Kuna wakati unajikuta unafanya maamuzi fulani kwenye maisha yako, na huwezi kusema kwa nini umeyafanya. Unajikuta umeyafanya moja kwa moja bila hata ya kufikiri kwa kina. Yaani ni kama akili yako ilishakariri namna fulani unavyofanya mambo yako na kuendeleza hivyo.

Mazingira yetu yanaathiri sana maamuzi tunayoyafanya, tukishayazoea mazingira tuliyopo, tunaanza kujikuta tunafanya maamuzi ambayo hatujui hata kwa nini tunafanya. Maamuzi yanajitokeza yenyewe na sisi tunatekeleza tu.

Mazingira yetu yanaanza na wale ambao wanatuzunguka, maamuzi mengi tunayofanya yanatokana na aina ya watu ambao wanatuzunguka. Upo usemi maarufu kwamba wewe ni wastani wa watu watano wanaokuzunguka. Kwamba hata kama sijui tabia yoyote kuhusu wewe, ukiniambia watu wako watano wa karibu nikaangalia tabia zako, nitaweza kutabiri tabia zako kwa usahihi wa asilimia 90.

Kama unazungukwa na watu ambao hawajali, moja kwa moja unajikuta na wewe hujali. Kama umezungukwa na watu ambao hawayafurahii maisha, na wewe hutayafurahia maisha. Kama waliokuzunguka wamekata tamaa, na wewe lazima utakata tamaa.

Wale wanaotuzunguka wana nguvu kubwa sana kwenye aina ya maamuzi tunayofanya, na kwa pamoja hao ndiyo wanatawala maamuzi mengi ambayo mtu anayafanya.

Kitu kingine kwenye mazingira kinachoathiri maamuzi yetu ni kile kinachoingia kwenye akili na fikra zetu. Kila aina ya habari unayoipata, kila maarifa unayoyapata, kila kipindi cha tv au redio unachofuatilia, kila mtandao wa kijamii unaotumia, unahusika kwenye kushawishi aina ya maamuzi unayofanya.

Kila ambacho kinaingia kwenye akili yako kwa wingi ndiyo kinachotoka kwenye maisha yako kama maamuzi. Kama unatumia muda mwingi kufuatilia habari hasi, maamuzi yako mengi utayafanya kwa kufikiria hasi. Na kama muda wote akili yako inaingiza habari chanya, utayafanya maamuzi yako kwa kufikiria chanya.

Rafiki, huwa tunafikiri kamba tupo huru, kwamba maisha tunayoishi tumeyachagua wenyewe. Lakini tunajidanganya, hatupo huru kama tunavyofikiri. Maisha tunayoishi siyo maamuzi yetu kama tunavyodhani. Ushawishi wa nje ni mkubwa sana kwenye maamuzi tunayoyafanya kwenye maisha yetu.

Ili kuweza kufanya maamuzi sahihi kwako na maamuzi bora, lazima kwanza ujue udhaifu huu ambao tunao, udhaifu wa maamuzi yako kuathiriwa na mazingira. Ukishajua hilo, sasa jukumu lako linakuwa kutengeneza mazingira ambayo yatakuwa na athari nzuri kwa maamuzi utakayofanya.

Kwa mfano kwa kugundua wanaokuzunguka wana madhara kwenye maamuzi yako, unachagua kuzungukwa na watu chanya, watu waliofanikiwa au wanaoelekea kwenye mafanikio, watu wanaoamini inawezekana na hawajakata tamaa. Pia kwa kuelewa uzito wa kile unachoruhusu kiingie kwenye fikra zako, unazilinda sana fikra zako, unaondoa kila fikra hasi na kujaza akili yako fikra chanya za kuwezekana.

Usikubali mazingira yakupeleke bila ya mpango, badala yake yapangilie mazingira ili uweze kufanya maamuzi bora zaidi kwako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha