“The things you run from are inside you”

Hongera mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari UNACHOKIKIMBIA KIPO NDANI YAKO…
Huenda haya yalishakutokea au umeona yanatokea kwa wengine;

👉🏼Unaondoka kwenye kazi fulani kwa sababu unaona haikufai au haikulipi, unaenda kwenye kazi nyingine ambayo unaamini inakufaanna kukulipa, lakini baada ya muda mambo kwenye kazi mpya yanakuwa kama kwenye kazi ya zamani.

👉🏼Unavunja mahusiano na mtu uliyekuwa naye kwa sababu kuna mambo kwake hukuyapenda au hamkuendana, unaanzisha mahusiano mapya ambayo unafikiri yatakuwa mazuri, lakini baada ya muda, yale yaliyokuwa yanakusumbua kwenye mahusiano ya mwanzo, yanaanza kukusumbua tena kwenye mahusiano mapya.

👉🏼Unafanya biashara ambayo unaona inakusumbua, haikulipi, wakati huo huo unaona kuna biashara nyingine nzuri na watu wananufaika nayo. Unaacha biashara uliyokuwa unafanya na kwenda kwenye biashara hiyo mpya, muda siyo mrefu yale matatizo yaliyokuwa yanakusumbua kwenye biashara uliyotoka, unaanza kuyaona kwenye biashara mpya unayofanya.

Ipo mifano mingi rafiki ya namna unavyotoka eneo moja linalokusumbua, unaenda eneo jingine ukiwa na matumaini usumbufu hautakuwepo, lakini baada ya muda unagundia usumbufu umekufuata kule pia.

Ukweli ni kwamba, chochote unachojaribu kukikimbia, kipo ndani yako.
Hivyo popote unapoenda, unapeleka kitu hicho na ndiyo maana matatizo yamekuwa yanawafuata watu popote wanapokwenda.
Ni sawa na mbwa anayekimbiza mkia wake mwenyewe. Hata akiweka kasi kiasi gani, bado hataweza kuukamata, kwa sababu upo ndani yake.

Rafiki, kama kuna kitu kinakusumbua kwenye maisha yako, kabla hujatafuta jawabu la nje, anza kwanza kutafuta jawabu la ndani. Kabla hujachukua hatua kwa nje, anza kuchukua hatua kwa ndani.
Angalia ni nini kilichopo ndani yako ambacho kinavutia matatizo unayokutana nayo.

Je ni namna unavyoamini?
Je ni hasira na kinyongo imebeba ndani yako?
Je unajiona hufai na hustahili?
Anza kuchimba ndani na utaona kila tatizo unalokutana nalo kwenye maisha yako, linaanzia ndani yako.
Na ukishatatua tatizo lililopo ndani, nje kunakaa sawa kwenyewe.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuangalia ndani yako na kuona vyanzo vya matatizo uliyonayo ili kuyatatua na siyo kuyakimbia.
#Fanya #HakunaSababu #NiLeoTu #IngiaMzimaMzima #AnzaNaHatuaMoja #MafanikioNiHakiYako #NidhamuMsingi #WhatEverItTakes #WachaManenoWekaKazi #SkinInTheGame #OwnTheDayOwnYourLife #UsileteSababuLetaMatokeo #MudaNiSasa

Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha