Mara nyingihuwa tunajifunza jinsi ya kufanya vitu, kisha tunafanya hivyo kwa maisha yetuyote. Tunafika hatua ya kuwa tunafanya kwa mazoea na hakuna tena ubunifu. Kadiritunavyozidi kurudia kufanya kile kile kila siku ndivyo hamasa pia inavyoshukana kushindwa kupiga hatua.
Ili tuendelee kuwa na hamasa ya kufanya zaidi, ili tuweze kuwa wabunifu na kuja na njia tofauti, lazima tuweze kufanya tofauti na tulivyozoea kufanya. Lazima tuwe tunajaribu vitu vipya ambavyo hatujawahi kufanya na kupitia vitu hivyo vipya tunajifunza kile ambacho hatukuwa tunajua.
Lakini wengi huwa hawajui waanzie wapi kufanya vitu vipya, kwa sababu hata wanapofikiria kuboresha wanachofanya, bado wanaanzia pale pale walipo na hivyo kujikuta hakuna cha tofauti sana ambacho wamefanya.
Njia rahisi ya kufanya vitu vipya ni kujiuliza kama usingekuwa unajua chochote kuhusu unachofanya sasa, ungefanyaje? Kama ungekuwa ndiyo mgeni kabisa, hujui unachofanya kinafanywaje, je ungefanya vipi?
Kwa kujiuliza swali hili utaanza kupata picha ya tofauti na ulivyozoea, utaanza kuona vitu kwa mtazamo wa tofauti na kuona hatua tofauti za kuchukua.
Wakati mwingine jiulize kama wewe ndiye unayepokea kile unachofanya, yaani kama ndiyo mteja unayetegemea huduma unazotoa, kipi cha tofauti ungependa kupata? Kwa njia hiyo pia utapata njia bora zaidi za kufanya chochote unachofanya.
Jiulize maswali haya mara kwa mara, hata kama huyafanyii kazi mara moja, bado majibu utakayoyapata yatakuwa na manufaa makubwa sana kwako. Yatakufanya uone vitu kwa mtazamo mwingine na hata kuboresha namna unavyofanya maamuzi yako.
Nikukumbushe rafiki, kama unataka kupata matokeo ya tofauti na unayopata sasa, lazima uwe tayari kufanya tofauti na unavyofanya sasa. Na njia ya kufanya tofauti ni kufikiria kama ndiyo unaanza na hujui, hii itakupa mtazamo sahihi wa yale ambayo ni muhimu zaidi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,