Hongera sana mwanamafanikio kwa nafasi hii nyingine nzuri ambayo tumeipata leo.
Ni fursa bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari WATU WASIO NA MUDA…
Watu wasio na muda, wapo makaburini, wameshakufa na hawana tena maisha.
Hawa ndiyo wakituambia hawana muda, tunaweza kuwaelewa, kwa sababu hakuna tena wanachoweza kufanya na maisha yao.

Lakini pale mtu aliyepo hai, mtu anayepumua na mwenye afya njema anapokuambia hana muda, hapo ndipo unajiuliza mtu huyu anamaanisha nini.
Kwa sababu kila aliye hai ana muda.
Hakuna mtu aliyepunjwa haya masaa 24 ya kila siku.

Tatizo letu siyo muda, tatizo letu ni matumizi ya muda tulionao.
Tunatumia hovyo sana muda wowote ambao tunao na hili linatugharimu sana.
Tunafanya chochote tunachojisikia na tunawaruhusu wengine wajichukulie muda wetu kwa namna wanavyotaka wao wenyewe.
Tunakimbizana na vitu ambavyo havina mchango kwa sisi kuwa na maisha bora, vinachukua muda wetu mwingi na tunabaki hatuna muda wa kufanya yale muhimu.

Kila unapojiambia huna muda, chukua kalamu na karatasi kisha orodhesha kila ulichofanya kwenye siku yako iliyopita. Orodhesha kila kitu hata kama ni kidogo kiasi gani.
Baada ya kuorodhesha kila kitu, weka alama ya vema mbele ya yale ambayo yanakupeleka kwenye mafanikio.
Kisha pitia tena orodha hiyo, angalia mambo mangapi yana alama ya vema kisha ona jinsi muda mwingi umeupoteza kwa yasiyo muhimu.
Baada ya zoezi hili, fanya yale yenye vema pekee, hayo mengine achana nayo mara moja.

Ukweli ni kwamba muda unao, tena wa kutosha, ni wewe tu umeamua kuupoteza muda huo kwa yale ambayo siyo muhimu kwako.
Jua unakopotezea muda wako na uanze kushika hatamu ya maisha yako.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kulinda muda wako usipotee kwa kuutumia kwa yale muhimu pekee.
#Fanya #HakunaSababu #NiLeoTu #IngiaMzimaMzima #AnzaNaHatuaMoja #MafanikioNiHakiYako #NidhamuMsingi #WhatEverItTakes #WachaManenoWekaKazi #SkinInTheGame #OwnTheDayOwnYourLife #UsileteSababuLetaMatokeo #MudaNiSasa

Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha