Rafiki yangu mpendwa,

Kufanikiwa kwenye ujasiriamali imekuwa ni kitu kigumu kwa walio wengi.

Watu wengi sana wamekuwa wanafikiria na kupanga kuingia kwenye ujasiriamali, lakini ni wachache wanaochukua hatua na kuingia kwenye ujasiriamali.

Katika wachache ambao wanaingia, wengi wao wamekuwa wanaishia kushindwa kwenye ujasiriamali. Ni wachache sana ambao wanakuja kufanikiwa kwenye ujasiriamali.

Kushindwa huku kwa wengi na kufanikiwa kwa wachache kumefanya ujasiriamali uonekane ni kitu kigumu na kinachowafaa wachache waliochaguliwa. Wengi wamekuwa wanapata hofu wanapotaka kuingia kwenye ujasiriamali na kuona kwamba wengi walioingia wameshindwa.

UJASIRIAMALI+PICHA

Lakini unapoangalia kwa undani, unagundua moja ya vitu vinavyochochea ujasiriamali kuwa mgumu kwa wengi, ni uongo ambao watu wamepewa kuhusu ujasiriamali. Mambo mengi ambayo watu wanajua na kuamini kuhusu ujasiriamali siyo sahihi, na hivyo yamekuwa kikwazo kwao kufanikiwa.

Kwenye makala ya leo tunakwenda kupata ukweli kuhusu ujasiriamali, tunakwenda kujifunza mambo matano ambayo kila anayetaka kufanikiwa kupitia ujasiriamali na biashara anapaswa kuyajua na kuchukua hatua.

Karibu ujifunze mambo haya matano ya kweli kuhusu ujasiriamali na uweze kuyaweka kwenye maisha yako ili uweze kufanikiwa kwenye ujasiriamali na biashara kwa ujumla.

  1. Ujasiriamali ni asili yetu binadamu.

Watu wamekuwa wanaamini kwamba kuna watu ambao wamezaliwa kuwa wajasiriamali na wengine wamezaliwa kuwa waajiriwa pekee. Imani hii imewafanya wengi kukubali kushindwa kwenye ujasiriamali, wakiamini siyo asili yao. Huu ni uongo.

Ujasiriamali ni asili yetu sisi binadamu, kila mtu ana ujasiriamali ndani yake. Ukiangalia historia ya maisha ya wanadamu hapa duniani, kwa kipindi kirefu tumekuwa tunaendesha maisha yetu kupitia ujasiriamali.

Mfumo huu wa kuingiza kipato kupitia kuajiriwa hauna hata miaka 200 mpaka kufikia sasa, lakini binadamu tumekuwepo hapa duniani kwa miaka mingi mno.

Waliotutangulia waliweza kuishi na sisi tukapatikana kwa sababu walijihusisha na shughuli za kijasiriamali ili kupata kile wanachotaka, kwa sehemu kubwa chakula, mavazi, malazi na usalama.

Wapo waliookota matunda, wapo waliochimba mizizi, wapo waliowinda, wapo waliolima, wapo waliofua vyuma na shughuli nyingine za aina hiyo ambazo kwa miaka mingi zimekuwa ndiyo msingi wa jamii zetu.

Mfumo rasmi wa ajira ambao umekuwepo hapa duniani siyo kwa miaka mingi sana kwa sasa unaanguka, hivyo unatulazimisha kila mtu kurudi kwenye asili yetu ambayo ni ujasiriamali.

Ukweli unaopaswa kuondoka nao hapa ni kwamba ujasiriamali ni asili ya kila binadamu na wewe una sifa zote za kufanikiwa kwenye ujasiriamali, ni kuchukua hatua tu.

SOMA; Njia Kumi (10) Za Kupata Mpenyo Ambao Utaiwezesha Biashara Yako Kukua Na Kufikia Mafanikio Makubwa.

  1. Ujasiriamali ndiyo njia yenye hatari ndogo kwenye kipato.

Uongo mwingine ambao umetengenezwa na kuaminiwa na wengi kwenye ujasiriamali ni kwamba ujasiriamali ni hatari sana kwenye kipato. Kwamba huna uhakika wa kipato na hilo linakuwa hatari, hasa pale unapokuwa na uhitaji wa fedha na usiweze kuzipata haraka.

Wengi wameaminishwa kwamba ajira ndiyo njia a uhakika na yenye hatari ndogo kwenye upande wa kipato. Kwamba kila mwezi mtu ana uhakika wa kupokea mshahara wake na hivyo ni kitu unachoweza kukitegemea.

Huu ni uongo ambao umekuwa kikwazo kwa wengi kufanikiwa kwenye ujasiriamali. Ukweli ni kwamba, kuingiza kipato kwa kutumia ajira ndiyo njia yenye hatari kubwa sana hasa kama ndiyo unayoitegemea pekee. Iwapo lolote litatokea na wewe kusimamishwa au kukosa ajira, basi unakuwa kwenye wakati mgumu kifedha.

Lakini kwenye ujasiriamali, ukishaijua misingi yake na kuchukua hatua sahihi, hatari inapungua sana. Kwa mfano kama una biashara ambayo ina wateja 100, haiwezekani wateja wote 100 wakaamua siku moja kwamba hawatanunua tena kwako. Wanaweza kupungua wachache, labda 10, lakini bado utabaki na wengine 90. Wakati kwenye ajira, mwajiri wako akisema hakutaki tena kipato chako kinakauka kwa asilimia 100.

Ukweli wa kuondoka nao hapa ni ujasiriamali ni njia salama ya kutengeneza kipato kuliko ajira. Muhimu ni kuijua misingi sahihi ya kufanikiwa kwenye ujasiriamali na kuiishi hiyo.

  1. Hakuna njia ya mkato ya mafanikio kwenye ujasiriamali.

Watu wengi wamekuwa wanaingia kwenye ujasiriamali kwa mtazamo kwamba ni njia ya mkato na ya haraka ya kupate fedha. Ndiyo maana watu wamekuwa wanatumia muda mwingi kukimbizana na fursa mpya na wasipate mafanikio.

Watu wamedanganywa sana kuhusu fursa mbalimbali kwamba zitawatoa haraka kwenye umasikini. Watu wamepewa hesabu za kwenye karatasi, zikawahamasisha, wakaingia kichwa kichwa na kupata hasara kubwa sana.

Ukweli ni kwamba ujasiriamali siyo njia ya kufanikiwa haraka na pia hakuna njia ya mkato ya mafanikio kwenye ujasiriamali. Ujasiriamali unahitaji kazi, unahitaji muda na unahitaji uvumilivu. Utashindwa sana kabla hujafanikiwa. Kama unaingia kwenye ujasiriamali kwa sababu unaamini utafanikiwa haraka bila ya kuweka kazi, umeshashindwa kabla hata hujaanza.

Ukweli wa kuondoka nao hapa ni huu, ujasiriamali siyo njia ya mkato ya kufanikia na hakuna njia ya mkato ya kufanikiwa kwenye ujasiriamali. Unahitaji muda, kazi na uvumilivu ili kufanikiwa kwenye ujasiriamali.

  1. Unapaswa kwenda sehemu yenye mkusanyiko kidogo.

Kosa kubwa ambalo watu wamekuwa wanalifanya kwenye ujasiriamali ni kuiga wengine. Pale mtu anapoona wengine wanafanya biashara ya aina fulani, anajiambia hiyo inalipa na hivyo anaifanya pia. Hapa mtu anajipeleka kwenye ushindani ambao unamuumiza sana.

Ili kufanikiwa kwenye ujasiriamali, unapaswa kwenda sehemu yenye mkusanyiko mdogo, kwa kufanya kile ambacho hakuna wengine wanaokifanya. Au kama kuna wanaofanya, basi wewe unafanya kwa utofauti.

Utafanikiwa kwenye ujasiriamali kama utakuwa na kitu cha tofauti, ambacho wateja wako hawawezi kukipata sehemu nyingine isipokuwa kwako tu.

Ukweli wa kuondoka nao hapa ni huu, ili kufanikiwa kwenye ujasiriamali, kuwa na kitu kinachokutofautisha na wengine, kitu ambacho wateja wanakipata kwako tu.

SOMA; Hatua Nane Za Kutengeneza Biashara Inayokupa Uhuru Mkubwa Na Unayoweza Kuiuza.

  1. Kufanikiwa kwenye biashara moja haimaanishi unajua biashara zote.

Mafanikio kidogo kwenye ujasiriamali kwa wengi imekuwa kikwazo kwa mafanikio makubwa zaidi. Mtu anaanzisha biashara moja, inafanikiwa na kufanya vizuri na hapo ndipo kushindwa kunapoanza. Anaamini kwa vile amefanikiwa kwenye biashara moja, basi anaweza kufanikiwa kwenye kila aina ya biashara. Hivyo mtu anaanza kujihusisha na biashara nyingine nyingi na tofauti, kwa kuamini uzoefu wake kwenye biashara moja utamsaidia kwenye biashara nyingine.

Hili limekuwa linapelekea wengi kushindwa sana na kuharibu mafanikio yao ya mwanzo.

Unapaswa kujua kwamba kufanikiwa kwenye aina moja ya biashara haimaanishi unaweza kufanikiwa kwenye kila biashara. Biashara zinatofautiana, biashara zina changamoto tofauti. Kama umefanikiwa kwenye biashara ya aina fulani, ni vyema kuendelea kuweka nguvu zako kwenye biashara hiyo na utaweza kufanikiwa zaidi. Na kama unataka kuingia kwenye biashara ya aina nyingine, ingia ukijua unakwenda kuanzia chini na kujifunza zaidi.

Mafanikio unayopata kwenye biashara moja yasikupe kiburi cha kuona unaweza kila aina ya biashara. Weka nguvu zako kwenye kile unachoweza kufanya vizuri na achana na vitu vingine vyote.

Ukweli wa kutoka nao hapa ni huu, kufanikiwa kwenye biashara moja haimaanishi unajua kila aina ya biashara. Weka nguvu zako kwenye kile unachojua na kama unataka kuingia kwenye biashara tofauti, basi ingia ukijua unakwenda kuanza upya.

Rafiki, mambo hayo matano kuhusu ujasiriamali ni mambo ambayo wengi wamekuwa wanadanganywa na kujidanganya na kufanya safari ya ujasiriamali kuwa ngumu zaidi. Jua ukweli huu na uishi kwenye ujasiriamali na kwa hakika utaweza kuiga hatua sana kupitia ujasiriamali.

Rafiki, kama ungependa kuendelea kupokea makala na mafunzo mengine mazuri kwenye email yako, fungua hapa na ujaze fomu; http://eepurl.com/dDZHvL

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

WhatsApp Image 2019-07-13 at 19.06.36