Hongera sana mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari VITU VISIVYOLAZIMISHWA…
Kuna vitu kwenye maisha ambavyo huwezi kuvipata kwa kulazimisha,
Hivi ni vitu muhimu ambavyo unavihitaji sana kwa mafanikio yako.
Ni vitu vinavyohusisha mahusiano yetu na wengine.

Huwezi kulazimisha upendo, kama inabidi umlazimishe au kumshawishi mtu akubali kwamba anakupenda, mtu huyo hakupendi. Kadiri unavyolazimisha upendo ndivyo unavyozidi kuubomoa.
Njia pekee ya kumfanya mtu akupende ni kwa wewe kuanza kumpenda.
Na siyo kumpenda kwa sababu unataka alipe kwa kukupenda,
Bali unampenda kwa sababu ndiyo maisha uliyochagua wewe, maisha ya upendo kwa wengine.
Kadiri unavyowapenda wengine bila ya masharti yoyote, ndivyo nao wanavyokupenda wewe bila ya masharti au kulazimishwa, inatokea tu.

Huwezi kulazimisha heshima, kama inabidi ulazimishe au kuwashawishi wengine kwamba wanapaswa kukuheshimu, hawakuheshimu.
Kadiri unavyolazimisha heshima ndivyo unavyozidi kuipoteza.
Njia bora ya kuwafanya watu wakuheshimu ni kwa wewe kuanza kuwaheshimu wao kwanza.
Mheshimu kila mtu kwa sababu ya utu wake na siyo kwa sababu ya cheo au nafasi aliyonayo.
Binadamu ni viumbe ambao huwa tunajikuta tunarudisha kile ambacho wengine wanatupatia, hivyo unapoanza kuwaheshimu wengine, na wao pia wanakuheshimu wewe.
Ni kitu ambacho hakilazimishwi, wala hakitegwi, kinatokea kama sehemu ya maisha unayochagua kuyaishi.

Rafiki, chochote unachotaka kwenye maisha yako, anza kwa kukitoa kwa wengine kwanza, anza kukifanya kuwa sehemu ya maisha yako ya kila siku. Kisha dunia itakujibu kwa kurudisha kile unachotoa.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kukaribisha unachotaka kwa kuwa na kufanya na siyo kwa kulazimisha.
#Fanya #HakunaSababu #NiLeoTu #IngiaMzimaMzima #AnzaNaHatuaMoja #MafanikioNiHakiYako #NidhamuMsingi #WhatEverItTakes #WachaManenoWekaKazi #SkinInTheGame #OwnTheDayOwnYourLife #UsileteSababuLetaMatokeo #MudaNiSasa

Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha