Rafiki yangu mpendwa,

Juma namba 47 la mwaka 2018 linakwenda kuachana na sisi, masaa 168 tuliyoyaanza mwanzoni mwa juma hili, yanakwenda kumalizika. Lakini wakati muda huu unatuacha, hatupaswi kubaki watupu, hatupaswi kuwa kama tulivyolianza juma hili. Kama tutaruhusu hilo litokee, tutakuwa tumechagua kupoteza juma letu zima.

Kila juma tunapaswa kujifunza vitu vipya ambavyo hatukuwa tunavifahamu hapo awali. Kila juma tunapaswa kujaribu vitu vipya ambavyo hatujawahi kufanya hapo awali. Ni kwa njia hizo mbili, kujifunza mambo mapya na kujaribu vitu vipya ndiyo tunaweza kupiga hatua kubwa kwenye maisha yetu.

Kwa upande wa kujifunza, mimi nipo tayari kukushirikisha maarifa bora mara zote, na kwa upande wa kuchukua hatua, pia nipo kama kocha kukusimamia uchukue hatua sahihi, kama unashindwa kuchukua hatua hizo mwenyewe. Hivyo karibu sana tufanye kazi kwa pamoja ili uweze kufikia ndoto zako kubwa na mafanikio makubwa pia.

Juma hili nimekuandalia maarifa mengi na mazuri, tenga muda wako kujifunza haya kwa kina, tafakari jinsi yanavyohusika na kila eneo la maisha yako, kisha chukua hatua mara moja.

Karibu kwenye tano za juma, tujifunze na kuchukua hatua ili kuyafanya maisha yetu kuwa bora zaidi.

#1 KITABU NILICHOSOMA; MAWAZO 151 YA KUONGEZA MAUZO.

Moja kati ya vitabu nilivyosoma juma hili ni kitabu 151 QUICK IDEAS TO INCREASE SALES ambacho kimeandikwa na Linda Sparks.

Ni kitabu ambacho kimeeleza mawazo 151 ya kukuwezesha kuongeza mauzo zaidi kwenye chochote unachofanya.

Kabla hujasema mauzo hayakuhusu, nikukumbushe kwamba kila mmoja wetu anauza. Iwe umeajiriwa, umejiajiri, unafanya biashara au ni kiongozi kwa namna yoyote ile, kila siku unauza.

Maisha ni mauzo na yeyote anayeweza kuuza vizuri zaidi ndiye anayefanikiwa. Tunauza muda wetu, utaalamu wetu, uzoefu wetu, huduma zetu na hata bidhaa mbalimbali. Pia tunauza mawazo yetu, ushawishi wetu na hata ndoto na maono makubwa tuliyonayo.

Kwa kifupi kila kitu kwenye maisha kinategemea kuuza. Hivyo hatua ya kwanza kwako ni kuhakikisha unakuwa muuzaji mzuri.

Na ndiyo maana mimi rafiki yako, nimechukua muda kukushirikisha mawazo haya 151 ya kuweza kuuza zaidi.

Neno; mwandishi anasema mawazo yote haya 151 yanafanya kazi vizuri, lakini siyo yote yatakufaa kwa wakati mmoja, hivyo pitia mawazo yote 151 na kisha chagua yale unayoweza kufanyia kazi sasa hivi. Kila siku endelea kuyapitia na kuna fursa zitakazojitokeza ambazo zitakuwezesha kutumia mawazo mengine ambayo hujayatumia sasa.

Baada ya hayo machache ya utangulizi, sasa twende moja kwa moja kwenye mawazo hayo 151 ya kuongeza mauzo zaidi.

  1. Lazima uwe na mpango wa maendeleo ya biashara ambao unajumuisha kila kinachofanyika kwenye biashara. Mpango huu unapaswa kujulikana na kila mtu. Kila kinachofanywa kwenye biashara lazima kiwe na lengo la kuwafanya wateja waendelee kuwepo na walete wateja wengine zaidi.
  2. Zipo njia nyingi za kuwafikia wateja wa biashara yako, tumia nyingi uwezavyo na usitegemee moja au chache pekee. Njia unazoweza kutumia; matangazo, maonesho ya kibiashara, taarifa kwa uma, tovuti, mauzo ya moja kwa moja, uandishi na mafunzo mbalimbali.
  3. Hatua tatu kwenye mpango wa maendeleo ya biashara; moja mteja kukujua, mbili, mteja kununua, tatu, mteja kuendelea kununua zaidi. Kila hatua ina mambo ya kuzingatia ili kufanikiwa.
  4. Tengeneza imani kwa wateja tarajiwa, kabla mteja hajanunua kwako, lazima kwanza akuamini, na hilo ndiyo jukumu lako la kwanza, la kutengeneza imani.
  5. Hatua tatu za mzunguko wa mauzo, moja kuwatambua wateja sahihi wa kile unachouza, mbili, kuwaandalia pendekezo la kile unachotaka kuwauzia, huku ukieleza manufaa watakayopata. Tatu, kuwasilisha pendekezo la mauzo kwa mteja na kumshawishi kununua.
  6. Mauzo hayaishi pale mteja anaponunua, bali ndiyo yanaanza. Mteja akishanunua, jua imani yake kwako ni kubwa, hivyo angalia kipi zaidi unaweza kumuuzia na atakuwa tayari kununua zaidi na zaidi, kama ulichomuuzia mwanzo ni sahihi kwake.
  7. Wateja hawanunui kile unachouza, bali wananunua suluhisho la matatizo yao. Hivyo elezea unachouza kwa namna kinatatua matatizo waliyonayo.
  8. Ijue thamani ya maisha ya mteja kwako, kisha kuwa tayari kulipa gharama kumpata. Kwa mfano kama mteja ananunua kwako mara moja kila mwezi, na kila akinunua unapata faida ya shilingi elfu 10, kwa mwaka unapata faida ya laki moja na ishirini kwa mteja huyo. Kama mteja atakuwa na wewe kwa miaka mitano, atakuingizia faida ya laki sita. Je hutakuwa tayari kulipa laki moja kumpata mteja wa aina hii?
  9. Unapaswa kuwa na malengo ya kibiashara kwenye kila eneo la biashara yako, ambayo yanafanyiwa kazi ili kuikuza biashara hiyo.
  10. Jua ni thamani gani unayoongeza kwa wateja wako na simamia hiyo. kadiri unavyoongeza thamani zaidi, ndivyo unavyotengeneza fedha zaidi.
  11. Tumia mali ambazo tayari zipo kwenye biashara kuongeza mauzo zaidi. Mfano wa mali hizo ni wateja ulionao sasa, wafanyakazi ulionao, na hata sifa nzuri ya biashara yako. Vyote hivi ukivitumia vizuri utaweza kuuza zaidi.
  12. Tumia njia zilizoonesha mafanikio kipindi cha nyuma na ziboreshe zaidi. Kama kuna njia fulani iliyokupa matokeo mazuri, basi hiyo ni njia sahihi na usiiache, endelea kuitumia na kuiboresha zaidi.
  13. Pata wateja zaidi, lakini ambao ni wazuri na sahihi kwa biashara yako. siyo kila mteja atakufaa, hivyo chagua aina ya wateja ambao utaweza kuwahudumia vizuri, na tafuta wengi wa aina hiyo.
  14. Jua wateja wako wanatokea zaidi eneo gani kisha kuwa na kitu cha kuwakumbusha wateja wako kwenye eneo hilo.
  15. Punguza mzigo kwenye biashara yako, kama kuna wateja ambao ni mzigo kwa biashara yako, wapunguze. Kama tulivyoona hapo juu, siyo kila mteja ni sahihi kwako, chagua wale sahihi na achana na wengine.
  16. Tengeneza sifa na jina zuri la biashara yako (brand) ambalo litajiuza lenyewe. Kama biashara yako haijawa na jina lenye sifa nzuri, anza kulijenga sasa.
  17. Shirikiana na jamii inayokuzunguka, ishirikishe kuhusu biashara yako kwa sababu jamii hiyo ndiyo ina wateja wako.
  18. Kila njia inapelekea kwenye mauzo. Chochote unachofanya kwenye biashara yako, jiulize je kinakuwezesha kuuza zaidi, kama jibu ni hapana, achana na kitu hicho. Kila unachofanya, kinapaswa kupelekea kuuza zaidi.
  19. Matangazo yana sehemu yake. Japo matangazo yana gharama kubwa, kuna wakati unahitaji matangazo ili kuwafikia wengi zaidi.
  20. Taarifa kwa uma ni njia rahisi na isiyo na gharama ya kuufanya uma ujue kuhusu uwepo wa biashara yako. Hapa biashara yako inatoa taarifa fulani zenye maslahi kwa uma na watu wanajua uwepo wa biashara hiyo.
  21. Waandishi wa habari wanahitaji habari zaidi kwa ajili ya vyombo vyao vya habari. Unaweza kutumia nafasi hiyo kuwashirikisha habari mbalimbali zinazohusiana na biashara yako. Hapa inakuwa kama umepata nafasi ya bure ya kutangaza biashara yako.
  22. Habari kuhusu biashara yako inapotangazwa au kuchapwa kwenye vyombo vya habari, omba ruhusa ya kusambaza habari hiyo zaidi. Kadiri wateja wanapoona biashara yako imeshirikishwa kwenye vyombo vya habari wanaiamini zaidi.
  23. Vyombo vya habari ni rafiki yako, siyo mama yako. Vyombo hivi vinataka vitu vinavyoendana na yale wanayotangaza. Hivyo unapokuwa na habari kuhusu biashara yako, angalia ni vyombo gani na vipindi gani vitaifaa habari hiyo.
  24. Tengeneza urafiki baina ya biashara yako na jamii inayoizunguka. Ifanye biashara yako kuwa sehemu ya jamii, watu waione kama kitu chao na hapo utaweza kuuza zaidi.
  25. Tovuti ni zaidi ya matangazo yanayoruka kwa masaa 24 kila siku. Unapaswa kuwa na tovuti inayomweleza mteja wako kila kitu kuhusu biashara yako.
  26. Mpango wako wa bei nao ni njia ya kuitangaza zaidi biashara yako. Kuwa na bei rafiki na kutoa thamani zaidi kutakuwezesha kuuza zaidi. Lakini epuka kuuza kwa bei ya chini au kupunguza bei.
  27. Shirikiana na biashara nyingine kwenye kutangaza. Kama kuna biashara ambazo mnashirikiana wateja, lakini hamuuzi kitu kimoja, mnaweza kushirikiana kutangaza kwa pamoja na mkawafikia wateja wenu.
  28. Maonesho ya kibiashara ni sehemu nzuri ya kujua zaidi kuhusu soko la biashara yako na wateja pia. Tumia maonesho kujifunza zaidi kuliko kutegemea kuuza zaidi kwenye maonesho.
  29. Uza moja kwa moja na kupitia wauzaji wengine pia. Usitumie njia moja pekee, kuuza moja kwa moja kunakupa faida kubwa, lakini pia kuuza kupitia wengine kunakuwezesha kuwafikia watu wengi zaidi.
  30. Wasiliana na watu ambao hata huwajui, kwa lengo la kuwafanya wajue biashara yako na huduma unazotoa. Usiishie tu kufanya biashara na wateja ulionao sasa, endelea kuongeza wengi zaidi kwa kuwasiliana na hata ambao hawakujui.
  31. Chagua eneo ambalo utaweza kulisimamia na kulihudumia vizuri. Wafanyabiashara wengi hupenda kuuza kwa kila mtu na kila eneo, lakini hii ni njia inayochisha. Ni bora kuchagua eneo moja ambalo utalijua vizuri na kulihudumia vizuri kabla hujaenda kwenye maeneo mengine zaidi.
  32. Kuwasiliana na wateja wako kwa barua au barua pepe bado kuna manufaa makubwa. Kwa zama hizi, hakikisha unakuwa na barua pepe za wateja wako na mara kwa mara wasiliana nao.
  33. Chapisha mawazo yako kwa njia mbalimbali, kupitia uandishi au njia nyingine, hapa utajiweka kama mtaalamu aliyebobea na wale wanaojifunza watakuamini na kununua kwako zaidi.
  34. Jihusishe na mambo ya kijamii kwa kupeleka sehemu fulani ya faida unayoipata kusaidia matatizo ya kijamii. Hili litawasukuma watu kununua, wakijua faida inayopatikana inapelekwa kwenye misaada fulani hivyo nao wanakuwa wamechangia misaada hiyo.
  35. Tafuta na tumia nafasi za kuongea na kuwafundisha wengine, hilo litakupa nafasi ya kujulikana zaidi na hata kuweza kuuza zaidi pia.
  36. Njia bora ya kupata wateja wapya ni kuwatumia wateja ulionao sasa. Washawishi wateja ulionao wakuletee wateja wengine, kwa kuwaambia watu wao wa karibu kuhusu wewe. Wateja wanaoletwa na wateja, huwa wanakuwa wateja bora sana.
  37. Andaa tukio la kibiashara au shiriki kwenye matukio mbalimbali yanayoandaliwa kama sehemu ya kuitangaza zaidi biashara yako. matamasha mbalimbali ya michezo ni njia nzuri ya kutangaza biashara yako.
  38. Pangilia shughuli zako unazofanya kwenye biashara zote ziendane na kupeana nguvu zaidi. Kuanzia manunuzi, mauzo, huduma kwa wateja, vyote vilenge kuongeza mauzo zaidi.
  39. Tengeneza malengo ya mauzo na kipimo cha kupima malengo hayo, pamoja na ukomo wa muda. Kisha kila mtu achukue hatua kukamilisha malengo hayo.
  40. Tengeneza mikakati bora ya kukuwezesha kufikia malengo ya mauzo uliyojiwekea.
  41. Uza zaidi kwa wateja ambao tayari unao, hii ni hazina kubwa kwenye biashara yako. Wafanyabiashara wengi huwasahau wateja walionao na kukimbizana na wateja wapya kila siku. Usimpoteze mteja hata mmoja ambaye umewahi kumuuzia.
  42. Tafuta njia ya kuboresha mahusiano yako na wateja, angalia vitu gani mnapendelea kisha kuwa na mazungumzo kwenye maeneo hayo.
  43. Tumia muda mfupi kukamilisha mauzo yako kwa mteja mmoja ili uweze kuwauzia wateja wengi zaidi.
  44. Tengeneza ushirikiano kwenye biashara yako, watu wote wafanye kazi kama timu moja kushirikiana rasilimali zilizopo kwa maendeleo ya biashara.
  45. Moja ya njia bora za kuongeza mauzo ni kuja na uvumbuzi mpya ambao unapatikana kwako tu. Hili litawafanya wateja kuja kwako kwa sababu hawawezi kupata sehemu nyingine.
  46. Tengeneza kalenda ya matukio yako ya kibiashara, wakati gani utatoa bidhaa au huduma mpya na wakati gani utahitaji kupata wasaidizi zaidi. Unapokuwa na kalenda unajiandaa mapema kabla ya muda.
  47. Nenda na msimu au vitu vinavyovuma na ona jinsi gani unaweza kuhusisha biashara yako na msimu ambao upo. Watu wengi hupenda kufanya maamuzi kupitia kundi, hivyo unapoiweka biashara yako kwa namna ambayo kundi inalielewa, utauza zaidi.
  48. Wateja wananunua siyo kwa sababu wewe unauza, ila kwa sababu wana matatizo na uhitaji wa unachouza, elewa hilo na litumie kuwafikia wateja wengi zaidi.
  49. Wajue vizuri wateja wako kisha washirikishe fursa mbalimbali zitakazowasaidia zaidi. Kwa kuchukua hatua hizo, wateja watakufikiria muda wote na wanapokuwa na uhitaji wanakuja kwako.
  50. Imarisha sana mawasiliano yako na wateja wako ili usiwapoteze. Ukipoteza mteja mmoja, inabidi utafute wengine wawili ndiyo utakuwa umerudi pale ulipokuwa. Hivyo usipoteze mteja yeyote.
  51. Jua malengo na maono makubwa ya wateja wako, kisha ona jinsi gani biashara yako inawasaidia kufikia malengo hayo, waeleze hilo na watakuwa tayari kununua kwako.
  52. Jitengenezee nasafi yako kwenye soko, nafasi ambayo utailinda na kuifanyia kazi kuhakikisha wateja wako wanaendelea kupata huduma bora.
  53. Zijue bajeti za wateja wako na hilo litakusaidia kuweza kuwapatia kile kinachowafaa kulingana na bajeti waliyonayo.
  54. Ongea lugha ya mteja, kama mteja hakuelewi au havutiwi na wewe, hutaweza kumuuzia hata kama bei ni ndogo kiasi gani. Kila mteja kuna vitu anapendelea, ukijua na kutumia hivyo, utaweza kuuza zaidi.
  55. Kuridhika kwa mteja ndiyo jukumu lako kuu, hivyo usiishie tu kuuza, bali fuatilia kuona ni kwa namna gani mteja ameridhishwa kwa kile alichonunua.
  56. Kuwa na taarifa za kutosha kuhusu washindani wa mteja wako, kisha tumia taarifa hizi kumsaidia kufanya maamuzi bora. Mfanye mteja aone kununua kwako kunamwezesha kushinda zaidi.
  57. Ielewe vizuri sekta unayofanyia biashara, elewa sekta ya wateja wako ili uweze kuwahudumia vizuri.
  58. Wawezeshe wateja wako kuziona fursa zaidi na kuzitumia kupiga hatua zaidi.
  59. Jua hali ya kifedha ya wateja wako, hasa mapato na matumizi, hili litakupa picha kwenye uwezo wao wa kununua lakini pia litakupa picha ya manunuzi wanayopendelea kufanya zaidi.
  60. Mwoneshe mteja jinsi ambavyo kutumia bidhaa au huduma unayomuuzia kutampunguzia gharama za kuendesha maisha yake au biashara yake. Hivyo ni muhimu kujua gharama zinazomsumbua.
  61. Jua mteja anapendelea kuongolea nini, kisha anzisha mazungumzo kwenye maeneo anayopendelea na utamfanya anunue zaidi.
  62. Yajue malengo ya muda mfupi ya mteja wako, hasa unapofanya biashara na biashara nyingine, kwa sababu malengo hayo ya muda mfupi ndiyo yanayowasukuma kufanya maamuzi.
  63. Hakikisha unakuwa na taarifa sahihi za wateja wako, na ziandike kwa usahihi, usimpoteze mteja kwa sababu tu umekosa taarifa zake sahihi, huo unakuwa ni uzembe wa kujitakia.
  64. Jiunge na yale yanayoendelea kwenye jamii na kwenye dunia, kama ni msimu wa sikukuu basi andaa yale yanayoendana na msimu huo. Kila biashara zina msimu wake, jua msimu wa biashara yako na jiandae vizuri.
  65. Watu wanapenda sana kusherekea, ona jinsi gani unaweza kutumia kusherekea kwa watu kama sehemu ya kutangaza zaidi biashara yako.
  66. Fuatilia sheria na taratibu zinazohusiana na biashara yako na jua mabadiliko yoyote yanayotokea na jinsi yanavyoweza kuathiri mauzo.
  67. Sherehe za kitaifa kama siku ya uhuru, siku ya mashujaa na kadhalika ni wakati mzuri wa kuungana na wengine kupitia biashara yako, na kuwafanya wanunue zaidi kile unachouza kama sehemu ya sherehe ya kitaifa.
  68. Watu wanapenda kushiriki matamasha mbalimbali, shiriki kwenye matamasha kama biashara au andaa tamasha lako la kibiashara na iwe sehemu ya kutangaza na hata kuuza zaidi.
  69. Shirikiana na taasisi za kijamii zinazotatua matatizo ya kijamii kama magonjwa sugu, watoto yatima, magonjwa ya watoto na kadhalika. Mteja akijua kwamba kwa kununua kwako anachangia mambo ya kijamii pia, anakuwa tayari kununua zaidi.
  70. Kuna sherehe nyingine kama siku ya mama au siku ya baba, watu wengi huwa wanazichukulia hizi sherehe kama sehemu ya kuwakumbuka wazazi wao, ona jinsi gani biashara yako inaweza kuhusika na kuwafanya watu wanunue zaidi kwa ajili ya wazazi wao.
  71. Wape wateja wako taarifa sahihi zinazowawezesha kufanya maamuzi. Tunaishi kwenye kipindi cha mafuriko ya taarifa na maarifa, watu hawajui hata waamini nini maana maarifa ni mengi na yanakinzana. Jiweke wewe kama mtu unayetoa taarifa sahihi kwa wateja wako na watakuamini na kununua kwako.
  72. Kuwa jasiri kwa kuwa na kitu ambacho unakisimamia hata kama kuna wengine wanapingana nacho. Kwa njia hii utawakosa baadhi ya wateja, lakini utawapata wateja wanaosimamia unachosimamia na watakuwa wateja wanaokuamini sana.
  73. Kuwa wewe, wateja wanapenda kununua kwa mtu ambaye ni halisi, ni yeye na siyo anayeiga kwa wengine. Washirikishe wateja wako kuhusu wewe, wape hadithi zako na hili litawafanya wateja wako kuona wewe ni rafiki yao. Kama unaiga au kuigiza, wateja wataona hilo na watapoteza imani kwako.
  74. Kuwa mwema, onesha kujali kwa kweli kuhusu wateja wako. Usiwe tu mtu ambaye unataka kupata faida, bali onekana kuwa mtu ambaye unajali maisha ya wateja wako kuwa bora zaidi.
  75. Usiogope kuwaeleza wateja kuhusu bei, waeleze na wafafanulie vizuri kulinganisha bei na thamani wanayopata. Usiogope kwamba mteja ataona bei ni kubwa, eleza zaidi thamani anayopata na bei itaonekana ni ya kawaida.
  76. Kuwa na vitu vya nyongeza ambavyo mteja anaweza kununua pia na usiogope kumjulisha mteja kuhusu hivyo vya nyongeza. Wakati bora kwa mteja kununua zaidi ni mara baada ya kuwa amenunua. Hivyo usimwache mteja akaondoka na kiu ya ununuzi ikiwa ndani yake, mpe vitu vingine vitakavyomfaa pia.
  77. Weka utaratibu mzuri wa malipo, makubaliano ya malipo yawe wazi na yanayoeleweka. Isitokee baada ya manunuzi mkaanza kusumbuana kulipana.
  78. Usiumizwe pale unapomweleza mteja kila kitu na bado hanunui, hujapoteza, bali umesogea karibu zaidi na mteja. Jua namba zako kibiashara, mfano ukiongea na watu 10 watatu wananunua. Hivyo wale saba wengine ni kukamilisha kuwapata watatu watakaonunua.
  79. Kwenye biashara ya duka na reja reja, kuwa na mpangilio mzuri wa bidhaa ambao unamvutia mteja. Hasa yale maeneo ambayo mteja anatumia muda wake mwingi, mfano wakati anasubiria kufanya malipo.
  80. Unaweza kuwa na bidhaa au huduma unayoiuza kwa hasara, lakini lengo ni kuwaleta wateja kwenye biashara, kiasi kwamba wakifika watanunua na bidhaa nyingine ambazo utatengeneza faida. Angalia jinsi ya kutumia hili kwenye biashara yako.
  81. Toa zawadi kwa wateja wako, hata kama ni ndogo, wateja wanathamini zawadi na watakuja tena kwa ajili ya zawadi.
  82. Biashara kubwa huwa zinawatumia wasanii na watu maarufu kama mabalozi wao, kwa sababu watu wanawapenda watu maarufu, wanahamishia upendo huo kwa biashara wanazoziwakilisha.
  83. Kama unauza vitu vingi vinavyoendana, unaweza kuviweka kwenye kifungashio kimoja na kuuza vyote kwa pamoja kwa bei ya chini kuliko mteja angenunua kimoja kimoja.
  84. Tumia matangazo marefu, yale yanayotoa maarifa kuuelewesha uma hasa pale unapokuja na bidhaa au huduma mpya. Kadiri watu wanavyoelewa ndivyo wanavyokuwa wateja wazuri.
  85. Unaweza kuweka utaratibu wa kuwa na kadi za wateja wanaonunua mara kwa mara na wakifikisha kiwango fulani wanapata zawadi au ofa. Kadiri kiwango cha zawadi kinavyokaribia, ndivyo wateja wananunua zaidi.
  86. Mwandalie mteja zawadi ambayo hakuitegemea, zawadi ambayo ni ndogo lakini anakutana nayo bila ya kutegemea, hili linamfanya aikumbuke zaidi biashara yako.
  87. Pata nafasi ya kukaa na mteja wako na kumjua kwa undani zaidi, hiyo inakusaidia kumhudumia vizuri zaidi.
  88. Tumia vipaji ulivyonavyo kuhakikisha mteja anapata zaidi kwenye biashara yako kuliko anavyoweza kupata sehemu nyingine. Weka upekee wako kwenye biashara yako.
  89. Ifanye njia yako ya kufanya biashara iwe njia ya kukutangaza. Julikana kama mtu unayetekeleza kile unachoahidi, unayefanya kitu kwa usahihi na watu watakuja kwako wakitegemea kupata hayo.
  90. Angalia soko ambalo limeachwa au kupuuzwa na biashara kubwa kuliko wewe na lihudumie vizuri soko hilo, linaweza kuwa sehemu ya wewe kutokea.
  91. Kuwa na bajeti ya masoko na matangazo kwenye biashara yako. Eneo la masoko na matangazo ni eneo unalopaswa kulipa uzito unaostahili.
  92. Ifanye biashara yako kuwa sehemu rafiki kwa wateja wako kutembelea. Kama unafanya biashara ya mgahawa, hoteli au za namna hiyo, unaweza kutoa huduma za bure za mtandao wa intaneti, vitabu na hata majarida ya kujisomea.
  93. Tumia simu kutengeneza mahusiano bora na wateja wako, wasiliana nao mara kwa mara.
  94. Unapotumia mtandao wa intaneti kuwafikia wateja wako, unahitaji kuweka juhudi za ziada ili wateja wakuamini kwa sababu hawakuoni moja kwa moja. Tumia shuhuda za wengine waliohudumiwa vizuri ili kujenga imani.
  95. Kama unawakaribisha wateja kwenye biashara yako kwa kitu cha bure au cha bei ndogo, hakikisha unakuwa na njia bora ya kuwageuza kuwa wateja wanaolipa. La sivyo utaishia kuwa na wateja wengi ambao hawanunui mpaka kuwe na ofa au vitu vya bure.
  96. Watumie watu wengine kutangaza biashara yako na wanapoleta wateja, wape kamisheni kulingana na faida ambayo mteja ameingiza. Kwa kutumia programu ya aina hii, utawafikia wateja wengi zaidi.
  97. Tengeneza tukio la biashara yako kujitolea kwenye shughuli mbalimbali za kijamii, hili linaimarisha mahusiano na jamii.
  98. Tengeneza matukio ya biashara yako, ambapo unawaleta pamoja wateja wako na wafanyakazi wako. Hii inakuwa njia nzuri ya kuwafikia wengi.
  99. Angalia rasilimali zote ulizonazo na ona ambazo zinaweza kuwasaidia wengine na wao wakakusaidia kuitangaza biashara yako zaidi.
  100. Unaweza kuandaa maonesho maalumu ya biashara yako, hasa kuwafanya wateja wajue zaidi kuhusu biashara yako, maana unaweza kuwa na wateja lakini wasijue vitu vingine unavyouza.
  101. Shirikiana na wafanyabiashara wengine katika kutangaza kwa pamoja, hasa pale unapofanya biashara ambayo inaonekana haiwezi kujitofautisha. Unaposhirikiana na wengine, unaweza kuwapata wateja wao pia.
  102. Unapaswa kuwa na blogu ya biashara yako, sehemu ambapo unashirikisha maarifa na taarifa zinazohusiana na biashara yako. wateja wako watakufuatilia na kukuchukulia wewe kama mshauri muhimu kwao.
  103. Jifunze kutoka kwenye biashara ya vitabu, watu wengi walifikiri ujio wa intaneti na vitabu vya nakala tete utaua biashara ya vitabu, lakini ndiyo kwanza inashika nguvu. Na hii ni kwa sababu biashara hiyo inabadilika kila wakati, inamfanya mteja ajisikie vizuri kutembelea duka la vitabu, kwa kuongeza huduma bora zaidi kama sehemu ya kusomea, waandishi kukutana na wasomaji na kadhalika.
  104. Unaweza kupata nafasi ya kutangaza kwa kutoa sehemu ya faida yako kwa jamii, hii itakusaidia kama huna bajeti kubwa ya matangazo.
  105. Kama una huduma au bidhaa ambazo hazijauzwa na unataka kuzitoa kwa haraka, zitoe kwa namna ambayo itaitangaza biashara zaidi. Usitoe tu kama zawadi au kuuza kwa punguzo kiasi kwamba watu wakawa wanavizia wakati wa punguzo, unaweza kutumia kama sehemu ya kutangaza biashara yako zaidi, kwa kupeleka au kuzitangaza eneo ambalo watu hawajui kuhusu biashara yako.
  106. Baadhi ya biashara kubwa huwa zinatoa mashindano au bahati nasibu kwa mtu kushinda na kupata zawadi kubwa. Ona jinsi ya kutumia hili ili kuwafanya watu wanunue zaidi.
  107. Tengeneza jumuiya ya wateja wa biashara yako, mtu akiwa mteja wako anajiona yupo ndani ya jumuiya ambayo inamjali na hatoondoka.
  108. Ifanye biashara yako imwezeshe mteja kufanya kile anachopenda kufanya lakini anashindwa kukifanya.
  109. Kama biashara yako ni ya wateja kulipa kwa kujirudia, unapokaribia wakati wa mteja kulipa tena, mkumbushe manufaa anayoyapata kwa kuendelea kulipia huduma unayompa.
  110. Kama biashara yako ina kitu cha mteja kujaribu, usiogope kumpa mteja ajaribu, hata kama hatanunua, kitendo cha kujaribu kinamsogeza karibu zaidi na kununua.
  111. Angalia kama unaweza kutoa huduma ambayo mteja analipia ada moja na kupata huduma zote. Hii inamfanya mteja aone ananufaika zaidi, hata kama hatatumia kila kinachotolewa. Mfano mzuri ni kulipia kiasi kimoja lakini kuchagua kula chochote ambapo kunafanywa na baadhi ya migahawa.
  112. Angalia ndani ya mpango wako wa biashara kuona njia za ziada za kutangaza zaidi na kuongeza mauzo.
  113. Kama biashara yako inatumiwa watu kuuza, basi unapaswa kuwa na watu wengi sana wanaohusika kwenye mauzo. Kama bidhaa au huduma ina wateja, kadiri unavyokuwa na wauzaji wengi, ndivyo wateja wanapata huduma bora.
  114. Hakikisha kila anayehusika kwenye biashara yako anajua ni nini biashara hiyo inauza.
  115. Kila mfanyakazi wa biashara yako anapaswa kuielewa biashara yako kwa undani na aweze kuielezea kwa wengine na siyo kujua tu wajibu wake. Wafanyakazi wako ni watu wa matangazo pia.
  116. Tengeneza mfumo wa taarifa za biashara zako, ambapo kila mfanyakazi anaweza kueleza kwa kifupi mnajihusisha na nini, mnatoa huduma gani, mnatatua matatizo gani na mnalenga wateja wa aina gani. Mfanyakazi wako anaweza kukutana na mtu kwenye sherehe na akimweleza hayo akapenda na kuwa mteja.
  117. Watumie wale unaonunua kwao kama sehemu ya wewe kutangaza zaidi. Wauzaji hao wanakutana na wanunuaji wengi, wakijua unatoa huduma gani, itakuwa rahisi kwao kukuunganisha na wengine wanaohitaji huduma hiyo.
  118. Wateja ulionao sasa wanaweza kukusaidia kuuza zaidi, kwa kuangalia tabia zao katika manunuzi, unaweza kuwafikia wengine wenye tabia kama zao pia.
  119. Itumie jamii inayokuzunguka kuuza zaidi, hata kama watu hawajanunua kwako, waweke kama sehemu ya wateja tarajiwa na endelea kuwapa jumbe za kuifanya waijue biashara yako. kadiri wanavyosikia kuhusu wewe, ndivyo wanavyokufikiria na kutaka kujaribu kufanya biashara na wewe.
  120. Unapaswa kukusanya taarifa nyingi na za kutosha kuhusu wateja wako na hata wale ambao siyo wateja wako. Kadiri unavyokuwa na taarifa nyingi zaidi ndivyo unavyoweza kuuza zaidi. Mfano kama ukijua tarehe ya kuzaliwa ya mteja wako, kisha tarehe hiyo inapofika ukamtakia heri ya siku ya kuzaliwa, ni rahisi kumkaribisha kununua baada ya salamu hizo.
  121. Wafanyakazi wa biashara yako lazima wawe watu wenye mtazamo chanya, mtazamo wa kuwapa hamasa wateja ili waweze kununua. Kama wafanyakazi wamepoa na hawana msukumo wa kuwahamasisha wateja, hutaweza kuuza kwa wengi.
  122. Tengeneza utamaduni wa biashara yako, ambapo wafanyakazi wote wanakuwa na utaratibu fulani unaoisukuma biashara yako mbele zaidi.
  123. Yajue majukumu ambayo watu wanafanya kila siku ambayo yanaongeza mauzo kwenye biashara na hayo yapewe kipaumbele. Kipaumbele kikubwa kwenye biashara kinapaswa kuwa mauzo, maana ndiyo yanayoleta mapato kwenye biashara.
  124. Orodhesha njia zote ambazo unaweza kumpoteza nazo mteja, kisha usifanye hata kimoja kati ya hivyo.
  125. Kuna wakati wateja wanakuwa wamezoea biashara yako kiasi cha kuona hakuna jipya, hapa unaweza kuja na mpangilio mpya wa bidhaa au huduma zako na watu wakaona kama kuna upya.
  126. Weka vitu vinavyowavutia wateja kwenye biashara yako, hasa wakati wanasubiria, na hili litawafanya waamue kununua kwa kadiri wanavyoona vitu hivyo. Mfano supermarket huwa zinaweka bidhaa fulani kwenye maeneo ambayo wateja wanasubiria kulipia na hizo hununuliwa zaidi.
  127. Kabla hujakazana kuweka nguvu zaidi kwenye mauzo, tathmini upya kwanza soko lako. Kama soko ni dogo, hata ungeweka nguvu kiasi gani, bado mauzo yatakuwa chini.
  128. Tengenea kipindi kirefu cha matarajio, kama kuna huduma au bidhaa mpya unayoleta, wafanye wateja waitegemee mapema kabla ya siku ya kutoka kufika. Hii inawafanya wateja kusubiria kwa hamu na kuwa tayari kununua inapotoka.
  129. Uliza kwa nini tano kwa mteja wako ili kujua sababu halisi inayomsukuma kununua. Anza na kwa nini anataka kununua, akikupa jibu muulize pia kwa nini, akitoa jibu uliza tena kwa nini. Ukifika kwa nini ya tano, utakuwa umeshaifahamu sababu ya ndani ya mteja kununua, na itakuwa rahisi kwako kumuuzia.
  130. Usiwe tu muuzaji, bali kuwa mtatuzi wa matatizo ya wateja wako. Wafanye wateja wajue wanapokuwa na matatizo, mtu sahihi wa kuyatatua ni wewe.
  131. Tengeneza maelezo mazuri ya kuhusu biashara yako pale unapokwenda kuwasilisha kwa wateja wako, wafanye wateja wakukumbuke kwa namna ulivyoelezea biashara yako.
  132. Kuwa na lishe ya kiakili kila siku kama muuzaji. Ianze siku yako kwa kusoma kitu kinachokupa hamasa, kwa kutekeleza majukumu yaliyo muhimu na kushukuru kwa kila jambo. Haya yanakupa hamasa ya kuuza zaidi.
  133. Kuwa mbele ya mteja wako kila wiki, usiache mteja mpaka akakusahau sana. kumbuka mteja uliyenaye sasa hivi, kuna biashara nyingine zinamwinda, hivyo kama atakusahau, atabebwa na wengine. Mara kwa mara kuwa na mawasiliano ambayo yanamfanya mteja asikusahau.
  134. Wekeza zaidi ndani yako, kadiri unavyowekeza ndani yako kwa kuwa na maarifa sahihi kuhusu biashara yako na kuhusu uuzaji, ndivyo unavyoweza kuuza zaidi.
  135. Kuwa mtaalamu aliyebobea kwenye biashara unayoifanya, andaa mafunzo kwa wateja na uma kwa ujumla, hili litawafanya watu wakuamini na kuona ni mtu sahihi kwao.
  136. Neno lako liwe sheria yako, ukiahidi tekeleza, usije na sababu, fanya kila unachopaswa kufanya kutimiza ahadi uliyotoa kwa wateja. Hakuna kitu kinachopoteza wateja kama ahadi hewa.
  137. Unapokuwa kwenye hali ya chini, labda hujisikii vizuri au umekwazika, usiruhusu hilo likae kwenye akili yako kwa muda mrefu litaharibu biashara yako. mara moja weka fikra za hamasa na matumaini ili uweze kuuza zaidi.
  138. Tenga muda wa mapumziko na kuwa mbali na biashara yako angalau mara moja kwa mwaka. Hiki ni kipindi unachotumia kutafakari zaidi kuhusu biashara yako, kuweka mipango ya ukuaji zaidi na kuboresha ndoto zako kubwa.
  139. Usikubali mazoea yajengeke ndani yako, dunia ya sasa inabadilika kwa kasi sana. kila siku jisukume kuwa bora zaidi ya jana.
  140. Unapofungua biashara kwenye eneo jipya, mwanzoni unaweza kuwa na wakati mgumu kuuza. Huu ni wakati ambao unapaswa kuutumia kuwajua wateja wako wapya na kujua eneo kwa ujumla.
  141. Uhalisia 101; kipato ndiyo damu ya biashara, angalia ni kipato gani unaingiza na kama biashara inaweza kujiendesha.
  142. Uhalisia 102; angalia ukubwa wa soko lako, ukubwa wa soko ni kipimo muhimu kwa ukuaji wa biashara yako. kama soko siyo kubwa juhudi nyingine zitashindwa.
  143. Uhalisia 103; angalia ni wapi unapoteza wateja wa biashara yako. Biashara nyingi huwa zinapoteza wateja au hazibadilishi wateja tarajiwa wengi kuwa wateja. Jua makosa yako wapi na uyarekebishe.
  144. Pima kile unachotaka kukisimamia na kukuza. Kama kitu huwezi kukipima, hutaweza kukikuza pia.
  145. Angalia vipimo vya ukuaji wa biashara, kama vile manunuzi, uhitaji wa wateja na ongezeko la wateja. Tumia vipimo hivi kukuza biashara zaidi.
  146. Jua kitu gani wateja wako wanathamini na pia jua jinsi unavyoweza kupima kuridhika kwao na kile wanachokipata kwako.
  147. Kila idara kwenye biashara yako lazima ijihusishe na mauzo na siyo watu wa mauzo pekee. Kazi ya mauzo ni ya kila mtu kwenye biashara yako, kila mtu kwa kitengo chake lazima ajue anahusikaje na kuongeza mauzo zaidi.
  148. Sema ASANTE mara nyingi uwezavyo, sema kwa mdogo, andika kama ujumbe. Mwambie mteja asante mara nyingi na atakuja kwako zaidi na zaidi.
  149. Kuwa mtu wa shukrani kwa kila kinachotokea kwenye maisha yako na utakuwa mtu unayewavutia wengine kuwa karibu na wewe.
  150. Kuwa na mtazamo wa utele na siyo wa uhaba. Usishindane kwa kuona labda mwingine akipata wewe umekosa, badala yake jua kuna vitu vya kumtosha kila mtu anayeweka juhudi kupata.
  151. Sherekea na toa zawadi kwa ushindi unaopatikana kwenye biashara. Pale timu yako inapofikia malengo mliyoweka, kuwa na tukio la kusherekea na hata kuwashukuru na kuwatambua watu kwa mchango wao.

Rafiki, hizo ndiyo mbinu 151, ni nyingi, chagua zile unazoweza kuanza kutumia sasa na nyingine za baadaye. Pia kwa zile zinazofanana zitumie kwa pamoja.

Ikuze biashara yako zaidi kwa kuongeza mauzo zaidi kwa mbinu hizi 151 za kuongeza mauzo zaidi kwenye biashara yako.

#2 MAKALA YA WIKI; TUMIA MAJUTO KUFANYA MAAMUZI SAHIHI.

Rafiki, mara nyingi tumekuwa tunafanya maamuzi yetu kwa kutumia kigezo cha kufanikiwa au kushindwa, furaha au kutokuwa na furaha. Lakini vigezo hivi vimekuwa havina uhalisia sana. Ni rahisi kujidanganya kwenye vigezo hivyo, ukafanya maamuzi ambayo ndani ya muda mfupi yanaonekana ni bora, lakini kwa muda mrefu yana madhara makubwa kwako.

Kama unataka kufanya maamuzi bora kwenye maisha yako, tumia kigezo cha majuto. Hiki ni kigezo ambacho kitakuwezesha kufanya maamuzi sahihi ambayo yanazingatia muda mfupi na muda mrefu.

Juma hili nilikuandalia makala ya jinsi ya kufanya maamuzi kwa kigezo cha majuto. Kama hukupata nafasi ya kusoma makala hiyo, unaweza kuisoma hapa; Hivi Ndivyo Unavyoweza Kutumia Majuto Kama Kipimo Cha Kufanya Maamuzi Bora Kwenye Maisha Yako.

Pia kwa wale ambao wanapata changamoto kwenye kupokea email ninazotuma kila siku, hasa za kipengele kipya cha DAKIKA MOJA, kuna maelekezo muhimu hapa ya kuhakikisha unapata email hizi. Unaweza kusoma maelekezo hayo hapa; Kama Unapata Shida Ya Kupokea Email Za Mafunzo Ninazotuma Soma Hapa.

#3 TUONGEE PESA; PESA SIYO MAKARATASI.

Nina hakika umewahi kusikia kauli hii, kauli kwamba fedha ni makaratasi tu. Ni kauli ambayo wanapenda kuitumia sana wale ambao hawana fedha, kama sehemu ya kuwanyanyasa wenye fedha. Wanaamini fedha ni makaratasi tu na waliozipata ni bahati yao.

Kadhalika wale wanaotafuta fedha kwa njia za mkato kama wizi, utapeli, ulaghai na njia nyinginezo, msingi wao kwenye fedha ni makaratasi. Na ndiyo maana wanafikiria suluhisho ni kutumia njia yoyote kuzipata, kitu ambacho kinaweza kutokea, lakini hakitatui tatizo la fedha walilonalo.

Kwa mfano kama fedha ingekuwa ni makaratasi, tungetegemea watu wanaoiba au kutapeli, wakishapata fedha mara moja basi waachane na njia hizo. Lakini huwa hawawezi kuziacha, kwa sababu fedha wanayopata haidumu muda mrefu.

Rafiki, fedha siyo makaratasi unayoyashika mkononi, fedha ni wazo, fedha ni thamani ambayo watu wapo tayari kubadilishana nayo.

Ukianza kuchukulia fedha kama wazo, kama thamani ya kubadilishana, ndipo unapoweza kujijengea msingi imara wa kukuwezesha kupata fedha mara zote. Kwa sababu ukishakuwa na msingi na ukaufuata, utapata matokeo bora mara zote.

Ukishajua fedha ni wazo na thamani, unakazana kuyaweka mawazo yako sawa kifedha, kisha unajiandaa kutoa thamani kubwa ili kuweza kulipwa kiasi kikubwa sana.

Mara zote hutakuwa na uhaba wa fedha wala kuwa na wasiwasi unapata wapi fedha, kwa sababu unajua fedha ni thamani, hivyo ukitoa thamani tegemea kupata fedha.

Unapofikiria kuhusu fedha, usiyafikirie makaratasi au namba unazosoma kwenye akaunti, badala yake fikiria thamani, kadiri unavyotoa thamani zaidi, ndivyo unavyotengeneza kipato zaidi.

#4 HUDUMA NINAZOTOA; ACHA KUJIDANGANYA KWENYE MUDA.

Kama kuna eneo moja ambalo kila mtu huwa anapenda kujidanganya basi ni kwenye muda. Utasikia kila mtu anasema nikipata muda nitafanya, kama vile kuna sehemu muda wa ziada umefichwa na mtu anaweza kuupata. Au kama vile kuna siku unaweza kupita njiani ukaokota muda wa ziada.

Rafiki, ukweli ni kwamba hakuna mtu anayeweza kupata muda, bali kila mtu anaweza kutengeneza muda.

Kwa sababu wote tunajua masaa 24 ya siku ndiyo kila mtu anayo, hivyo chochote unachotaka kufanya, lazima iwe kwenye masaa hayo 24.

Na mimi nimekuwa nakuambia hili, ndani ya masaa 24 una muda mwingi mno, mpaka mwingine umeamua kuupoteza wewe mwenyewe.

Yaani masaa 24 ni mengi sana kwako kiasi kwamba huwezi hata kuyasimamia vizuri, hivyo kuna dakika na hata masaa ya siku yanakuponyoka usijue muda huo umepotelea wapi.

Rafiki, kama unakazana na muda, kama una mengi ya kufanya kuliko muda unaoona unao, kama unatamani ungepata muda zaidi wa kufanya yale ambayo ni muhimu, basi jawabu lipo.

MASAA MAWILI YA ZIADA

Kwenye kitabu nilichoandika, PATA MASAA MAWILI YA ZIADA KILA SIKU, nimekushirikisha jinsi unavyoweza kuipangilia siku yako na yale unayofanya kila siku kiasi cha kujihakikishia una masaa mawili kwa ajili ya kufanya chochote unachotaka kufanya lakini unajiambia huna muda.

Ndani ya kitabu hiki, nimekuonesha kwa mifano kabisa wapi unayatengeneza masaa hayo mawili, na sijakuacha na masaa hayo tu, bali nimekushauri njia bora ya kuyatumia na kuyawekeza ili yakupe matokeo bora zaidi kwa baadaye.

Kama bado hujasoma kitabu hiki, kipate na uanze kukisoma leo, ili uweze kutawala muda wako na kufanya yale ambayo ni muhimu kwako.

Kitabu ni softcopy, na kinatumwa kwa email, gharama yake ni tsh elfu 5. Kukipata tuma fedha pamoja na email kwenda namba 0717 396 253 au 0755 953 887. Usikubali kuacha muda wako unaendelea kupotea huku ukitamani ungepata zaidi. Tayari unao muda zaidi, ni wewe kujua na kuanza kuutumia.

#5 TAFAKARI YA KUFIKIRISHA; AMINI KWENYE UZURI WA NDOTO ZAKO.

“The future belongs to those who believe in the beauty of their dreams.” – Eleanor Roosevelt

Kila mtu ana ndoto kubwa za maisha yake, na kama unataka kuamini hili, mfuate mtoto mdogo, kati ya miaka 5 mpaka miaka 9 na muulize ukiwa mkubwa unataka kuwa nani, na bila ya wasiwasi, bila ya mashaka yoyote, atakujibu anataka kuwa nani.

Lakini rudi kwa mtoto huyo huyo miaka 10 baadaye, na muulize ukitaka kuwa mkubwa unataka kuwa nani, na utashangaa mabadiliko yatakayokuwa yametokea. Kwanza hataweza kukujibu kwa kujiamini kama alivyofanya miaka kumi iliyopita. Pili majibu yake yatakuwa na wasiwasi na hofu, yatakuwa ni majibu ya kutegemea kama mambo yataenda vizuri.

Nini kimetokea ndani ya miaka hii kumi? Jibu ni hili, jamii inakuwa imeondoa ile imani thabiti na isiyovunjika iliyokuwa ndani ya mtoto.

Watu wengi hawaamini kwenye uzuri wa ndoto zao, hawana imani thabiti kwamba lazima wafikie ndoto hizo. Badala yake wanachukulia kama ni kitu ambacho wangefurahi kama wangekipata.

Rafiki, kama huamini kwenye uzuri wa ndoto zako, kama huamini ndiyo kitu bora kabisa kinachoweza kutokea kwenye maisha yako, kama huamini kwamba unaweza kufikia ndoto hizo licha ya changamoto, hutaweza kuzifikia. Kwa sababu safari haitakuwa rahisi, na wale wenye imani kubwa ndiyo watabaki kwenye safari hiyo, huku wenye imani haba wakipotea haraka sana.

Amini kwenye uzuri wa ndoto zako, amini unaweza kufikia ndoto hizo na chukua hatua kama vile hakuna kinachoweza kukuzuia wewe kufikia ndoto hizo, kwa sababu ni kweli hakuna cha kukuzuia.

Rafiki, hizi ndizo tano za juma namba 47, juma bora ambalo tulikuwa nalo. Tukatumie tano hizi za juma, na yale tuliyojifunza kwenye juma hili linaloisha, ili juma namba 48 likawe juma bora zaidi kwetu. Kumbuka kujifunza vitu vipya na kujaribu vitu vipya kila juma.

Makala hii imeandikwa na Kocha Dr Makirita Amani.

Dr. Makirita ni Daktari wa binadamu, Kocha wa mafanikio, Mwandishi na Mjasiriamali.

Dr. Makirita anaendesha mafunzo ya mafanikio kwa wale waliojitoa hasa kufanikiwa kupitia program ya KISIMA CHA MAARIFA.

Kama bado hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA, tuma sasa ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa njia ya wasap namba 0717 396 253 (tumia wasap tu)

Kupata huduma nyingine za ukocha tembelea www.amkamtanzania.com/kocha

Kupata vitabu vizuri vya kusoma tembelea www.amkamtanzania.com/vitabu