Hongera sana mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo. Ni nafasi bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari AKILI ZA KAMARI…
Rafiki, watu wengi huwa hawajui kazi kubwa unayopaswa kuifanya KIMWILI, KIAKILI NA KIROHO ili uweze kufanikiwa.
Wengi wanafikiri mafanikio yanakuja tu, ukishayataka.
Na hii ndiyo sababu wachache pekee ndiyo wanaofanikiwa pamoja na kwamba wahitaji wa mafanikio ni wengi.
Rafiki, kazi kubwa sana unayopaswa kuifanya kifanikiwa!
KIAKILI; Lazima ujue kwa hakika nini unataka, unataka kukipata lini na njia ipi sahihi ya kukipata.
KIROHO; Lazima uamini sana kwenye kile unachotaka, ujiamini wewe mwenyewe na uiamini ile njia sahihi ya kukipata, usiwe na mashaka yoyote kwenye imani hizo.
KIMWILI; Lazima uwe tayari kuusukuma mwili zaidi ya ulivyozoea, kufanya zaidi ya kawaida na kuunyima baadhi ya vitu ambavyo mwili unataka.
Vitu hivi vitatu lazima viende pamoja, kwa utatu wake, na hakipaswi kuachwa nyuma hata kimoja.
Sasa shida kubwa sana, shida ambayo inawavuruga wengi na kuwazuia kufanikiwa, ni kitu nakiita AKILI ZA KAMARI.
Hizi ni akili za kufikiria ipo njia ya mkato na rahisi ya kupata kile unachotaka, ambayo haihusishi kufanya kazi.
Kwa akili hizi ndiyo unawakuta watu wanaota mchana, ndoto za kijinga kama kufikiri kuna bahati fulani itawaangukia na wataondoka kwenye changamoto walizonazo.
Hizi ndizo akili zinazowafanya watu wacheze michezo ya bahati nasibu na kubahatisha.
Hizi ndizo akili zinazowapelelea wengi kutapeliwa.
Sasa shida kubwa ya akili hizi siyo tu kujaribu njia hizo, bali zinabomoa ule msingi muhimu wa mafanikio.
Ukishafikiria na hata kujaribu njia ya mkato ya mafanikio, maana yake unakuwa umepoteza imani kabisa na ile njia sahihi uliyokuwa unaitumia awali. Hivyo hata kama utarudi kuitumia, bado hutaiamini moja kwa moja na hivyo haitakusaidia.
Rafiki, tengeneza malengo imara na imani thabiti ambayo haiyumbishwi na chochote kile, uandae mwili wako kwa mapambano, kisha achana kabisa na AKILI ZA KAMARI.
Linapokujia wazo kwamba kuna njia fupi na rahisi ya kupata unachotaka, ondokana na mawzo hayo haraka sana na rudi kwenye njia yako sahihi.
Bila ya msimamo mkali kama huo, akili za kamari zitakusumbua sana.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kutumia AKILI, ROHO NA MWILI kwa mafanikio yako makubwa na kuachana kabisa na AKILI ZA KAMARI.
#Fanya #HakunaSababu #NiLeoTu #IngiaMzimaMzima #AnzaNaHatuaMoja #MafanikioNiHakiYako #NidhamuMsingi #WhatEverItTakes #WachaManenoWekaKazi #SkinInTheGame #OwnTheDayOwnYourLife #UsileteSababuLetaMatokeo #MudaNiSasa
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha