Wote tunajua ya kwamba ili kufanikiwa lazima uweze kuitofautisha na wengine.
Kufanya kile ambacho kila mtu anafanya, kwa namna ile ile ambayo wanafanya, kutakupelekea kupata matokeo ambayo wengine wanafanya.
Sasa kama hayo ndiyo matokeo ambayo umekuwa unayapata na hayajakufikisha unakotaka kufika, unahitaji kuanza kufanya tofauti.
Na tofauti unayopaswa kufanya ni kufanya kwa namna ambayo wewe utasimama tofauti kabisa na wengine, wewe utaonekana tofauti na wengine, na wale unaowalenga watakuona wewe kabla hawajawaona wengine.
Sasa watu wamekuwa wanatumia njia ya mkato kutengeneza utofauti huo, na njia rahisi ya mkato imekuwa kupiga kelele zaidi ya wengine.
Kwa kuwa kila mtu anapiga kelele, basi watu hufikiri kama wataweza kupiga kelele zaidi ya wengine, watasikika na kuonekana tofauti. Lakini ukweli ni kwamba kwenye kelele, hakuna kelele inayosikika zaidi ya nyingine. Kelele zinaishia kuwa kelele na watu wanajifunza kuzipuuza.
Hatua ya kwanza ya kujitofautisha na wengine, ni kuangalia nini watu wanapendelea zaidi kufanya, kisha fanya kinyume na wao.
Kwa mfano watu wengi wanapenda kulalamika, basi wewe usiwe mtu wa kulalamika kabisa, kuwa mtu wa kuchukua majukumu na kuyafanyia kazi. Usiwe na chochote na cha kulalamikia. Mambo yanapokwenda tofauti na ulivyotegemea unachukulia hilo kama jukumu lako na kuchukua hatua za tofauti.
Pia watu wengi wamekuwa wanafanya kwa ukawaida, wamekuwa wanaweka juhudi kidogo kwa sababu labda wanalipwa kidogo au wateja wanaowahudumia hawajali sana. Wewe kuwa kinyume, weka juhudi kubwa sana hata kama unalipwa kidogo, mpe mteja huduma bora kabisa hata kama anacholipa ni kidogo. Kwa kufanya zaidi kunakuweka wewe mbele ya wengine na hili linakutofautisha na wengine.
Jitofautishe na wengine kwa ufanyaji bora na siyo kwa kelele, jiweke kwenye nafasi ya kuonekana kwenye kundi kubwa la watu kupitia matokeo bora unayotoa na siyo kupitia kelele unazopiga. Kila mtu anaweza kupiga kelele, ni wachache pekee wanaoweza kutoa matokeo ya tofauti, kuwa mmoja wa hao wachache.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,