Watu wamekuwa wakibishana ni namna gani unapaswa kufanya kazi, na mabishano huwa yamekuwa kwenye maeneo mawili, nguvu na akili.
Wapo wanaosema unapaswa kufanya kazi kwa akili zaidi na siyo nguvu zaidi. Na wapo wanaoamini kwamba kazi bora ni ile inayofanywa kwa akili zaidi na nguvu zaidi.
Wale wanaosema wanatumia akili zaidi na siyo nguvu, huwa hawafanyi makubwa, kwa kuwa wanaishia kutoa mawazo mazuri lakini hawawi mfano kwenye ufanyaji.
Wale wanaoweka nguvu zaidi na akili zaidi kwenye kazi zao wanapiga hatua zaidi, kwa sababu hawaishii tu kutoa mawazo mazuri, bali pia wanaonesha kwa mfano. Hivyo hata kama wana watu wanaowasaidia, wanaona namna gani vitu vinapaswa kufanywa.
Lakini njia hizo mbili pekee hazitoshi kumpeleka mtu kwenye mafanikio makubwa. Nguvu na akili pekee hazikutoshi kujitofautisha na wengine ambao nao wanatumia nguvu na akili.
Kipo kitu cha tatu unachopaswa kuweka kwenye kazi zako baada ya nguvu na akili, kitu hicho ni muda.
Kwa hiyo sasa, unapaswa kufanya kazi zako kwa nguvu zaidi, akili zaidi na muda zaidi. Hata uweke nguvu na akili kiasi gani, kama unafanya kwa muda ambao wengine wanafanya, utaishia kupata matokeo ambayo siyo ya tofauti sana na wengine wanavyopata.
Lakini kama utaweka muda zaidi, kama utaanza mapema na kuchelewa kumaliza, huku ukiweka nguvu zaidi na akili zaidi, lazima utapata matokeo makubwa sana.
Elon Musk, mjasiriamali bilionea na mgunduzi anasema kama wengine wanafanya kazi masaa 40 kwa wiki, na wewe ukaamua kufanya kazi masaa 100 kwa wiki, utakuwa na uzalishaji mara mbili ya walionao wengine.
Huu ndiyo umuhimu wa kuweka muda zaidi kwenye kazi zako, kwa sababu unapata nafasi ya kuzalisha zaidi na kupiga hatua zaidi kwenye maisha yako.
Hivyo kila unapoifikiria kazi yako, fikiria vitu vitatu, akili zaidi, nguvu zaidi na muda zaidi. Asiwepo yeyote ambaye anaweka vitu hivyo zaidi kuliko wewe. Na siyo kwamba unafanya ili kushindana, bali unafanya ili kupiga hatua kubwa zaidi kwenye maisha yako.
Vitu hivyo vitatu vipo ndani ya uwezo wako, acha uvivu na weka kazi kwa namba inavyopaswa kuweka na utayavuna matunda ya kazi unayoweka.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,