Mwandishi mmoja amewahi kuandika, dunia haikulipi kile unachostahili kulipwa, bali inakulipa kile unachokubali kulipwa.

Hii ina maana kwamba, kipato ulichonacho sasa, siyo kile unachostahili kupata, bali kile ambacho umekubali dunia ikulipe. Na kama umekuwa na kipato cha aina hiyo kwa muda mrefu, hakiongezeki, basi wewe umekubaliana kabisa na dunia kwamba hakuna shida hata ikiendelea kukulipa unachopata sasa.

Kama isingekuwa hivyo, ungeshakataa, ungeshapambana, ungeshafanya vitu vya ziada ili tu ulipwe zaidi. Kama kipato unachopata kisingekuwa kinakutosha hata kupata chakula, usingekaa kama ulivyokaa sasa, ungepambana, ungefanya kazi za ziada, ungejituma zaidi mpaka kipato chako kikuwezeshe kuendesha maisha yako.

Leo nataka nikukumbushe na kukusisitizia hili muhimu sana, kwamba dunia inakulipa kulingana na thamani yako. Jinsi ambavyo wewe mwenyewe unajithaminisha, ndivyo na dunia nayo inakuthaminisha.

Kiasi cha fedha unacholipwa kwenye kazi au biashara unazofanya, ndiyo kiasi ambacho umekikubali kiakili, ndiyo kiasi ambacho kwa mtazamo wako ndiyo thamani yako. Kama thamani yako ya ndani ingekuwa juu zaidi kuliko kile unachopata, ungeshachukua hatua kuhakikisha unapata kile kinachoendana na thamani yako.

Hivyo basi rafiki yangu, kama unataka kuongeza kipato chako, sehemu sahihi ya kuanzia siyo kwenye kile unachofanya, na wala siyo kwa kwenda kwa mwajiri wako na kumwambia nataka ongezeko la mshahara.

Badala yake unapaswa kuanzia ndani yako, unapaswa kuanza na mtazamo ambao unao, unapaswa kuanza na ile thamani uliyonayo ndani yako. Kwa kuanza na kukuza thamani ya ndani, thamani ya nje nayo inaanza kubadilika, utaanza kutoa kazi za tofauti na kila mtu ataona unastahili kulipwa zaidi.

Thamani yako ya ndani inavyokuwa kubwa zaidi, unaanza kutoa thamani kubwa ya matumizi kuliko unayopata kwenye fedha, na hapo kinachofuatia ni fedha kuongezeka zaidi.

Unapoanza kujichukulia kwa uzito tofauti, unapoona kile unachofanya kina umuhimu mkubwa kuliko ulivyozoea na unapoanza kufanya kwa ubora zaidi ya ulivyozoea, kipato chako nacho kinaanza kukua zaidi.

Sehemu pekee ya kuanzia katika kuongeza kipato chako, katika kupiga hatua zaidi ya pale ulipo sasa, ni kuanzia kwenye mtazamo wako.

Mtazamo wako unafanya kazi kama pasi ya umeme, moto unaotoka kwenye pasi hauwezi kuzidi kiwango cha moto ambacho umekiweka, ukizidi tu pasi inajizima mpaka moto ule upungue. Kama unataka pasi itoe moto zaidi, lazima uweke kiwango cha juu zaidi cha moto.

Kadhalika, kipato unachopata wewe ni kutokana na ukomo uliojiwekea kwenye mtazamo wako kuhusu kipato unachoweza kuingiza. Ndiyo maana siku ukipata kipato cha ziada, utakitumia vibaya mpaka kiishe, maana akili yako haijazoea kuwa na kipato cha aina hiyo.

Hivyo lazima uanze kwenye mtazamo wako, kwa kuongeza kiwango chako cha kipato kifikra, kupandisha zaidi thamani unayojifikiria kuwa nayo. Kwa namna hii hutaridhishwa tena na matokeo madogo unayopata sasa, utafanya zaidi na kutegemea kupata zaidi.

Anza na thamani ya ndani na dunia itakulipa zaidi kadiri thamani hiyo inavyokuwa zaidi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha