linaondoa kabisa ile faida ambayo ungeweza kuipata, lakini anapokuja kununua tena, unatengeneza faida.

Chukua mfano unauza kitu ambacho bei yake ni elfu 10 na faida unayopata ni elfu 3. Mteja ananunua kitu hicho kila mwezi mara moja na unaweza kwenda naye kwa angalau miaka mitatu. Sasa unaweza kumpa mteja wako zawadi au punguzo la hiyo elfu tatu na hata zaidi anaponunua kwa mara ya kwanza. Lakini atakapoendelea kununua, utarudisha faida hiyo na zaidi.

Kabla ya kuchukua hatua hii unapaswa kukokotoa kiasi cha faida unachopata na muda ambao mteja atanunua ili uweze kupata matokeo mazuri.

SITA; KUWA NA KITU CHA KUKUTOFAUTISHA NA WENGINE.

Ili kufanikiwa kwenye biashara au chochote unachofanya, unapaswa kujitofautisha na wale wanaofanya kile unachofanya. Hivyo hapa unahitaji kutengeneza utofauti wako na kuwaeleza wateja nini wakija kwako wanapata ambacho hawawezi kupata sehemu nyingine yoyote ile.

Angalia jinsi washindani wako wanafanya mambo yao, kisha wewe kuwa na njia bora zaidi ya kufanya ambayo inawapa wateja thamani kubwa, kisha hakikisha wateja wanajua kuhusu utofauti wako. Njia zote za masoko unazotumia zinapaswa kueleza utofauti wako na wengine, ili wateja washawishike kuja kwako na siyo kwenda kwa wengine.

Baadhi ya maeneo ambayo unaweza kujitofautisha kwenye biashara ni bei, huduma, ubora, upekee, uharaka, uhakika na mengine.

Njia bora ya kujitofautisha ni kuchagua eneo dogo (niche) ambalo utalihudumia vizuri zaidi kuliko kuhangaika na eneo kubwa. Hapa unachagua aina fulani ya wateja, wenye sifa za kipekee ambao utaweza kuwahudumia vizuri na kuachana na wateja wengine wote. Kuachana na wateja wengine huwa ni kitu kigumu kwa wafanyabiashara wengi, lakini unapaswa kukumbuka kwamba huwezi kuwaridhisha watu wote.

Tengeneza ujumbe unaobeba utofauti wako kibiashara na kila unapokutana au kuwasiliana na wateja hakikisha unawapa ujumbe huo. Ujumbe huu unapaswa kurudiwa rudiwa mara nyingi mpaka watu wauelewe na kuihusisha biashara yako na ule utofauti unaotengeneza. Yaani pale mteja anapotaka kitu cha tofauti na kinachomfaa yeye, basi anajua atakipata kwako.

SABA; ONDOA KABISA HATARI KWA MTEJA.

Tumeona kikwazo cha wateja kununua kwa mara ya kwanza kwako ni hatari ya kupoteza fedha zao iwapo kitu walichonunua hakitawafaa kama walivyotaka. Tumejifunza njia moja ya kuwapa ofa au zawadi ambayo itawasukuma kununua.

Ipo njia nyingine yenye nguvu zaidi, ambayo ukiitumia lazima mteja anunue. Njia hiyo ni kuondoa kabisa hatari kwa mteja. Yaani hapa unaondoa nafasi yoyote ile ya mteja kupoteza fedha zake, na unakwenda mbele zaidi kwa kumlipa kwa muda au chochote alichopoteza.

Jay anaiita mbinu hii BETTER-THAN-RISK-FREE GUARANTEE (BTRF). Biashara nyingi huwa zinamrudishia mtu fedha aliyonunulia kitu kama hakijamfaa, au kumpa kitu kingine. Sasa wewe unahitaji kwenda zaidi ya hapo, unahitaji kumrejeshea mteja kile alicholipa, lakini pia kumlipa fidia kwa muda aliopoteza au usumbufu uliomsababishia.

Kwa kuwa tayari kumlipa fidia mteja wako pale ambapo hajaridhishwa na ulichomuuzia inaonesha unamjali sana na pia una uhakika sana na kile unachouza. Kadiri mteja anavyopata uhakika wa aina hii, ndivyo anavyokuwa tayari zaidi kununua kile unachouza.

Kama kweli unajali kuhusu wateja wako na kama kweli unaamini kwenye kile unachouza na umechagua kuwazia wateja sahihi, unaweza kutumia mbinu hii na hutapata hasara yoyote. Kwa sababu kwanza utawahudumia wateja sahihi na watakuwa tayari kwenda na wewe kwa muda mrefu.

NANE; UZA VITU VYA NYONGEZA.

Mteja anapokuja kwako na kukubali kununua kitu kimoja, una fursa kubwa ya kumuuzia vitu vingine vinavyoendana na kile ambacho mteja amenunua.

Hivyo tumia fursa hiyo kuuza zaidi, pale mteja anaponunua kitu kimoja, mwoneshe vitu vingine vinavyoendana na kile alichonunua na mshawishi kununua. Kumbuka maslahi ya mteja ndiyo unayaweka mbele, hivyo unampa vitu vya ziada ambavyo unajua vitamsaidia sana.

Kwa kila bidhaa au huduma unayouza, kuwa na vitu vingine vinavyoendana nayo na mteja anaponunua kitu kimoja, mwonyeshe vitu vingine vinavyoendana na hicho alichonunua.

Njia nyingine unayoweza kutumia kumuuzia mteja zaidi ni kuuza vitu kwa pamoja. Mfano mteja akinunua kitu kimoja basi anapata kimoja, lakini akinunua vitu viwili, anapata kimoja bure. Wengi husukumwa kununua viwili ili kupata hicho cha bure.

Pia unaweza kuweka ofa ya muda mfupi ambayo mteja akichukua hatua anaifaidi, lakini akichelewa anaipoteza.

TISA; PIMA KILA KITU.

Kila hatua unayochukua kwenye biashara yako, unapaswa kuipima, la sivyo hutaweza kujua kama inaleta matokeo sahihi au la. Usiendeshe biashara yako kwa kubahatisha, badala yake iendeshe kwa kupima kila unachofanya na kisha kufanya maamuzi sahihi kutokana na matokeo unayoyapata baada ya kupima.

Kwenye biashara, mara nyingi unachotaka wewe siyo ambacho soko linataka, unachopenda wewe siyo ambacho soko linapenda. Hivyo acha kujifikiria wewe na angalia soko linapenda nini kisha lipe.

Kama unaendesha matangazo, pima matangazo hayo kwa kutumia njia mbalimbali kama kutumia vichwa vya habari tofauti, kutumia vyombo vya habari tofauti, kutoa ofa tofauti, kutumia bei tofauti na hata kutoa ofa tofauti. Kisha pima matokeo unayopata kwa kila njia unayotumia na ile inayoleta matokeo mazuri ndiyo inakuwa njia kuu.

Kila unachofanya kwenye biashara yako, unapaswa kukipima na kujua matokeo yake. Na hata baada ya kupata matokeo bora kabisa na kuchagua njia kuu, bado unapaswa kuendelea kupima kadiri unavyokwenda ili uweze kujua matokeo unayopata na kama kuna njia bora zaidi basi itumike hiyo.

Unapokuwa unapima, unapaswa kuanza kwa hatua ndogo na ukishapata matokeo basi unakwenda kwenye hatua kubwa. Kwa mfano kama unajaribu tangazo, anza kwa kuwafikia watu wachache kisha ukishaona njia bora ndiyo unapeleka tangazo hilo kwa watu wengi zaidi.

KUMI; TUMIA WATEJA WA BIASHARA NYINGINE.

Kila biashara ina wateja ambao haiwatumii, hawa ni wateja ambao wamekusanywa na biashara ila kwa muda mrefu hawajanunua. Lakini pia zipo biashara ambazo zina wateja wengi na hazihusiani kabisa na biashara yako, yaani siyo washindani wako. Hapo unaweza kutumia wateja wa biashara nyingine kuwatangazia biashara yako.

Unachofanya hapa ni kutumia biashara nyingine ambazo siyo shindani na kuomba kutangaza biashara yako kupitia orodha ya wateja walionao. Iwe ni kwa mawasiliano ya email, namba za simu au barua.

Hapa unaingia makubaliano na biashara hiyo kwa kulipa kamisheni kutokana na wale wateja watakaonunua bidhaa yako. Biashara nyingi zitakupa nafasi ya kutangaza biashara yako kwenye orodha yake kama siyo biashara shindani na kama bidhaa au huduma unayotoa ni ya uhakika kwa wateja.

Angalia biashara zote kubwa na zenye wateja wengi na omba kutumia wateja wake kutangaza biashara yako, wewe utanufaika kwa kupata wateja zaidi, kwa sababu kumbuka hawatanunua mara moja pekee. Na biashara inayokuruhusu utangaze kwa wateja wake itanufaika kwa kamisheni inayopata.

KUMI NA MOJA; TENGENEZA MPANGO WA RUFAA.

Hakuna tangazo lenye nguvu kwenye biashara yako kama rufaa ambayo mteja wako anampa mtu mwingine. Watu huwa wanawaamini sana watu wao wa karibu. Hivyo mtu anaposikia kuhusu biashara yako kutoka kwa mtu wa karibu yake, anaamini zaidi kuliko anaposikia matangazo yako.

Hapa kuna fursa kubwa sana ya kukuza biashara yako na kuwafikia wateja wengi zaidi ambayo wafanyabiashara wengi wamekuwa hawaitumii. Wengi wamekuwa wanawaambia wateja wawaletee wateja zaidi, lakini hawana mpango wowote wa kuwasaidia wateja kufanya hivyo.

Unapaswa kutengeneza mpango wa rufaa kwenye biashara yako, mpango ambao unawawezesha wateja wako kukupa wateja wengi zaidi.

Mpango huu unaanza kwa kuainisha sifa za wateja unaowalenga, kisha unapomhudumia mteja na akaridhika, unamwomba akupe watu ambao wana sifa za wateja unaowalenga. Wakishakupa majina na mawasiliano ya watu hao, unawaomba wawaambie kuhusu wewe lakini na wewe pia unawatafuta na kuwaambia wamekaribishwa na mtu wao wa karibu ambaye amenufaika sana na biashara yako.

Ili kuwapa wateja hamasa ya kukupa wateja zaidi unapaswa kuweka motisha kama wa zawadi au ofa mbalimbali ambazo mteja atapata kwa kuleta wateja wengine zaidi.

Kumbuka mkakati mkuu ni maslahi ya mteja mbele, hivyo kama mteja wako amenufaika na kile unachofanya, ni wajibu wako kuhakikisha na watu wake wa karibu pia wananufaika. Hivyo unapomwomba akupe wateja zaidi, siyo kwa manufaa yako tu, bali kwa manufaa yake na watu wa karibu pia.

KUMI NA MBILI; RUDISHA WATEJA WALIOPOTEA.

Kila biashara huwa inapoteza wateja, sasa kwa kuwa wafanyabiashara wengi hawapimi, huwa hawajui kiasi cha wateja wanaopotea. Lakini kama utachukua idadi ya wateja mwanzo wa mwaka na kuja kulinganisha na wateja wa mwisho wa mwaka, utagundua kuna wateja wengi wamepotelea katikati. Hapa kuna fursa kubwa sana kwako kukuza biashara yako, kama utaweza kuwarudisha wateja waliopotea kwenye biashara yako.

Zipo sababu tatu zinazowafanya wateja waache kununua kwako, moja, maisha yao yamebadilika, mbili, wamekwazika kwenye biashara yako, tatu, hawahitaji tena bidhaa au huduma unayouza.

Pitia biashara yako na jua wateja wote ambao walikuwa wananunua zamani ila kwa sasa hawanunui tena. Tengeneza mfumo wa kufanya nao mawasiliano, kwanza kujua kwa nini wameacha kununua na pili kuwakaribisha kununua au kukuletea wateja zaidi.

Kama sababu ya kuacha kununua ni maisha kubadilika, angalia jinsi gani unaweza kuwahudumia kwa hali yao ya sasa. Kama ni kwa sababu walikwazika kwenye biashara yako, rekebisha kilichotokea. Na kama sababu ya kuacha kununua ni hawahitaji tena bidhaa au huduma zako, basi waombe wakupe watu wengine ambao wanaweza kunufaika na biashara yako kama wao walivyonufaika nayo.

Kwa vyovyote vile, kuwasiliana na wateja ambao wameacha kununua utajifunza njia bora za kuendesha biashara yako lakini pia utaweza kwarudisha wale waliopotea.

KUMI NA TATU; TUMIA MAANDISHI KUWAFIKIA WATEJA WENGI ZAIDI.

Zipo njia mbalimbali za masoko ambazo zinakuwezesha kuwafikia wateja wengi. Unaweza kutumia matangazo ya vyombo vya habari, lakini haya ni gharama kubwa. Unaweza kutumia watu wa masoko kuwatembelea wateja, lakini hawa hawawezi kufika kwa watu wengi kwa muda mmoja.

Ipo njia moja ambayo ni gharama rahisi na inawafikia wengi kwa wakati mmoja. Njia hiyo ni maandishi. Kwa kuandika barua au barua pepe na kutuma kwa wateja wako tarajiwa, unawafikia wengi kwa gharama kidogo.

Njia ya kutuma barua ilikuwa inafanya kazi vizuri siku za nyuma, ila kwa sasa imekosa nguvu. Njia ya barua pepe ina nguvu kubwa na gharama kidogo. Pia zipo njia nyingine kama kutumia mtandao wa intaneti na mitandao ya kijamii.

Kikubwa ni kujua jinsi ya kutumia maandishi kuweza kuwashawishi watu kuja kununua kile unachouza. Na hapa unapaswa kuwa na kichwa cha habari ambacho kinamvutia mtu kusoma, ufunguzi ambao unamnasa mtu aendelee kusoma, maelezo ambayo yanaeleweka vizuri na mwisho ambao unampa mteja hatua za kuchukua mara moja.

Jifunze uandishi wa kibiashara kwa kusoma matangazo na barua za mauzo za makampuni makubwa, kisha jifunze kuandika kwa ushawishi mkubwa.

KUMI NA NNE; NUNUA WATEJA.

Njia nyingine ya kupata wateja wapya kwenye biashara yako ni kununua wateja kwa wale ambao wanauza orodha za wateja. Wapo watu ambao wana orodha kubwa ya wateja kulingana na sifa mbalimbali. Unachofanya ni kwenda kwao na kuwaambia sifa za wateja unaotaka kuwafikia, kisha wanakupatia watu hao na unalipia kutumia orodha hiyo.

Unaweza pia kununua wateja kupitia matangazo ya mitandao ya kijamii, ambapo unachagua sifa za watu ambao unataka kuwafikia, kisha unalipia na tangazo lako linaoneshwa kwa wale unaowalenga.

Zipo njia mbalimbali za kununua wateja ambazo zitakusaidia kuuza zaidi.

Upande wa pili ni wewe kutengeneza orodha ya wateja ambao unaweza kuwauza kwa watu wengine wenye uhitaji. Kila unapowahudumia wateja, kusanya taarifa zao na tengeneza orodha yako ya wateja. Utaweza kuitumia wewe mwenyewe na hata kuwakodishia wengine nao waitumie kuuza bidhaa zao.

KUMI NA TANO; TUMIA SIMU KUUZA.

Simu yako ni nguvu kubwa sana ya kukuwezesha kuwafikia wateja wengi na kuwauzia pia. Itumie simu yako kama kifaa cha masoko na mauzo kwa kuwasiliana na wateja wako kabla na baada ya kununua.

Kila mteja anayefika kwenye biashara yako au anayejibu kutokana na matangazo yanayotolewa na biashara, taarifa zake zinapaswa kuhifadhiwa. Hifadhi namba zao za simu na tengeneza mpango wa kuwa unawapigia simu wateja wako.

Kwa wale ambao hawajanunua wapigie kuwaeleza manufaa ya kile unachouza na kuwashawishi kuja kununua. Kwa ambao wameshanunua wapigie kujua wanaendeleaje na kile walichonunua kimewafaaje.

Kwa kutumia simu yako vizuri utaweza kuwafikia wateja wengi na kuuza zaidi.

Njia bora ya kuandaa mpango huu wa simu ni kurusha matangazo ambayo yanawataka wateja wako kupiga simu, kutuma ujumbe au kuja kwenye biashara yako. Na mteja akishakutafuta, basi tunza mawasiliano yake, hasa simu na hapo utaendelea kuyatumia kwa masoko na mauzo zaidi.

KUMI NA SITA; TUMIA MTANDAO WA INTANETI VIZURI.

Mtandao wa intaneti una nguvu kubwa ya kuweza kuwafikia wateja wengi zaidi. Watu wengi wamekuwa wanachukulia mtandao wa intaneti kama sehemu ya kutoa maarifa na taarifa pekee, lakini pia unaweza kutumika kupata wateja zaidi wa biashara yako.

Katika kutumia mtandao wa intaneti kupata wateja zaidi unapaswa kuwa na vitu viwili;

Moja unapaswa kuwa na tovuti ya biashara yako, hii inaeleza kila kitu kuhusu biashara yako. Hapa ndipo nyumbani kwa biashara yako mtandaoni. Watu wanaweza kuingia na kupata taarifa muda wowote ule, masaa 24 kila siku. Unaweza pia kuuza bidhaa zako moja kwa moja kwenye tovuti ya biashara yako.

Mbili unapaswa kuwa na blogu ya biashara yako. Blogu hii unaitumia kutoa taarifa na maarifa yanayohusiana na biashara yako. Unaweza kuitumia blogu kutoa elimu kwa wateja wako kuhusu biashara yako, hivyo watu wanapokuwa na shida na kutafuta suluhisho, wanaletwa kwenye blogu ya biashara yako. Kwa kupata ushauri wako mzuri, wanakuamini na kuwa tayari kununua kile unachouza.

Tumia vitu hivyo viwili ili biashara yako iweze kunufaika na mtandao wa intaneti.

KUMI NA SABA; BADILISHANA MALI KWA MALI.

Kabla ya kuja kwa matumizi ya fedha, watu walikuwa wanabadilishana mali kwa mali. Kama wewe ni mfugaji na unahitaji nafaka, basi ulitoa mbuzi ili kupata mahindi. Ujio wa fedha umeondoa ile dhana ya kubadilishana mali kwa mali.

Lakini bado unaweza kuitumia kwenye biashara yako, hasa pale unapohitaji kukua zaidi lakini huna fedha. Unachoangalia ni nini unachoweza kutoa ili kupata kile unachohitaji. Kwa mfano kama unafanya biashara ya kuuza magari, na unataka kupata matangazo kwenye vyombo vua habari. Unaweza kuwapa watu wa vyombo vya habari punguzo kwenye magari na wao wakakupa muda wa matangazo bila ya kulipa fedha.

Kila biashara ina kitu inachoweza kutoa kwa wengine na ikaokoa matumizi ya fedha. Na pale ambapo unahitaji kitu kutoka kwa mwingine, lakini yeye hawezi kunufaika na unachotoa, basi unaweza kutafuta mtu wa tatu, ambaye utampa kile ulichonacho wewe na anakihitaji, na yeye atampa yule unayemlenga kile anachohitaji, halafu unayemlenga anakupa unachohitaji wewe.

Kama kuna vitu unahitaji kwenye biashara yako na huna fedha, angalia wale unaotaka wakupe na ona ni mali gani unaweza kuwapa na wao wakakupa kile unachotaka.

KUMI NA NANE; BORESHA MAWASILIANO NA WATEJA WAKO.

Wazungu wana usemi usemao; out of site, out of mind, yaani kile ambacho hukioni basi hukifikirii. Hii ndiyo inatokea kwa biashara nyingi. Kuna wateja wameacha kununua kwako siyo kwa sababu yoyote mbaya ambayo umefanya, bali kwa sababu amekusahau, wametingwa na maisha yao na wewe hujawakumbusha.

Hivyo tengeneza utaratibu wa kuwasiliana na wateja wako mara kwa mara na kwa njia mbalimbali. Unaweza kuwapigia simu, kuwatumia ujumbe mfupi wa simu, kuwatumia barua pepe, kuwatumia kadi za salamu au pongezi mbalimbali.

Kadiri unavyowasiliana na wateja wako, na siyo tu kwenye kuwatangazia, bali kuwapa salamu na kuwatakia heri, ndivyo wanavyokufikiria zaidi na kuwa tayari kununua kwako zaidi.

KUMI NA TISA; UNAPASWA KUWA NA MALENGO.

Watu wengi wanaoendesha biashara hawana malengo yoyote makubwa wanayoyafanyia kazi. Hivyo wanajikuta wakiendesha biashara zao kwa mazoea. Na hili ndiyo linasababisha biashara nyingi kudumaa na kufa.

Kuepuka hili, weka malengo makubwa ya biashara yako, kisha yagawe kwenye hatua ndogo ndogo za kuchukua. Usijiwekee malengo madogo na unayoyafikia kirahisi, bali jiwekee malengo makubwa na yanayokusukuma sana.

Ukishakuwa na malengo makubwa, kila hatua unayochukua hakikisha inakusogeza karibu zaidi na malengo hayo.

ISHIRINI; MAFANIKIO YASIYO NA UKOMO.

Mafanikio kidogo huwa ni kikwazo cha mafanikio makubwa. Watu wengi wanapojiwekea malengo na wakayafikia, wanaridhika na kuona wameshafika kilele cha mafanikio. Hapo ndipo wengi huanza kuanguka.

Kama unataka mafanikio yasiyo na ukomo, unapaswa kuweka malengo mapya makubwa pale unapofikia malengo makubwa uliyojiwekea awali. Usifike wakati ukajiona kwamba umeshafika kileleni. Kila wakati jichukulie kama ndiyo unaanza, jitume zaidi na utazidi kupata mafanikio makubwa.

Wale wanaoona wameshafanikiwa na hawahitaji kujisumbua tena ndiyo wanaoanguka baada ya kufanikiwa.

ISHIRINI NA MOJA; UNA UTAJIRI MKUBWA KULIKO UNAVYOFIKIRI.

Maisha yana uwezo wa kukupa chochote unachotaka, swali ni wewe unataka nini. Watu wengi wamekuwa wanajizuia kufanikiwa zaidi kwa kutaka vitu vidogo ambavyo ni chini kabisa ya uwezo wao.

Pima mafanikio yako kwa kulinganisha uwezo wako na matokeo unayopata sasa. Mara nyingi unapofanikiwa kidogo watu wa nje watakuambia umeshafika kileleni, lakini ndani yako utajua kama bado hujatumia uwezo wako wote.

Ukweli ni kwamba kila mtu ana uwezo mkubwa kuliko anaotumia sasa, hivyo usikubali kujiwekea ukomo wowote. Kumbuka una utajiri mkubwa kuliko unavyofikiri, ni wewe kuutambua na kuutumia.

Hizi ndizo njia 21 za kukuwezesha wewe kufikiri, kuchukua hatua na kutengeneza kipato kikubwa kuliko wale ambao wanafanya kile unachofanya. Fanyia kazi hatua hizi kwenye kazi yako, biashara yako na maisha kwa ujumla na hutabaki hapo ulipo sasa.

#3 MAKALA YA JUMA; NJIA KUMI ZA KUPATA MPENYO WA MAFANIKIO.

Kuna watu huwa tunawaona wanafanya vitu vya kawaida kabisa kama ambavyo watu wote wamezoea kufanya. Lakini siku moja wanapata matokeo makubwa kuliko wanavyofanya na hapo tunafikiria labda wamepata bahati.

Lakini pia wapo watu ambao wanaonekana kuwa na bahati kuliko wengine, kwa sababu kila wanachogusa kinaleta matokeo mazuri.

Ukweli ni kwamba, hakuna watu wachache ambao wana bahati na wengine wasio na bahati. Bahati iko sawa kwa wote, ila kuna wanaoweza kuzitumia bahati zinazokuja kwao na wengine hawajui hata kama bahati zinakuja upande wao.

Kuna njia mbalimbali za kutengeneza bahati kwenye maisha yako, njia ambazo zinaleta mpenyo kwenye kile unachofanya, iwe ni kazi au biashara. Wale wanaotumia njia hizi na kupata mpenyo wanaonekana kuwa watu wenye bahati sana. Habari njema ni kwamba hata wewe unaweza kutengeneza mpenyo kwenye maisha yako.

Kwenye makala ya juma hili tumejifunza njia kumi za kutengeneza mpenyo wa kibiashara ambao utaweza kukufikisha kwenye mafanikio makubwa. Njia hizi pia unaweza kuzitumia kutengeneza mpenyo kwenye maeneo mengine ya maisha yako.

Kama hukupata nafasi ya kusoma makala hii ya juma, hakikisha unaisoma sasa hivi. Fungua hapa kuisoma; Njia Kumi (10) Za Kupata Mpenyo Ambao Utaiwezesha Biashara Yako Kukua Na Kufikia Mafanikio Makubwa.

Kwenye makala hiyo pia tunajifunza njia tatu pekee za kuikuza zaidi biashara yako na kuongeza kipato chako. Ukiweza kufanyia kazi njia hizo tatu, biashara unayofanya au unayotaka kufanya itafanikiwa sana. Fungua usome ili uweze kujifunza na kupiga hatua.

#4 TUONGEE PESA; HATUA MBILI ZA KUONGEZA KIPATO CHAKO.

Rafiki yangu mpendwa, moja ya vitu ambavyo nimekuwa nakusisitizia sana wewe rafiki yangu ni kuwa na vyanzo mbadala vya kukuingizia kipato. Hii ndiyo njia pekee kwako kuweza kupata uhuru kamili wa maisha yako.

Kama kipato chako kinategemea mtu mmoja au wachache basi haupo huru, utalazimika kufanya kile ambacho anayedhibiti kipato chako anakutaka ufanye, hata kama hutaki kukifanya au unaona siyo sahihi kufanya.

Mfano unapokuwa umeajiriwa na chanzo pekee cha kipato chako ni mshahara unaopata kwenye ajira hiyo, unajikuta unakuwa chini ya mwajiri wako, kufanya chochote anachotaka hata kama kwa upande wako siyo kitu sahihi au muhimu kufanya.

Hivyo ili kupata uhuru kamili, ili kupata mafanikio makubwa kwenye maisha yako, unapaswa kuwa na vyanzo tofauti, kipato chako kusitegemee mtu mmoja au watu wachache.

Zipo njia nyingi sana za kuongeza njia za kuingiza kipato na hatimaye kuongeza kipato chako. Lakini njia zote hizi tunaweza kuzigawa kwenye hatua mbili, ambayo inarahisisha sana uchukuaji hatua wa mtu katika kuongeza kipato.

Hatua ya kwanza; ongeza thamani zaidi pale ulipo sasa.

Hatua ya kwanza ya kuongeza kipato chako ni kuongeza thamani zaidi pale ulipo sasa. Hapa huhitaji kuanza kufanya kitu kipya, bali unaendelea kufanya kile unachofanya sasa, lakini kwa viwango vya juu zaidi ambavyo vinakuwezesha kutengeneza kipato zaidi.

Kama una biashara hapa unakazana kuwahudumia vizuri zaidi wateja ambao tayari unao, kuongeza wateja wapya na kuwapa vitu vipya ambavyo wateja wanahitaji lakini kwako havipatikani.

Kama upo kwenye ajira ni kuongeza thamani unayotoa kwenye ajira hiyo, kwa kuchukua majukumu mengi na makubwa, kufanya kazi kwa muda mrefu zaidi na kufanya kazi yako kwa viwango vya juu zaidi. Japokuwa kwenye ajira kuna ukomo, bado ni sehemu ya kuanzia ili kuondoka kwenye utumwa huo.

Hatua hii ni muhimu sana kwa kila mtu kuitumia kwa sababu haihitaji uwe na rasilimali za ziada. Mfano watu wengi wamekuwa wanasema wangekuwa na fedha wangeanzisha au kukuza zaidi biashara walizonazo. Kwa kuwa hawapati fedha wanazotaka, basi wanabaki vile walivyo. Kama kila mtu angefanyia kazi hatua hii ya kwanza na kufanya zaidi pale alipo sasa, wangeweza kutengeneza kipato zaidi na kwenda kufanya kile hasa wanachotaka kufanya.

Hatua ya pili; fanya kitu cha tofauti.

Hatua ya pili kwenye kuongeza kipato chako ni kufanya kitu cha tofauti na unachofanya sasa. Hapa ndipo unakwenda kuanza biashara mpya kama huna biashara au kuanza biashara ya tofauti na ile unayofanya sasa au kwenye eneo tofauti na unalofanyia biashara sasa.

Hii ni hatua muhimu na unayopaswa kuichukua kwa umakini, kwa sababu inahitaji maamuzi unayokwenda kuyasimamia kwa muda mrefu. Wengi wamekuwa wanachukua hatua hii bila ya kujitathmini vizuri na kujikuta wametengeneza gereza zaidi kwa kile kipya wanachokwenda kufanya.

Mfano mtu anakwenda kuanzisha biashara mpya wakati biashara anayofanya sasa bado hajaweza kuiendesha vizuri, kinachotokea ni biashara zote mbili kufa. Au mtu anatoka kwenye ajira moja na kwenda kwenye ajira nyingine, kitu ambacho hakibadilishi sana hali yake ya maisha.

Kama unataka kuongeza kipato chako, anzia hapo ulipo sasa na chagua kitu cha kufanya zaidi. Kama ni biashara fikiria wateja wapya unaoweza kuafikia, huduma na bidhaa mpya unazoweza kuwapatia na ubora wa huduma unazotoa. Kama ni kwenye ajira angalia majukumu makubwa zaidi unayoweza kufanyia kazi, muda zaidi unaoweza kuweka kwenye kazi zako na thamani kubwa zaidi unayoweza kuzalisha. Ukishaweka juhudi kubwa kwenye kile unachofanya sasa, ndipo sasa unaweza kufanya kitu cha tofauti.

Kila mtu ana fursa nyingi za kufanya zaidi kwenye kile anachofanya sasa, hebu anza kutumia fursa hizi ili kuongeza kipato chako zaidi.

#5 TAFAKARI YA KUFIKIRISHA; KITU KIMOJA AMBACHO WATU WANAHITAJI SANA.

“People are silently begging to be led.” ― Jay Abraham

Jay Abraham anatupa siri kubwa sana kuhusu kitu ambacho watu wanakihitaji sana; KUONGOZWA.

Rafiki, hili linaweza kukushangaza na kukufanya ujisikie vibaya, lakini ukweli ni kwamba watu wanapenda kuongozwa. Watu hawapendi kuchukua jukumu la kuongoza, bali huwa wanaangalia nani anaongoza na kumfuata yeye.

Mahali popote, kuanzia kwenye familia, kwenye biashara, kwenye kazi na jamii kwa ujumla, watu hawapendi kuwa mbele na kuongoza, wengi wanapenda kuwa wafuasi na kufuata anayeongoza.

Watu hawapendi kuongoza kwa sababu uongozi unamtaka mtu kufanya maamuzi magumu na mazito, ambayo yanaweza yasiwafurahishe wengi, lakini inabidi yafanyike. Watu hawapendi kuongoza kwa sababu hawapendi lawama. Watu hawapendi kuongoza kwa sababu hawapendi kupingwa na kukosolewa.

Lakini pia, wale ambao wanaongozwa huwa hawafikii mafanikio makubwa. Siku zote viongozi ndiyo wanaofikia mafanikio makubwa, kwa sababu ndiyo wanaoamua nini wanataka na kufanyia kazi ili kupata wanachotaka.

Hivyo rafiki yangu, kama unataka kuwa na mafanikio makubwa kwenye maisha yako, chagua kuwa kiongozi. Chagua kile unachoamini na kukisimamia, na utashangaa watu wengi watakufuata, hata kama hujawaomba wakufuate. Kadiri unavyokuwa na maono makubwa na kuyasimamia, ndivyo utakavyovuta wafuasi wengi zaidi.

Kwenye maisha yako, kazi na hata biashara, chagua kuwa kiongozi, acha kufuata wengine wanachofanya na tengeneza maono makubwa ya kile unachotaka na yasimamie. Utawavutia wengi watakaopenda kwenda pamoja na wewe na utaweza kufanikiwa sana.

Watu wanapenda kuongozwa, simama kama kiongozi na wafuasi watakufuata.

Rafiki, hizi ndizo TANO ZA JUMA hili la 29, ambazo zimekupa msingi sahihi wa kujua unachotaka na jinsi ya kukipata kwa kuanzia pale ulipo sasa. Fanyia kazi haya uliyojifunza kwa kuanzia hapo ulipo sasa, kwa kazi au biashara unayofanya na utaona matokeo ya tofauti sana na uliyozoea kupata.

Kwenye #MAKINIKIA ya juma hili tutakwenda kujifunza MASWALI 50 YA KUJIULIZA NA KUJIPA MAJIBU ili kujua uimara na udhaifu wako, kwenye biashara, kazi na maisha binafsi. Kwa kujiuliza na kujijibu maswali hayo utaweza kuona hatua sahihi kwako kuchukua ili kuweza kufanikiwa zaidi.

Kupata #MAKINIKIA haya jiunge na CHANNEL YA TANO ZA JUMA ambayo ipo kwenye mtandao wa telegram. Maelekezo ya kujiunga na channel hii yapo hapo chini.

#PATA KITABU NA UCHAMBUZI ZAIDI.

Rafiki yangu mpenda, kama ungependa kupata kitabu tulichochambua kwenye makala hii ya tano za juma, pamoja na kupata uchambuzi wa mafunzo zaidi kutoka kwenye kitabu hiki, karibu ujiunge na channel ya TANO ZA MAJUMA 52 YA MWAKA.

Hii ni channel ambayo ipo kwenye mtandao wa TELEGRAM MESSENGER, ambapo kila juma nakutumia kitabu cha juma, uchambuzi huu na mafunzo ya ziada yote kwa mfumo wa pdf ambapo utaweza kusoma na hata kuhifadhi vizuri kwa matumizi ya baadaye. Pia kwa kujiunga na channel hii, utaweza kupata mafunzo yote ya nyuma na hata ukipoteza mafunzo hayo utaweza kuyapakua tena muda wowote unapoyataka.

Ada ya kujiunga na channel hii ni ndogo mno, ni shilingi elfu moja tu kwa wiki. Au unaweza kuchagua kulipa kwa mwezi (elfu 3) au kwa mwaka (elfu 30). Lakini wiki ya kwanza ni bure na hulipi chochote. Karibu ujiunge leo bure kwa kutuma ujumbe kwa njia ya telegram kwenda namba 0717396253. Ujumbe uwe na maneno TANO ZA MAJUMA YA MWAKA.

Makala hii imeandikwa na Kocha Dr Makirita Amani.

Dr. Makirita ni Daktari wa binadamu, Kocha wa mafanikio, Mwandishi na Mjasiriamali.

Dr. Makirita anaendesha mafunzo ya mafanikio kwa wale waliojitoa hasa kufanikiwa kupitia program ya KISIMA CHA MAARIFA.

Kama bado hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA, tuma sasa ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa njia ya wasap namba 0717 396 253 (tumia wasap tu)

Kupata huduma nyingine za ukocha tembelea www.amkamtanzania.com/kocha

Kupata vitabu vizuri vya kusoma tembelea www.amkamtanzania.com/vitabu