“Anything you’re good at contributes to happiness.” — Bertrand Russell

Ni siku nyingine mpya, siku bora na ya kipekee sana kwetu.
Siku tuliyokuwa tukiisubiria kwa shauku kubwa ili kuweza kutekeleza mipango tuliyojiwekea.
Twende tukaitumie vizuri nafasi hii nzuri ya leo ili tuweze kufanya makubwa zaidi.

Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunatumia msingi huu kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari KIUNGO KINGINE CHA FURAHA…
Kiungo kingine cha furaha ni ubobezi,
Kitu chochote ambacho umebobea, kitu ambacho unaweza kukifanya vizuri sana na kwa viwango vya juu sana, kinachangia sana kwenye furaha yako.

Kama kuna kitu unaweza kukifanya vizuri, na wengine wanakutegemea katika kufanya kitu hicho, kinachangia wewe kuwa na furaha.
Kwa sababu unaiona maana ya wewe kuwa kwenye hii dunia, unauona mchango wako kwenye maisha ya wengine na ile hali ya wengine kukutegemea, inakupa kujiamini na kuona mchango wako ni muhimu.

Lakini kama huna chochote ambacho unaweza kufanya vizuri na kwa ubora,
Kama huna chochote ambacho wengine wanaweza kutegemea kutoka kwako,
Maisha yako yanakosa maana kwako na hilo linachangia kukosa furaha kwenye maisha yako.
Utajiona upo upo tu nw hakuna yeyote anayekutegemea ili maisha yake yawe bora.

Ili kuwa na furaha zaidi kwenye maisha yako, chagua kitu au eneo ambalo utabobea, eneo ambalo wengine watakutegemea kupitia unachofanya, eneo ambalo ukifanya kitu wengine wanajua huyu ni fulani kafanya na wanaamini na kupokea kile ulichofanya.
Hili lipo ndani ya uwezo wako, ni wewe kuanza kuchukua hatua ili kuyafanya maisha yako na ya wengine kuwa bora zaidi.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuchagua eneo ambalo utabobea na wengine waweze kukutegemea kwenye eneo hilo.
#Fanya #HakunaSababu #NiLeoTu #IngiaMzimaMzima #AnzaNaHatuaMoja #MafanikioNiHakiYako #NidhamuMsingi #WhatEverItTakes #WachaManenoWekaKazi #SkinInTheGame #OwnTheDayOwnYourLife #UsileteSababuLetaMatokeo #MudaNiSasa

Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha