Wanasema nahodha mzuri hapimwi kwa utulivu wa bahari, na hili ni kweli kwenye kila eneo la maisha.

Pale mambo yanapokuwa vizuri, kila mtu anaweza kufanya anachosema atafanya.

Pale kila kitu kinapokwenda sawa, kila mtu anaweza kuishi kwa namna anavyopaswa kuishi.

Pale ambapo hakuna misukosuko yoyote, kila mtu anaweza kuishi kwa misingi ambayo amekuwa anaishi nayo, iwe ni ya dini, falsafa au misingi mingine ya kijamii.

Kwa kifupi, mambo yakiwa yanaenda vizuri, hutaweza kuzijua kwa uhakika tabia za watu. Ni rahisi kuigiza maisha pale mambo yanapokwenda vizuri.

Ni mpaka pale mambo yanapokwenda vibaya, pale mambo yanapokuwa magumu, pale misukosuko haiishi, ndipo unapoweza kuzijua kwa hakika tabia za watu.

Maana ni nyakati hizo ambapo misingi ambayo mtu anaiishi inajaribiwa, na kama haikuwa misingi ya kweli, unaanguka mara moja.

Tumekuwa tunawaona watu wanawalalamikia wenzao kwa kubadilika pale wanapokutana na magumu.

Labda ni watu walikuwa wakiishi pamoja kama mke na mume wakati mambo yapo vizuri, lakini ugumu unapokuja ndoa inavunjika.

Au ni mtu ambaye alikuwa mshika dini mzuri, lakini akapatwa na msukosuko mkubwa uliomfanya aachane na dini yake na kutafuta msaada kwa njia ambazo ni kinyume na dini yake.

Au hata ni kiongozi ambaye watu walimpenda na kumwamini wakati mambo yanakwenda vizuri, lakini wakati wa ugumu akabadili misimamo yake na watu wakapoteza imani kwake.

Rafiki, haya tunayoona yanatokea kwa wengi na hata kwetu wakati tunapokutana na magumu, yanasababishwa na kukosa ukomavu wa kimaisha.

Kipimo sahihi cha ukomavu kwenye maisha yako, ni kuweza kusimamia misingi unayoiishi bila ya kujali ni kitu gani kinaendelea kwenye maisha yako.  Wewe kila siku ya maisha yako unasimamia kile unachoamini, unaishi vile ulivyochagua, iwe mambo ni mazuri au mabaya, hilo halijalishi kwako.

Huu ndiyo ukomavu ambao tunapaswa kuufikia kama tunataka kuwa na maisha bora kwetu, yenye msimamo na wengine kuwa na imani na sisi.

Tunapaswa kuchagua maisha ambayo tunayaishi, na kisha kuyasimamia hayo kwa kipindi chote. Tunapokutana na neema sana au kukutana na mikosi sana, ndani yetu hatubadiliki, kwa sababu tunajua hayo ni ya nje na hayana nguvu ndani yetu.

Tunaweza kujifunza na kujijengea ukomavu wa aina hii kama tutachagua kuishi falsafa bora kwetu. Sehemu ambayo nimejifunza hili kwa kina ni kwenye falsafa ya Ustoa. Upo mfano wa mwanafalsafa Cato, ambaye alikuwa akipinga uongozi wa mabavu uliokuwepo katika kipindi chake. Kiongozi mmoja akamwambia kama utaendelea kunipinga nitakuua, na yeye akamjibu fanya unachofanya na mimi nitafanya ninachofanya, ni lini nilikuambia nitaishi milele?

Hii ni hatua ya juu kabisa ya ukomavu kimaisha, njia ya kuwa umechagua maisha utakayoyaishi na kuyasimamia kwa nyakati zote. Na huu ndiyo msimamo tunaopaswa kuwa nao kama tunataka kupata mafanikio makubwa kwenye maisha yetu.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha