Kama unasubiri usiwe na hofu kabisa ndiyo uweze kufanya unachotaka kufanya, hutaweza kupiga hatua yoyote kwenye maisha yako.

Maisha yetu tangu tunapozaliwa, tumezungukwa na hofu, na kinachotuwezesha kupiga hatua siyo kusubiri hofu iondoke, bali kuwa na ujasiri wa kuchukua hatua licha ya hofu kuwepo.

Kitendo tu cha kuzaliwa kimejawa na hofu, lakini tunaishinda hofu hiyo na kuingia duniani, japo kwa kilio kikubwa kutokana na mazingira kubadilika.

Kitendo cha kuanza kutembea mwenyewe kimejawa na hofu, na utaanguka mara kadhaa kabla hujaweza kusimama na kutembea mwenyewe.

Kila kitu kipya ambacho umewahi kujaribu kufanya kwenye maisha yako, hofu ilikuwa juu, lakini ulipoanza kufanya hofu ilianza kuondoka. Fikiria siku ya kwanza kuendesha chombo chochote, iwe ni baiskeli, pikipiki au hata gari, ulikuwa na hofu kubwa sana, lakini baada ya kuendelea kuendesha, hofu ile inaondoka kabisa.

Jawabu la hofu ni ujasiri, na ujasiri ni kuchukua hatua licha ya kutokuwa na uhakika mbele kuna nini, ujasiri ni kuikubali hofu kisha kuikabili, kutokukubali iwe kikwazo kwako.

Ukitaka kuanza maisha mapya hofu itakujaa, kwa sababu umeshazoea maisha ya zamani na huna uhakika na maisha hayo mapya.

Ukitaka kuanza biashara hofu itakutawala, kwa sababu huna uhakika kama itakwenda vizuri.

Ukitaka kuondoka kwenye ajira uliyonayo hofu itakutawala, kwa sababu utaona unaondoka kwenye uhakika na kwenda kusiko na uhakika.

Hakuna hata dakika moja ambayo hofu itakuacha ufanye mambo yako kama unavyotaka. Hivyo usijidanganye na kusubiri hofu iondoke au uwe na uhakika. Hakuna kitu chochote unachoweza kuwa na uhakika nacho kwenye maisha.

Hatua pekee ya kuishinda hofu ni kufanya, kuchukua hatua.

Kabla ya kufanya unakuwa unafikiria matokeo mabaya kabisa yatatokea, lakini unapoanza kufanya, hata kama hupati unachotaka, unagundua matokeo yanayotekea siyo mabaya kama ulivyokuwa unadhania, na hili linakupa ahueni na kukufanya upuuze hofu uliyonayo.

Kuwa jasiri rafiki, kuwa jasiri kwa kuchukua hatua licha ya kuwa na hofu. Kama kitu ni muhimu sana kwako, basi kifanye, kikifanikiwa utapata unachotaka na kama kikishindwa utajifunza. Ila kama hutafanya chochote, utabaki pale ulipo sasa na hutajifunza chochote kipya kwenye maisha yako.

Ujasiri unatoka ndani yako, ujasiri unakuja pale unapoweza kujiamini na kujitegemea, kwa kujua ndani yako upo uwezo mkubwa wa kukuwezesha kukabiliana na chochote utakachokutana nacho. Tumia nguvu hii vizuri ili kuweza kupiga hatua kubwa kwenye maisha yako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha