Watu wengi walioajiriwa huwa wana njia moja tu ya kuongeza kipato chao kupitia ajira waliyonayo. Njia hiyo ni kuomba kuongezewa mshahara. Na pale maombi yanapokataliwa, basi wanaanza kufanya kazi chini ya kiwango, kwa sababu wanaona hakuna haja ya kufanya zaidi.
Njia hiyo iliyozoeleka na wengi ni njia mbovu sana na imewafanya wengi kuzidi kukwama kwenye kipato walichokuwa nacho.
Rafiki, hakuna mwajiri yeyote anayeweza kukuongezea kipato kwa sababu tu umetaka ongezeko. Na pale unapopunguza kiwango chako cha kazi kwa sababu mshahara hauongezwi ndiyo kabisa unazidi kupunguza nafasi ya wewe kuongezewa kipato.
Njia bora ya kuongeza kipato kwenye ajira ni kujifunza kitu kipya kinachoongeza thamani kwenye kazi yako, kisha ukawa bora sana kwenye kitu hicho.
Unapaswa kupata ujuzi mpya, maarifa mapya ambayo yanaongeza thamani zaidi kwenye kazi unayofanya, kisha kutumia maarifa hayo kufanya zaidi. Kadiri unavyofanya zaidi na kuzalisha zaidi, mwajiri wako ataona tofauti yako na wengine na atakuwa tayari kuongeza mshahara wako hata kabla hujaomba.
Na kama utafanya hivyo lakini mwajiri wako asijali, basi jua kuna wengine wataona thamani kubwa unayotoa na watakuwa tayari kukupa nafasi nzuri sana kwenye maeneo mengine.
Rafiki, hufanyi kazi kwa ajili ya mwajiri wako au mtu mwingine yeyote, unafanya kazi kwa ajili yako mwenyewe, hivyo kazana kuwa bora zaidi kila siku, kwa sababu hilo ndiyo litakuletea wewe mafanikio makubwa.
Usisubiri mpaka mwajiri wako akupe mafunzo ndiyo ujifunze, badala yake jiongeze kwa kuwa na kitu cha tofauti na kuweza kutoa thamani kubwa zaidi kwenye siku yako.
Ni kanuni ya asili kwamba wale wanaotoa zaidi lazima pia wapokee zaidi. Hivyo usijali kwamba kwa nini ufanye sana wakati unalipwa kidogo. Mpaka sasa unalipwa kidogo kwa sababu unafanya kidogo. Hivyo ili kulipwa zaidi, lazima ufanye zaidi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,