Kitu kimoja ninachojifunza kila siku kuhusu mafanikio ni kwamba usipokuwa katili kwako wewe binafsi, mafanikio yatakuwa magumu sana.
Na ninasema katili bila ya kulainisha kauli kwa sababu watu wengi wamekuwa wanajidanganya sana kuhusu mafanikio.
Wengi wamekuwa wakiamini kwamba kama wakishakuwa na mtazamo chanya, na wakaamini mambo makubwa yanakwenda kutokea basi yatatokea.
Rafiki, hiyo ni asilimia moja ya mafanikio, asilimia 99 ipo kwenye kazi, kazi ambayo ni ngumu na ambapo utakutana na ugumu wa kila aina.
Sasa nasema lazima uwe katili kwa sababu kuna wakati mwili wako utakulaghai ufanye kitu fulani ambacho ni kinyume na kule unakokwenda, au unakulaghai usifanye kitu fulani ambacho ni muhimu, lakini kitu hicho kinaumiza mwili.
Kama hutaweza kuukatalia mwili wako pale unapotafuta urahisi, hutaweza kupiga hatua za mafanikio.
Unapaswa kujiwekea viwango vya hali ya juu sana, na kisha kuvifuata bila ya kujipa sababu. Unaposhindwa kufikia viwango hivyo jipe adhabu kali sana, usijionee huruma. Fanya kila unachopanga kufanya kwa wakati ambao umepanga kufanya na usipoteze hata dakika moja kwenye mambo yasiyo muhimu.
Kila wakati jifuatilie kujua kama unafanya kweli, na pale unapotoroka na kwenda kwenye mambo rahisi, jikamate mapema na jipe adhabu ili wakati mwingine usirudie.
Rafiki, kama mpaka hapa unasema huu ni ukatili na haufai kwenye maisha basi jua hujachagua maisha ya mafanikio.
Kwa upande wa pili, kwa wengine, usiwakazie kama unavyojikazia wewe, waache kwenye viwango vyao na jipe sababu pale wanaposhindwa. Wape nafasi ya kushindwa na usitegemee wawe na viwango vya juu kama vya kwako.
Kuwa mgumu sana kwako mwenyewe, lakini kuwa na wepesi kwa wengine.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,