Kila siku muda unazidi kuwa mgumu na adimu kupatikana kwa sababu masaa ya siku ni yale yale 24 na siku za juma ni zile zile 7, lakini kila siku vitu vya kufanya vinaongezeka.

Sasa vya kufanya vinapoongezeka, wakati muda ni ule ule, kinachotokea ni muda unakuwa wa uhaba na watu kupatwa na msongo wa mawazo.

Kadiri watu wanavyokazana kufanya mambo mengi zaidi kwenye muda mfupi walionao, ndivyo wanavyoshindwa kukamilisha yale muhimu na hilo linawaletea msongo zaidi.

Hivyo kujaribu kufanya mambo mengi kwa muda mfupi ulionao, ni moja ya sababu za muda kuwa adimu zaidi, moja ya sababu zinazopelekea mtu kuchoka sana wakati hakuna kikubwa ambacho amekamilisha.

Hebu fikiria siku yako na maisha yako yangekuwaje kama kwa siku ungekuwa unafanya mambo matatu pekee. Fikiria jinsi siku yako ingeenda kama usingekuwa unahitaji kubonyeza simu yako kila baada ya muda mfupi, kutaka kujua nini kinaendelea au wengine wanafanya nini.

Kadiri unavyofanya machache na muhimu kwenye muda ulionao, ndivyo ufanisi wako na uzalishaji unavyokuwa mzuri na mkubwa na ndivyo unavyofanikiwa zaidi.

Lakini ukishaanza kukazana kufanya mengi, kutaka kufanya kila kinachojitokeza mbele yako, unajikuta umegusa vitu vingi na hakuna ulichokamilisha, hilo linakuchosha sana na hakuna uzalishaji wowote ambao umekuwa umefanya.

Ndiyo maana hatua ya kwanza kabisa kwenye kudhibiti na kusimamia vizuri muda wako ni kuweka kwanza vipaumbele vyako. Anza na mambo yapi ni muhimu zaidi kwako, anza na yale tu ambayo yana mchango kufika kule unakotaka kufika.

Kila unapoianza siku yako chagua majukumu matatu muhimu sana ambayo utayafanyia kazi siku hiyo. Na yapange kulingana na umuhimu wake, ukianza na yale ambayo ni muhimu zaidi. Kisha tekeleza majukumu hayo kwanza kwenye siku yako. Anza na jukumu namba moja na usifanye kitu kingine kabla hujakamilisha jukumu hilo namba moja.

Na kama kuna majukumu yenye uzito sawa, unaweza kutenga muda wa kufanya kila jukumu na ndani ya muda huo uliotenga, fanya jukumu hilo tu na siyo kitu kingine.

Wakati wa kutekeleza majukumu muhimu kwako, simu ikae mbali au iwe kwenye utulivu kabisa kiasi kwamba haigeuki kuwa kelele kwako. Usiingie tamaa ya kuacha unachofanya kwa sababu unataka kuangalia nini kinaendelea. Ukishapanga cha kufanya, hicho ndiyo kipaumbele chako, fanya hicho pekee.

Ukiweza kujenga utaratibu wa aina hii kwenye muda wako, utaanza kuona una muda mwingi wa kufanya yale ambayo ni muhimu kwako. Wakati wengine wanalalamika muda unapotelea wapi, wewe unakuwa unautumia vizuri kwa yale ambayo ni muhimu zaidi kwako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha