Rafiki yangu mpendwa, juma namba 46 kwa mwaka huu 2018 ndiyo linaagana na sisi. Ni juma ambalo lilikuwa bora sana kwetu na imani yangu ni kwamba umeweza kufanya makubwa sana kwenye juma hili.

Hata kama hujayaona matokeo makubwa, wewe usijali, endelea kufanya makubwa, matokeo yanajikusanya na siku moja yataanza kuanguka kama mvua na watu watasema una bahati kweli.

Rafiki, najua umeshawahi kuchemsha maji, huweki maji kwenye moto na hapo hapo yakaanza kuchemka. Badala yake unachochea moto kwa muda, maji yanapata joto kidogo kidogo, unaendelea kuchochea, inafika hatua kwamba kwa kuweka moto kidogo tu, maji yote yanachemka. Sasa haimaanishi kwamba ule moto wa mwisho ndiyo umechemsha maji yale, bali tangu moto wa mwanzo, ulikuwa unachangia maji kuja kuchemka baadaye.

Hivi ndivyo unavyopaswa kuyaendea mafanikio yako, usitegemee matokeo ya hapo kwa hapo, kwamba umeweka juhudi kubwa na unapata matokeo makubwa hapo hapo. Mara nyingi sana utaweka juhudi kubwa lakini matokeo hutayaona, ila kuna siku utaweka juhudi kubwa, na matokeo yatakuwa makubwa kuliko juhudi uliyoweka, unakuwa umefikia hatua ya kuvuna matokeo ya juhudi zilizopita.

Rafiki, hii pia ina maana kwamba kama unaweka juhudi kubwa halafu hupati matokeo, hupaswi kukata tamaa, kwa sababu ukikata tamaa unapoteza juhudi zote za mwanzo ulizoweka.

KURASA ZA MAISHA YA MAFANIKIO

Nikukaribishe kwenye tano za juma hili la 46 mwaka 2018 twende tukajifunze pamoja, uyatafakari haya unayojifunza na jinsi ya kuyatumia kwenye maisha yako, kisha uyaweke kwenye matendo na uweze kupiga hatua sana kwenye maisha yako.

Karibu kwenye tano za juma;

#1 KITABU NILICHOSOMA; SHERIA KUMI ZA JUU ZA MAFANIKIO KIBIASHARA.

Watu wengi wamekuwa wanachukulia biashara kama muujiza ambao haueleweki, wapo wanaoendesha biashara kama bahati nasibu, kama pata potea. Wengine wanaendesha biashara kama siri nzito ambayo haipaswi kujulikana na wengine kabisa. Wengine wanatumia biashara kama kitu cha kuweza kuwatawala wengine, kuwatumikisha na kupata kile wanachotaka wao bila ya kujali wengine wanapata nini.

Hivi sivyo Jack Stack mkurugenzi wa kampuni ya Springfield Remanufacturing Corp (SRC) anavyoichukulia biashara. Jack, ambaye ni mwandishi wa kitabu bora kabisa cha njia bora ya kuendesha biashara kwa mafanikio, kinachoitwa THE GREAT GAME OF BUSINESS (GGOM) ametushirikisha njia sahihi za kuiendesha biashara kwa mafanikio makubwa sana, bila ya kufuata njia zilizozoeleka za kuendesha biashara.

Jack anaanza kwa kusema biashara siyo sayansi na wala siyo sanaa, badala yake biashara ni mchezo wa ushindani, ambao una sheria zake, una washindi, una washindwa na pia ipo njia ya kupima ushindi huo. Pia anakumbusha kwamba katika mafanikio ya biashara bahati na kipaji pia vinahusika.

Jack anasema ukichukua kundi la watu na kuwaweka pamoja, hawawezi kukubaliana wote kwenye kitu kimoja, kila mtu atakuwa na maoni yake na mambo anayopendelea. Lakini anasema kuna kitu kimoja ambacho kinawaleta watu pamoja, kitu hicho ni ushindi.

Hivyo anasema kama biashara itaendeshwa kama mchezo, na watu wakapewa njia za kushinda mchezo huo, watajitoa sana ili kuweza kushinda mchezo huo.

Jack amekuja na njia mpya ya kuendesha biashara na kampuni kwa ujumla, njia ambayo wamekuwa wanaitumia wao kuendesha kampuni yao kwa zaidi ya miaka 30 sasa na imekuwa na mafanikio makubwa sana.

Njia hii mpya ni ya kuendesha biashara kwa uwazi kabisa, kwa kila aliye kwenye biashara, hasa waajiriwa kujua kila kitu kinachoendelea kwenye biashara. Kujua kiasi cha mtaji, mauzo, gharama za uendeshaji na hata faida. Makampuni mengi yamekuwa yanafanya taarifa hizi kuwa siri, lakini Jack anasema usiri unapelekea makampuni mengi kufa.

Jack anasema kama taarifa zikiwa wazi, na watu wakijua kampuni hasa iko wapi, watachukua hatua sahihi. Jack anasema tabia ya binadamu ni moja, wasipopewa taarifa, huwa wanatengeneza taarifa zao wenyewe. Hivyo kampuni yoyote yeye usiri, wafanyakazi huwa wanakuwa na tetesi zao wenyewe, na hakuna kitu kibaya kwenye ufanisi wa kampuni kama tetesi.

Kwa mfano kama biashara haiendi vizuri, na kampuni haipati faida, kwa sababu wafanyakazi hawajawekwa wazi, watafikiri kwamba wakurugenzi wao wananufaika huku wafanyakazi wanateseka. Lakini kama hesabu za biashara zitakuwa wazi kabisa, na kila mtu anaona kwamba hakuna faida, imani inaengeka na watu wanajituma zaidi.

Pia Jack anapinga kitendo cha wafanyakazi kwenye biashara kufanywa kama watoto, ambao wanapewa maelekezo ya kufanya kile ambacho wameajiriwa kufanya tu, na hakuna kufanya cha ziada au kuchangia mawazo yao. Jack anasema kama wafanyakazi wakipewa jukumu la kuzalisha matokeo fulani na wakapewa sababu ya matokeo hayo kuwa bora, basi watajituma sana kuleta matokeo bora, kuliko wakiambiwa kwamba kazi yako wewe ni kufanya hiki pekee.

THE GREAT GAME OF BUSINESS ni kitabu ambacho kila mtu ambaye yupo kwenye biashara na anataka kuikuza zaidi biashara yake, hasa kuajiri na kutengeneza timu inayojituma na kufanya makubwa, anapaswa kukisoma.

Kitabu kina vitu vingi muhimu sana kwa ukuaji wa biashara, na pia kina maelekezo ya jinsi ya kutumia vitu hivyo katika ukuaji wa biashara.

Hapa nitakushirikisha vitu viwili muhimu;

MOJA; SHERIA KUMI ZA JUU ZA MAFANIKIO YA BIASHARA.

  1. UNAPATA UNACHOTOA.

Kile unachowapa wafanyakazi wako kwenye biashara, ndicho wanachokurudishia wewe. Hivyo kama unataka kupiga hatua zaidi kwenye biashara yako, unapaswa kuanza kwa kuwajali wafanyakazi waliopo kwenye biashara yako. Wanapojisikia kuwa sehemu ya biashara, wanajituma zaidi na kutoa zaidi.

  1. NI RAHISI KUMZUIA MTU MMOJA, NI VIGUMU KUWAZUIA WATU 100.

Hapa ndipo ulipo umuhimu wa timu, mtu mmoja huwezi kufanya kila kitu, ukiwa kwenye biashara peke yako, huwezi kushindana na walio wengi. Hivyo njia ya uhakika ya kufanikiwa kwenye biashara, ni kuwa na timu ya watu wanaofanya kazi pamoja.

  1. UNACHOWAFANYIA WENGINE, NDIYO UTAKACHOFANYIWA PIA.

Katika kuimarisha timu ya biashara, ni muhimu sana kuwatendea wengine vizuri. Kunyanyasa wengine kwa sababu tu wewe upo juu yao, hakutakuacha salama, kutarudi na kukuumiza wewe pia. Hivyo mara zote watendee wengine vizuri, hasa wale waliopo chini yako.

  1. UNAFANYA KILE UNACHOPASWA KUFANYA.

Ile kauli kwamba nimefanya kadiri ya uwezo wangu haina nafasi kwenye mafanikio ya biashara. Mafanikio hayaji kwa kufanya kile kilicho ndani ya uwezo wako, bali kwa kufanya kile unachopaswa kufanya. Mambo yatakuwa magumu lakini unapaswa kupambana kwa kufanya kilicho sahihi ili kufika unakotaka kufika.

  1. LAZIMA ITOKE NDANI YA MTU.

Katika kupambana na magumu ili kufanikiwa kwenye biashara, msukumo unapaswa kutoka ndani ya mtu mwenyewe na siyo nje. Hivyo lazima uwe na timu ya watu ambao tayari wana msukumo wa ndani wa kupiga hatua zaidi. Kama watu hawana msukumo wa ndani, hakuna msukumo wa nje unaoweza kuwasaidia.

  1. UNAWEZA KUWADANGANYA MASHABIKI, LAKINI HUWEZI KUWADANGANYA WACHEZAJI.

Biashara ni mchezo, wafanyakazi ndiyo wachezaji wenyewe, watu wa nje ni mashabiki tu. Unaweza kuwadanganya mashabiki kuhusu mwenendo wa biashara, kwa kuigiza kwamba mambo yanakwenda vizuri, lakini wale walio ndani wanajua kama mambo yanaenda vizuri au la. Huwezi kuwadanganya waliopo ndani, kwa sababu hata kama unaweka siri, kuna vitu wataona havipo sawa.

  1. UNAPONYENYUA CHINI, JUU KUNANYENYUKA PIA.

Kikwazo kikubwa cha ukuaji wa biashara ni faida halisi ya biashara. Biashara inaweza kuwa na mapato makubwa, ikawa na mali nyingi, lakini faida inayobaki baada ya kuondoa gharama zote inakuwa kidogo sana au haipo kabisa. bila ya faida, biashara haiwezi kukua. Hivyo katika kukuza biashara, anzia kwenye faida halisi, baada ya kuondoa gharama zote za kuendesha biashara. Ukiweza kukuza faida, na biashara pia itakua zaidi.

  1. WATU WAKIWEKA MALENGO YAO WENYEWE, WANAYAFIKIA.

Ni rahisi kwa uongozi kuwawekea wafanyakazi malengo ambayo wanapaswa kuyafanyia kazi, lakini wengi huwa hawayafikii. Lakini pale watu wanapowezeshwa kujiwekea malengo yao wenyewe, wanayafanyia kazi na kuyafikia, kwa sababu ni kitu chao wenyewe, hakuna anayewalazimisha.

  1. KAMA HAKUNA ANAYEFUATILIA, WATU WANAACHA KUJALI.

Baada ya kuweka malengo ambayo watu wanayafanyia kazi, kama hakuna mtu anayewafuatilia kwa karibu, watu wanaacha kujali na kurudi kwenye mazoea yao. Hivyo lazima uwepo mfumo wa kuwafuatilia watu katika utekelezaji wa malengo waliyojiwekea.

  1. MABADILIKO YANAANZIA JUU.

Mabadiliko ya kweli kwenye jambo na eneo lolote, huwa yanaanzia juu, yanaanzia kwenye uongozi na kisha yanasambaa kwa wengine. Kama uongozi unataka watu wabadilike, lakini wenyewe haubadiliki, inakuwa vigumu sana mabadiliko kutokea. Lakini mabadiliko yanapoanzia juu, chini nako kunabadilika.

SHERIA KUU YA MWISHO YA MAFANIKIO KWENYE BIASHARA;

Pale unapoweza kuwashawishi watu kwa uwezo wa juu wa kufikiri, unapata utendaji wa hali ya juu sana.

MBILI; MAMBO MATANO YA KUZINGATIA KWENYE MCHEZO WA BIASHARA.

Kitu cha pili ninachokwenda kukushirikisha ni mambo matano muhimu sana ya kuzingatia katika kuucheza mchezo wa biashara ili kuweza kufanikiwa kwenye biashara.

MOJA; TENGENEZA VIWANGO.

Kitu cha kwanza kufanya kwenye mchezo wa biashara ni kutengeneza viwango vya hali ya juu sana ambavyo kila aliyepo kwenye biashara anavifuata. Viwango hivi vinakuja baada ya kuwepo kwa uwazi kwenye biashara.

Kila aliyepo kwenye biashara anapaswa kujua kila kinachoendelea kwenye biashara hiyo. Hesabu zote za biashara zinapaswa kuwa wazi, na watu wanapaswa kufundishwa jinsi ya kusoma hesabu hizo za biashara.

Hivyo vinapowekwa viwango, mtu anajua nini anafanyia kazi na kinahusianaje na kuboresha namba za biashara.

MBILI; LIPA BONASI NA SIYO ONGEZEKO LA MSHAHARA.

Moja ya njia kuu za kutengeneza faida kwenye biashara ni kuwa na gharama ndogo za kuendesha biashara. Na moja ya vitu vinavyoongeza biashara ni mishahara. Katika kuendesha biashara kama mchezo, Jack anasema usiwaongeze wafanyakazi mshahara, badala yake wape bonasi.

Bonasi hii unaitoa baada ya faida kuwa imepatikana, kile kiasi kinachozidi kwenye asilimia ya faida, kinaenda moja kwa moja kama bonasi kwa wafanyakazi. Kwa kufanya hivi, unawapa wafanyakazi moyo wa kujituma zaidi ili kupata bonasi.

Na ili wafanyakazi waamini kwenye bonasi unayowapa, lazima hesabu za biashara ziwe wazi na kila mtu aweze kuzisoma. Pia wanapojua ni nini wanapaswa kufanya ili kufikia bonasi yao, wanajituma zaidi.

TATU; TENGENEZA MPANGO WA MCHEZO.

Lazima kuwepo na mpango wa mwaka mzima wa kufanyia kazi kabla mwaka wa biashara haujaanza. Mpango huo lazima uzingatie maeneo yote muhimu ya biashara, kuanzia mtaji, mauzo, gharama za uendeshaji, na hata uzalishaji. Huu ni mpango ambao unagawanywa kwa kila idara na kila mtu anajua nini anapaswa kufanyia kazi ili kuufikia. Mpango huu wa mwaka mzima pia unajumuisha bonasi itakayolipwa kulingana na ongezeko la faida litakalopatikana.

NNE; MAWASILIANO NI MUHIMU.

Mawasiliano ni muhimu sana kwenye uendeshaji na ukuaji wa biashara. Lazima watu wajue nini kinaendelea kwenye biashara, hatua ambazo zimefikiwa kwenye mpango wa mwaka na mategemeo yao kwa jinsi mambo yanavyoenda. Kuweka tu mipango na kutokufuatilia nini kinaendelea, kunashusha hamasa ya watu na kujikuta wanarudi kwenye mazoea.

Pia watu wasipopewa taarifa, huwa wanatengeneza taarifa zao wenyewe, na siyo taarifa nzuri.

TANO; WAPE WATU UMILIKI KWENYE KAMPUNI.

Njia bora kabisa ya kupata ushirikiano wa wafanyakazi kwenye biashara yako, ni kuwapa sehemu ya umiliki wa biashara hiyo. Unapaswa kuwa na mpango wa kuwapa hisa wafanyakazi wako na kuwafanya wazithamini hisa zao. Kwa njia hiyo, watafanya kazi kwenye biashara siyo kwa sababu tu wanalipwa, ila kwa sababu wanajua kadiri biashara unavyokuwa, ndivyo pia uwekezaji wao unakua.

Na kama mawasiliano ni mazuri, hesabu zipo wazi na watu wanajua kila kinachoendelea, wataamini na kuweka imani zaidi kwenye biashara hiyo.

Rafiki, hivyo ndivyo unavyoweza kuucheza mchezo wa biashara kwa mafanikio makubwa sana, yafanyie kazi kwenye biashara yako na pata muda wa kusoma kitabu hichi.

Pia kwa wale wenye biashara zinazokua, ambao wangependa huduma ya kutumia mfumo huu wa THE GRATE GAME OF BUSINESS kwenye kuzikuza zaidi, naweza kuwasaidia kwenye hilo, tuwasiliane kwa wasap namba 0717396253 ili tupange jinsi ya kufanyia kazi hili. Kwa wale waliopo kwenye LEVEL UP, huduma hii wataipata moja kwa moja.

#2 MAKALA YA WIKI; KANUNI YA MPENYO WA MAFANIKIO.

Kuna watu ambao huwa wanakutana na mafanikio makubwa kwenye maisha yao, kwa nje watu wanaona wamebahatika, ila kwa ndani watu hao walikuwa na kanuni wanayoifuata ili kupata mafanikio hayo.

Juma hili nilikushirikisha makala yenye kanuni ya jinsi ya kutengeneza mpenyo wa mafanikio kwenye maisha yako. Ndani yake nimekushirikisha hatua tano muhimu za kufuata ili kutengeneza mpenyo wa mafanikio, kama hukusoma makala hiyo basi isome hapa; Hii Ndiyo Kanuni Muhimu Ya Kutengeneza Mpenyo Wa Mafanikio Makubwa Kwenye Maisha Yako.

Pia nimeanzisha kipengele kipya cha makala za DAKIKA MOJA, hizi ni makala ambazo nazituma moja kwa moja kwenye email yako kila siku kabla ya saa 12 asubuhi, ikiwa na somo la kukupa hamasa na nguvu ya kufanya makubwa kwenye siku yako.

Kama hujaanza kupokea makala hizi, tafadhali jiandikishe kwenye mfumo wetu wa email hapa; www.amkamtanzania.com/jiunge

Pia kama unapata shida kupokea email zinazotumwa, nyingine unapata na nyingine hupati, ingia kwenye email yako kwenye eneo la SPAM na utazikuta email huko. Na kama hazitakuwa huko, nenda eneo la SEARCH kisha andika DAKIKA MOJA au maarifa@kisimachamaarifa.co.tz kisha tafuta na email utaziona.

Kama utaona email zilikuwa kwenye spam, bonyeza sehemu imeandikwa NOT SPAM. Pia ili kupokea email hizi moja kwa moja bila shida, nenda sehemu ya ADD TO CONTACT na weka email hii; maarifa@kisimachamaarifa.co.tz kwa njia hii email utazipata bila ya shida.

#3 TUONGEE PESA; PESA IPO KILA MAHALI.

Mpaka zama hizi, licha ya kuwepo kwa maarifa mengi na siri zote za mafanikio kuwekwa wazi, bado wapo watu wanaoamini kwamba kuna kazi au biashara zinazolipa kuliko nyingine.

Rafiki, kwenye kila kazi au kwenye kila biashara kuna watu wanaotengeneza fedha nyingi na wapo watu ambao hawatengenezi fedha kabisa.

Hivyo tunaweza kusema PESA IPO KILA MAHALI, kinachowatofautisha wale wanaopata fedha na wale wanaokosa, siyo kile wanachofanya, bali namna wanavyofanya kile wanachofanya.

Kwenye kitabu cha THE SCIENCE OF GETTING RICH, mwandishi anasema ipo namna ya kufanya vitu, ambayo wale wanaotengeneza utajiri wanaitumia na wale wasiokuwa na utajiri hawaitumii.

Namna hiyo ya ufanyaji wa mambo inaanzia kwenye fikra ambazo mtu anazo. Fedha zipo kila mahali, ila zinavutwa au kukimbizwa na fikra ambazo mtu anazo. Kama mtu anakuwa na fikra za kitajiri, fikra zinazovutia fedha, fikra hizi zitakaribisha fedha. Lakini kama mtu anakuwa na fikra za kimasikini, fikra zinazofukuza fedha, mtu anaishia kuwa masikini.

Anza sasa kutengeneza fikra za kitajiri, na utaweza kuzivuta fedha ambazo zimezagaa kila mahali.

#4 HUDUMA NINAZOTOA; HUDUMA YA KUWA KOCHA WAKO BINAFSI.

Rafiki, kuweka mipango mikubwa kwenye maisha yako siyo kitu kigumu kufanya, wengi wanaweka mipango hiyo. Tatizo linakuja kwenye utekelezaji. Watu wengi sana huwa wanashindwa kutekeleza yale waliyopanga.

Na sababu kuu ni ugumu wa kufanya yale ambayo mtu amepanga. Kila unapokutana na ugumu huwa unakuwa na kila sababu ya kuacha, utajishawishi kabisa kwa nini siyo muhimu sana kwako kuendelea kufanya au una kingine muhimu cha kufanya.

Unahitaji usimamizi wa karibu sana ili kuweza kufikia mafanikio makubwa. Na hapo ndipo mimi ninapoingia kwenye safari yako ya mafanikio.

Ninatoa huduma ya kuwa KOCHA WAKO BINAFSI, kwa kukusimamia kwa karibu ili uweze kufikia malengo makubwa ambayo umejiwekea. Ninapokuwa kocha wako, sikuruhusu ukate tamaa kirahisi, ninakusaidia uweze kupambana zaidi mpaka upate unachotaka.

Kama kuna kitu umekuwa unapanga kwa miaka mingi lakini utekelezaji unakuwa mgumu, karibu kwenye huduma hii ya KOCHA BINAFSI na nitakusaidia kwenye kufanyia kazi mipango hiyo.

Kama unahitaji huduma hii ya KOCHA BINAFSI niandikie kwenye wasap namba 0717396253. Karibu sana.

#5 TAFAKARI YA KUFIKIRISHA; IMALIZE SIKU YAKO HIVI.

“Finish each day and be done with it. You have done what you could; some blunders and absurdities have crept in; forget them as soon as you can. Tomorrow is a new day; you shall begin it serenely and with too high a spirit to be encumbered with your old nonsense.” – Ralph Waldo Emerson

Kila siku yako inapoisha, malizana nayo. Umefanya kila ulichoweza kufanya, umekosea na uzembe ulikuingia, sahau yote hayo haraka iwezekanavyo. Kesho ni siku nyingine mpya, unapaswa kuianza kwa usafi na hamasa ya hali ya juu ya kuachana na makosa ya nyuma.

Watu wengi wanapoweka mipango ya maisha yao, halafu siku moja ikavurugika, basi wanaruhusu siku zote zivurugike. Usikubali hili litokee kwako rafiki yangu. Kama siku yako moja imeharibika, anza siku inayofuata kwa upya wake, usikubali iharibiwe na jana. Jana imeshapita, leo una siku mpya, itendee vyema siku hiyo mpya.

Kila siku mpya kwako ni siku ya kuyaanza maisha yako upya, bila ya kujali jana uliharibu kiasi gani. Usikubali makosa yoyote ya jana yakuzuie kufanya kwa ubora leo.

Rafiki, nakutakia kila la kheri kwenye yale makubwa unayokwenda kufanyia kazi kwenye juma namba 47 la mwaka huu 2018. Nenda kaishi juma hilo kwa misingi yote ambayo tumekuwa tunashirikishana na utaweza kupiga hatua kubwa kwenye maisha yako.

Makala hii imeandikwa na Kocha Dr Makirita Amani.

Dr. Makirita ni Daktari wa binadamu, Kocha wa mafanikio, Mwandishi na Mjasiriamali.

Dr. Makirita anaendesha mafunzo ya mafanikio kwa wale waliojitoa hasa kufanikiwa kupitia program ya KISIMA CHA MAARIFA.

Kama bado hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA, tuma sasa ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa njia ya wasap namba 0717 396 253 (tumia wasap tu)

Kupata huduma nyingine za ukocha tembelea www.amkamtanzania.com/kocha

Kupata vitabu vizuri vya kusoma tembelea www.amkamtanzania.com/vitabu

Usomaji