“When a man with money meets a man with experience, the man with the experience ends up with the money, and the man with the money ends up with the experience.”

Siku mpya,
Siku nzuri na ya kipekee sana kwetu.
Tumepata nafasi nyingine bora sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari FEDHA NA UZOEFU….
Ili kufikia utajiri na uhuru wa kifedha, unahitaji vitu viwili muhimu, FEDHA NA UZOEFU.
Kuwa na fedha pekee bila ya kuwa na uzoefu, unaishia kupoteza fedha hizo.
Lakini kuwa na uzoefu ni njia bora ya kuweza kuongeza zaidi fedha zako.

Watu wengi wamekuwa wanatamani sana kupata fedha nyingi, ila hawana uzoefu kwenye kushika fedha nyingi kwa wakati mmoja.
Hivyo inapotokea wamepata fedha nyingi kwa wakati mmoja, ndipo matatizo makubwa huanza.
Wengi hupoteza fedha zote hizo ili tu kupata uzoefu.

Tunaona haya kwa wale wanaopata fedha nyingi kwa haraka, labda kushinda bahati nasibu, kupokea urithi au kupata mafao.
Wengi wanapokuwa na fedha hizi nyingi, lakini hawana uzoefu, huwa wanajiaminisha wanaweza kufanya chochote wanachotaka.
Hivyo wanaanza kukazana kufanya vitu vingi ambavyo hawajawahi kufanya na kinachotokea ni wanapoteza fedha walizonazo.

Mtu mwenye fedha anapokutana na mtu mwenye uzoefu, mwenye uzoefu anaishia kuwa na fedha na mwenye fedha anaishia kuwa na uzoefu.
Hapa ndipo wenye fedha lakini hawana uzoefu wanapopotezea fedha zao nyingi ili kupata uzoefu, kwa kujaribu vitu ambavyo hawajawahi kufanya wala hawajui vinafanywaje.

Ili kuepuka kupoteza fedha nyingi unazoweza kupata, weka juhudi kwenye kujijengea uzoefu wakati una fedha ndogo ndogo.
Anza kujijengea uzoefu wa uwekezaji kwa fedha ndogo ndogo ulizonazo.
Jijengee uzoefu wa biashara kwa fedha ndogo ndogo unazopata. Ili siku unapokutana na fedha nyingi, huanzi kubabaika ufanye nazo nini, badala yake unaweka kwenye yale maeneo ambayo ulishayaanza.

Anza kutengeneza uzoefu wako wa kifedha kwenye fedha ndogo ndogo na utaepuka sana kupoteza fedha nyingi kupata uzoefu.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kujijengea uzoefu wa kifedha kwa kila fedha ndogo inayopita kwenye mikono yako.
#Fanya #HakunaSababu #NiLeoTu #IngiaMzimaMzima #AnzaNaHatuaMoja #MafanikioNiHakiYako #NidhamuMsingi #WhatEverItTakes #WachaManenoWekaKazi #SkinInTheGame #OwnTheDayOwnYourLife #UsileteSababuLetaMatokeo #MudaNiSasa

Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha