Kila mtu anapenda kulipwa zaidi, lakini wengi hawapo tayari kuweka juhudi ili kulipwa zaidi. Wengi huishia tu kwenye malalamiko kwamba wanapaswa kulipwa zaidi. Lakini kwa kuwa malalamiko huwa hayana msaada, wanaishia kulipwa kidogo.
Popote ulipo, iwe umeajiriwa, umejiajiri au unafanya biashara, unapotaka kulipwa zaidi, kuna vitu vitatua ambavyo unapaswa kuvifanya, hivi vitatu ni lazima uvifanye, vyote kwa pamoja na siyo kuchagua kile unachopenda au unachoweza.
Moja; ongeza uzalishaji wako, fanya zaidi, toa matokeo zaidi, nenda hatua ya ziada kuliko ulivyozoea, toa kilicho bora zaidi. Huwezi kuzalisha vile vile ambavyo umekuwa unazalisha siku zote halafu ukataka ulipwe zaidi, ni kitu ambacho hakiwezekani.
Mbili; kuwa mbunifu zaidi, ubunifu utakuwezesha kuja na njia bora za kuzalisha zaidi na hilo litapelekea ulipwe zaidi. Kadiri unavyotumia ubunifu wako, ndivyo unavyokuja na njia bora kabisa za kufanya chochote unachofanya.
Tatu; jitofautishe na wengine, kama hakuna tofauti yako na wengine wanaofanya unachofanya, utaishia kulipwa sawa na hao wengine. Kwa sababu kama ukikataa, basi wengine watakubali na hivyo hakuna atakayekulipa wewe zaidi wakati wapo wengine kama wewe ambao watafanya kwa malipo kidogo. Jitofautishe na wengine kwa namna ambayo mtu ataweza kupata kitu fulani kwako tu na siyo kwa mtu mwingine. Ukifikia hatua hiyo, unakuwa na nguvu ya kupanga ulipwe kiasi gani, kwa sababu huwezi kulinganishwa na yeyote.
Kulipwa zaidi ni matokeo ya kile zaidi kilichopo ndani yako, kama ndani yako hakutakuwa na cha zaidi, jua kwamba nje hakitaongezeka chochote. Fanyia kazi mambo hayo matatu na utajikuta kipato chako kinaongezeka hata kabla hujaomba ongezeko. Kwa sababu kadiri thamani unayotoa inavyokuwa kubwa, ndivyo wanaoipokea wanakuwa tayari kulipa zaidi ili kuendelea kuipata.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,