Ni siku nyingine nzuri sana kwetu wanamafanikio,
Ni nafasi bora na ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari UPI MCHANGO WAKO?
Rafiki, kwa changamoto yoyote unayokutana nayo kwenye maisha yako, kuna mchango fulani ambao wewe unakuwa umeweka.
Hata kama makosa ni ya mtu mwingine na yako wazi kabisa, bado kuna namna wewe unakuwa umechangia mpaka ukutane na changamoto hiyo.
Hata kama kila mtu anaona wazi kwamba huna makosa, hata kama kila mtu anasema umeonewa au ni bahati mbaya kwako, usikwepe jukumu la mchango ulioweka kwenye matatizo uliyokutana nayo.
Kwa sababu siyo kila mtu anakutana na matatizo ambayo wewe umekutana nayo, hivyo kuna namna wewe mwenyewe umechangia.
Rafiki, hili ni gumu sana kuelewa na kukubaliana nalo, hasa kwa tabia zetu za kupenda kulaumu wengine na kulalamika.
Lakini kama utajipa muda wa kutafakari, utaona umechangiaje kwenye tatizo lolote ulilopo na ukijua mchango wako, wakati mwingine utakuwa makini zaidi.
Najua ni rahisi mtu mtu kufikiria, lakini wakati mwingine vitu vinatokea nje ya uwezo wetu na tunajikuta tayari tupo kwenye matatizo, hapo tumechangiaje?
Kwanza lazima ujiulize je ni kila mtu ameingia kwenye matatizo kama uliyonayo wewe?
Kama siyo basi jua wewe kuna namna umetengeneza au kukaribisha matatizo uliyokutana nayo.
Kwa mfano ulikuwa unavuka barabara na ghafla gari inakuja kwa kasi na kukugonga, je umechangiaje hapo?
Zipo njia nyingi ambazo umechangia, labda ulikosa umakini fulani wakati unavuka, huenda ungekuwa na subira zaidi usingekutana na changamoto hiyo.
Huenda pia umekaa ndani ya nyumba na radi ikakupiga, hapo umechangiaje?
Kwa namna nyingi mno, huenda hukupaswa kuwa ndani ya nyumba kwa wakati huo, huenda kuna miti imezunguka nyumba hiyo ambayo inavutia radi, ambapo kama ungekuwa umeikata au kupunguza, isingeweza kuvutia radi.
Rafiki, tunapojifunza kuangalia mchango wetu kwenye kila kinachotutokea, tunajiweka kwenye nafasi ya kuwa bora zaidi, kuliko tunapoishia kulaumu wengine pekee.
Usikubali kirahisi kwamba wewe umeonewa au hukuwa na namna ya kuzuia au kuepuka matatizo uliyokuwa nayo.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kujipima na kujua mchango ambao umeweka kwenye matatizo yoyote unayokutana nayo kwenye maisha yako, ili uweze kuwa na maisha bora zaidi.
#Fanya #HakunaSababu #NiLeoTu #IngiaMzimaMzima #AnzaNaHatuaMoja #MafanikioNiHakiYako #NidhamuMsingi #WhatEverItTakes #WachaManenoWekaKazi #SkinInTheGame #OwnTheDayOwnYourLife #UsileteSababuLetaMatokeo #MudaNiSasa
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha